Akiswali Sunnah Baada Ya Adhaan Ya Pili Itakuwa Ni Sunnah Ya Kabla Al-Fajr?

SWALI:

Assalamu Aleykum.

Shukran sana kwa juhudi munayofanya. Swali langu juu ya Sunnah kabliya ya alfjiri kuna hadith ya mtume S.A.W anasema rakaa mbili kabla ya salatul alfajri ni bora kuliko dunia na vilivyomo. Nauliza kama nikiingia msikiti baada adhan ya pili na nikaswali rakaa mbili na nikaingia swala hii itakuwa ni sunnah ya kawaida ama itakuwa ni hiyo rakaa mtume S.A.W amesema.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Sunnah ya baada ya Adhaana ya pili ya Swalaah ya Alfajiri. Amali zote ambazo Muislamu anafanya zinategemea na nia yake. Kwa minajili hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa maneno aliyosikika na 'Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu):

 

"Hakika vitendo huzingatiwa kwa nia, na kwa hakika kila mtu atalipwa kwa nia yake" (Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).

 

Kwa hiyo, jawabu lake litatokana na nia yako ni ipi wakati unataka kuswali hizo Rakaa mbili, je, nia ilikuwa unaswali kama ni Tahiyatul Masjid (Kuusalimu Msikiti), au nia ilikuwa ni Rakaa mbili za Qabliyah ambazo unazizungumzia?

Ikiwa ulikuwa umetia nia ya kuswali Tahiyyatul Masjid itachukuliwa kuwa ni hivyo na lau utakuwa umetia nia ya kuswali Rakaa mbili za kabla ya Alfajiri basi itachukuliwa kuwa ni Swalaah hiyo.

Nasaha yetu ni kuwa lau utakuwa umekwenda Msikitini mapema kwa Swalaah hiyo ni bora uswali rakaa mbili za Tahiyatul Masjid kwanza na baada ya hiyo uswali Rakaa mbili za kabla ya Alfajiri. Na lau umekwenda Msikitini na hali umechelewa na hakuna wakati wa kuswali zote mbili ni bora uswali Rakaa mbili kabla ya Alfajiri kwa kuweka nia hiyo.

 

Na baadhi ya Maulamaa wanakubali kuwa unaweza kuweka nia ya kuswali zote mbili kwa nia moja ikiwa unaona hakuna muda wa kuswali zote nne, yaani kuswali Rakaa mbili kwa nia ya kuwa ni Tahiyatul Masjid na hapo hapo ni Qabliyah na utakuwa kwa uwezo wa Allaah kuandikiwa kama umeswali Swalaah zote mbili.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share