03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji:Aqiyqah (Akika): Mnyama Anayetosheleza Kwa ‘Aqiyqah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

العَقِيْقَةُ

 

‘Aqiyqah (Akika)

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

03-‘Aqiyqah (Akika): Mnyama Anayetosheleza Kwa ‘Aqiyqah:

 

 

Tumeitaja Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:

 

"عَنِ اَلْغُلَامِ شَاتَانِ مُكَافِئَتَانِ ، وَعَنِ اَلْجَارِيَةِ شَاةٌ "

 

“Mtoto wa kiume achinjiwe kondoo wawili wenye umri sawa, na binti kondoo mmoja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ahmad (6/31), At-Tirmidhiy (1513), Ibn Maajah (3163)].

 

Kwa mujibu wa Hadiyth hii, wa kiume ni kondoo wawili, na wa kike ni kondoo mmoja.  Ni kauli ya Wanachuoni wengi akiwemo Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah.  Pia ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq na Abu Thawr.  [Al-Mughniy (9/363) na Al-Mawsuw’ah (30/279)].

 

Baadhi ya ‘Ulamaa akiwemo Ibn ‘Umar wamesema kuwa inatosheleza kondoo mmoja kwa mtoto wa kiume na kondoo mmoja kwa mtoto wa kike.  Dalili yao ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَقَّ عَنِ الْحَسَنِ وَالْحُسَيْنِ كَبْشًا كَبْشًا"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwachinjia (‘aqiyqah) Al-Hasan na Al-Husayn kila mmoja beberu mmoja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2841), An-Nasaaiy (7/166) na wengineo.  Hadiyth hii ina wenza wengi].

 

                                                           

 

 

 

 

 

Share