01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Vinywaji: Taarifu Yake, Uhalali Wake, Na Hukmu Yake Kisharia

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

العَقِيْقَةُ

 

‘Aqiyqah (Akika)

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

01-‘Aqiyqah (Akika): Taarifu Yake, Uhalali Wake, Na Hukmu Yake Kisharia:

 

 

Asili yake ni neno "العَقُّ" lenye maana ya mpasuko na mkato.  Mnyama anayechinjwa huitwa ‘aqiyqah kwa kuwa koo lake hupasuliwa na kukatwa.  Pia, unywele unaotoka juu ya kichwa cha mtoto anayezaliwa toka tumboni mwa mama yake huitwa hivyo, ni sawa mtoto wa wanadamu au wa wanyama.

 

Ama kiistilahi, ni mnyama anayechinjwa kwa mtoto mchanga kwa ajili ya kumshukuru Allaah Ta’aalaa kwa niya na masharti maalum.

 

·        Uhalali Wake Na Hukmu Yake Kisharia:

 

‘Aqiyqah ni jambo lililoruhusika kisharia kwa mujibu wa kauli ya ‘Ulamaa wote akiwemo Ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar na ‘Aaishah pamoja na Fuqahaa wa Kitaabi’iyna na Aimmatul Amswaar .  Na hii ni kwa dalili hizi zifuatazo:

                                                                                                                                     

1-  Hadiyth ya Salmaan bin ‘Aamir, amesema:  “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"مَعَ الْغُلاَمِ عَقِيقَتُهُ ، فَأَهْرِيقُوا عَنْهُ دَمًا ، وَأَمِيطُوا عَنْهُ الأَذَى ‏"‏ ‏

 

“Sambamba na kila mtoto (anayezaliwa) pana mnyama wake wa ‘aqiyqah.  Basi mwageni damu kwa niaba yake, na mwondosheeni adha”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq, ikiwa imepitishwa (5472), Ahmad ( 4/18), An-Nasaaiy (7/164), Abu Daawuwd (2839) na At-Tirmidhiy (1515)].

 

2-  Hadiyth ya Abu Hurayrah, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَعَ الْغُلَامِ عَقِيقَةٌ ، فَأَهْرِيقُوا عَنْهُ دَمًا ، وَأَمِيْطُوْا عَنهُ الْأَذَى"

 

“Sambamba na kila mtoto (anayezaliwa) pana mnyama wa ‘aqiyqah.  Basi mwageni damu kwa niaba yake, na mwondosheeni adha”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Barraaz (1236) na Al-Haakim (4/238)].

 

3-  Hadiyth ya Samurah bin Jundub, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"كُلُّ غُلاَمٍ رَهِينَةٌ بِعَقِيقَتِهِ ، تُذْبَحُ عَنْهُ يَوْمَ سَابِعِهِ ، وَيُحْلَقُ ، وَيُسَمَّى"

 

“Kila mtoto ni rehani kwa mnyama wake wa aqiyqah, huchinjiwa siku yake ya saba, hunyolewa na hupewa jina”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2838), An Nasaaiy (7/166), At-Tirmidhiy (1522), Ibn Maajah (3165) na wengineo].

 

4-  ‘Aaishah amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"عَنِ اَلْغُلَامِ شَاتَانِ مُكَافِئَتَانِ ، وَعَنْ اَلْجَارِيَةِ شَاةٌ "

 

“Mtoto wa kiume huchinjiwa kondoo wawili wenye umri sawa, na binti kondoo mmoja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ahmad (6/31), At-Tirmidhiy (1513), na Ibn Maajah (3163)].

 

5-  Ibn ‘Abbaas amesema: 

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَقَّ عَنِ الْحَسَنِ وَالْحُسَيْنِ كَبْشًا كَبْشًا"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwachinjia (‘aqiyqah) Al-Hasan na Al-Husayn kila mmoja beberu mmoja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2841), An-Nasaaiy (7/166) na wengineo.  Hadiyth hii ina wenza wengi].

 

Al-Hasan na Daawuwd wanaona kwamba ‘aqiyqah ni waajib kutokana na amri zilizomo ndani ya baadhi ya Hadiyth hizi.  Lakini Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanaona kwamba ‘aqiyqah ni jambo lililosuniwa.  Na hii ni kwa Hadiyth hii ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَنْ وُلِدَ لَهُ وَلَدٌ فَأَحَبَّ أَنْ يَنْسُكَ عَنْ وَلَدِهِ فَلْيَفْعَلْ"

 

“Mwenye kuruzukiwa mtoto na akapenda kumfanyia swadaqah mtoto wake huyo, basi afanye”.  Wameifanya Hadiyth hii kuwa imeondosha na kufuta amri  zilizomo kwenye Hadiyth zilizotangulia.

                                                           

 

 

 

 

 

 

Share