05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Kuwinda Na Hukmu Zake: Njia Ya Pili Ya Uwindaji: Kuwinda Kwa Kutumia Silaha Za Kuwindia Kama Pinde, Mishale Na Mfano Wake

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الصَّيْدُ وَأَحْكَامُهُ

 

Kuwinda Na Hukmu Zake

 

Alhidaaya.com 

 

 

05- Kuwinda Na Hukmu Zake: Njia Ya Pili Ya Uwindaji: Kuwinda Kwa Kutumia Silaha Za Kuwindia Kama Pinde, Mishale Na Mfano Wake.

 

[Al-Mughniy (9-301), na Al-Mufas-swal (3/14)].

 

Hakuna makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa kuhusiana na uhalali wa kula kilichowindwa kwa kutumia pinde au mishale likitajwa Jina la Allaah wakati wa kufyetuliwa. 

 

Katika Hadiyth ya ‘Adiyy bin Haatim, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 

"وَإِنْ رَمَيْتَ سَهْمَكَ فَاذْكُرِ اسْمَ اَللَّهِ ، فَإِنْ غَابَ عَنْكَ يَوْماً ، فَلَمْ تَجِدْ فِيهِ إِلَّا أَثَرَ سَهْمِكَ  فَكُلْ إِنْ شِئْتَ "

 

“Na unapofyetua upinde wako, basi litaje Jina la Allaah.  Na kama mnyama atapotea usimwone kwa siku moja, halafu usikute kwake isipokuwa athari ya  mshale wako tu, basi mle ukipenda”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5484) na Muslim (1929), na tamshi ni lake].

 

Na katika Hadiyth ya Abu Tha-‘alabah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwambia:

 

"فَمَا أَصَبْتَ بِقَوْسِكَ فَاذْكُرِ اسْمَ اللَّهِ ، ثُمَّ كُلْ.."

 

“Na yule uliyempata kwa kumlenga na mshale wako, basi litaje Jina la Allaah, kisha mle”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5487) na Muslim (1930)]

 

Kuwinda Kwa Kutumia Kipande Kizito Cha Mti Chenye Ncha Mbele "الْمِعْرَاَضُ"

 

Kinaweza kuchongwa mbele kikawa na ncha, au kufungiwa nchani kipande cha chuma chenye ncha kali na kurushiwa nacho mnyama.  Ikiwa kitampata mnyama kwa ncha yake, kikamjeruhi na mnyama akafa, basi ni halali kuliwa.  Lakini kikimpata kwa ubavu wake (ubapa) –na si kwa ncha yake- kikamuua kutokana na uzito wake, basi mnyama anakuwa na hukmu ya kuuliwa kwa kupigwa na kitu kizito, na hapo anakuwa si halali kuliwa.

 

Hii ndio kauli ya Maimamu wanne na wengineo katika Jumhuwr.  Na hii ni kwa Hadiyth ya ‘Adiyy bin Haatim aliyesema:  Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na "الْمِعْرَاضُ" akaniambia:

 

"إِذَا أَصَابَ بِحَدِّهِ فَكُلْ ، وَإِذَا أَصَابَ بِعَرْضِهِ  فَقُتِلَ فَلَا تَأْكُلْ ، فَإِنَّهُ وَقِيذٌ"

 

“Ikimpata kwa ncha yake, basi kula, lakini ikimpata kwa ubapa wake na mnyama akafa, basi usile, kwa kuwa ni mnyama aliyeuawa kwa kupigwa na kitu kizito”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2054) na Muslim (1929)].

 

Na zana au silaha zingine za kuwindia kama kipande hiki cha mti chenye ncha, ikiwa zitamuua mnyama kwa ubavu au ubapa wake bila kumjeruhi, basi mnyama si halali kuliwa.  Ni kama mshale kumpiga ndege kwa ubapa wake ukamuua, au mkuki, au singe, au upanga, vyote hivyo vikipiga kwa ubapa mnyama akafa, basi ni haramu mnyama huyo kuliwa.  Kadhalika, ikiwa silaha hizi zitampiga mnyama kwa ncha yake bila kumjeruhi lakini zikamuua kutokana na uzito wake, basi pia si halali kuliwa.  Ni hii ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"وَإِذَا رَمَيْتَ بِالْمِعْرَاضِ فَخَزَقَ فَكُلْهُ"

 

“Ukimrushia mnyama mi’iradh ikamjeruhi, basi mle”.  [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo].

 

Rasuli amefanya ncha kupenya mwili wa mnyama na kumjeruhi, ni sharti ya kuhalalika kuliwa, na kwa kuwa kama haikumjeruhi, basi inakuwa imemua kwa uzito wake, na hapo inakuwa ni kama imemuua kwa ubapa wake.  [Al-Mughniy (9/305) pamoja na nyongeza kidogo]

 

 

 

Share