Swalaah Ya Adhw-Dhwuhaa: Idadi Ya Rakaa Zake, Wakati Wake Na Fadhila Zake

 

Swalaah Ya Adhw-Dhwuhaa:  Idadi Ya Rakaa Zake, Wakati Wake Na Fadhila Zake

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI 1:

 

Naomba kujuwa kuhusu swala ya Dhuhaa hii nikwa ushahidi wa rasulallahi (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? na ina rakaa ngapi na inaanzia wakati gani?

 

SWALI 2:

 

Kuna sala ya dhuha. je hii sala hii inasaliwa mwezi gani? wakati gani? na ni rakaa ngapi? na ni kwa muda gani? na ni kwa madhumuni gani

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

SwalaAh ya Dhuhaa katika Swalaah za Sunnah za Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Nufayr, kutoka kwa Abuu Dar-daa na Abuu Dharr, kutoka kwa Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: Allaa Ta’aalaa Amesema:  Ee mwana Aadam Swali kwa ajili (kutafuta radhi) Zangu, rakaa (chache) mwanzo wa mchana (Dhuhaa) Mimi Nitakuwa tosha yako wakati wa jioni" [At-Tirmidhiy Hadiyth Namba [475], Abu Daawuwd Hadiyth Namba [1289] na Shaykh Al-Albaaniy katika Ir-waaul-Ghaliyl Namba [1465].

 

 

Swalaah hii haina miezi maalumu ya kuswaliwa, bali ni kuiswali kila siku katika maisha yake Muislamu kwa mwenye kuweza. 

 

Idadi Ya Rakaa Za Swalaatudhw-Dhwuhaa:

 

Zifuatazo ni kauli za ‘Ulamaa:

   

Kauli ya kwanza: Wingi wa rakaa zake kwa mujibu wa madhehebu Maalikiyyah, Shafi’iyyah, na Hanaabilah. (ni rakaa nane) na ushahidi wao ni Hadiyth ya:

 

 

عـَن أُمِّ هـَانئ   رضي الله عنها قالت : ذَهَبتُ إلى رسول ِ الله ِ صلى الله عليه وسلم عام الفـَتْح فـَوَجـَدْتُهُ يـَغْتـَسِل فـَلـَمَّا فـَرَغَ مـِنْ غـُسْلِه صَـلى ثـَمانيَ رَكَعاتٍ، وذَلكّ الضـُّحى"  ـ متفق عليه

Ummu Haaniy (Radhwiya Allahu ‘anhaa) anasimulia ya kwamba alikwenda nyumbani kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka ulipofunguliwa mji wa Makkah akamkuta anajiosha, alipomaliza aliswali rakaa nane… na hiyo ni Dhwuhaa”

 

 

Kauli ya pili: Ni kauli ya jamhuri ya ‘Ulamaa. Wao wanasema Swalaah ya Dhuhaa haina idadi maalum kwa ushahidi wa Hadiyth ya   ‘Aaishah (Radhwiya Allahu ‘anhaa):

  

 كَان رسولُ الله ِ صـَلى الله عليه وسلم يـُصـَلْي الضُّحـَى أرْبـَعاً، ويـَزيدُ ما شـَاءَ الله ـ رواه مسلم

 Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhwuhaa nne na huongeza Alivyomwezesha Allaah”   [Muslim]

 

 

Wakati Wa Swalaatudhw-Dhwuhaa:

 

Ama kuhusu wakati wa Swalaah ya Dhwuhaa unaanza robo saa mara baada ya kuchomoza kwa jua, mpaka kabla ya kuingia kwa wakati wa adhuhuri, yaani kama robo saa hivi ili usije kuingia wakati wa makruwh (uliochukiza kuswaliwa).

 

 

Fadhila Za Swalaatudhw-Dhwuhaa

 

عـَن أبي هـُريْرَة رضيَ الله عنه قا : أوصـَانـِي خـَليلي صـَلـَّى الله عليه وسلم بـِصـِيامِ ثـَلاثـَة ِ أيـَّام ٍ مـِنْ كـُل شـَهر ، وَ ركـْعـَتي الضـُّحى، وأنْ أوتـِرَ قبلَ أنْ أرقـُـد"  متفق عليه ـ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu ‘anhu) kwamba “Ameniusia rafiki yangu Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam Swiyaam (funga) siku tatu katika kila mwezi, Rakaa mbili Dhwuhaa na niswali Witr kabla ya kulala” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 Na pia:

 

عـَن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه ، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ ،وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى))  رواه مسلم

Kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa swadaqah. Kwa hiyo kila tasbiyh (kusema ‘SubhaanaAllaah’) ni swadaqah, na kila tahmiyd (kusema ‘AlhamduliLLaah’) ni swadaqah na kila tahliyl (kusema ‘La Ilaaha Illa Allaah’) ni swadaqah  na kila takbiyr (kusema ‘Allahu Akbar’) ni swadaqah na kuamrisha mema ni swadaqah na kukataza maovu ni swadaqah na itamtosheleza (Mtu) kwa Rakaa mbili za Dhwuhaa)) [Muslim]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:

 

Kuna Du’aa Maalumu Ya Swalaah ya Dhwuhaa?

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share