02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kuwinda Na Hukmu Zake: Ni Wakati Gani Kuwinda Ni Marufuku?

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

الصَّيْدُ وَأَحْكَامُهُ

 

Kuwinda Na Hukmu Zake

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

02- Kuwinda Na Hukmu Zake: Ni Wakati Gani Kuwinda Ni Marufuku?

 

 

Kuwinda kwa asili yake ni halali, lakini inakuwa ni marufuku katika hali hizi zifuatazo:

 

Ya Kwanza:  Ikiwa kuwinda ni kwa kujifurahisha tu, au kujipumbaza au kucheza, na si kwa ajili ya kumchinja mnyama na kunufaika na nyama yake.  Ikiwa ni kwa lengo hilo la kujipumbaza, basi ni haramu.  Ni kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا تَتَّخِذُوا شَيْئًا فِيهِ الرُّوحُ غَرَضًا"

 

“Msikifanye kiumbe chochote chenye roho tageti ya kulengwa shabaha”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1957), An-Nasaaiy (4443) na Ibn Maajah (3187)].

 

Na imepokelewa toka kwa Sa’iyd bin Jubayr kwamba amesema: 

 

"مَرَّ ابْنُ عُمَرَ بِنَفَرٍ قَدْ نَصَبُوا دَجَاجَةً يَتَرَامَوْنَهَا ، فَلَمَّا رَأَوُا ابْنَ عُمَرَ تَفَرَّقُوا عَنْهَا ‏.‏ فَقَالَ ابْنُ عُمَرَ: مَنْ فَعَلَ هَذَا؟  إِنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَعَنَ مَنْ فَعَلَ هَذَا"

 

“Ibn ‘Umar aliwapitia watu wakiwa wamemfunga kuku huku wakimlenga shabaha kwa zamu.  Walipomwona Ibn ‘Umar walitawanyika wakamwacha.  Ibn ‘Umar akauliza:  Nani kafanya hivi?!  Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani aliyefanya hivi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1958].

 

Ya Pili:  Ikiwa mwindaji amehirimia Hajji au ‘Umrah, hapo ni haramu kwake kuwinda.  Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُمًا"

 

“Na mmeharamishiwa mawindo ya nchi kavu madamu mtakuwa katika ihraam”.  [Al-An’aam: 96].

 

Haya yashafafanuliwa katika Kitabu cha Hijjah.

 

Ya Tatu:  Ni haramu kuwinda kwenye Al-Haramayn, yaani Makkah na Madiynah hata kwa mtu ambaye hajahirimia.  Hili lishaelezwa pia kwenye Kitabu cha Hijjah.

 

Ya Nne:  Ni haramu kuwinda kinachomilikiwa na mtu mwingine.

 

 

 

Share