05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji:‘Aqiyqah (Akika): Miongoni Mwa Hukumu Za ‘Aqiyqah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

العَقِيْقَةُ

 

‘Aqiyqah (Akika)

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

05-‘Aqiyqah (Akika): Miongoni Mwa Hukumu Za ‘Aqiyqah:

 

 

1-  Wakati Wake:

 

Ni Sunnah mtoto achinjiwe siku yake ya saba ya kuzaliwa.  Ni kwa Hadiyth ya Samurah bin Jundub:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الغُلاَمُ رَهِينَةٌ بِعَقِيقَتِهِ ، تُذْبَحُ عَنْهُ يَوْمَ سَابِعِهِ ، وَيُحْلَقُ ، وَيُسَمَّى"

 

“Mtoto ni rehani kwa mnyama wake wa aqiyqah, huchinjiwa siku yake ya saba, hunyolewa, na hupewa jina”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2838), An Nasaaiy (7/166), At-Tirmidhiy (1522), Ibn Maajah (3165) na wengineo].

 

Kama siku ya saba itapita, basi iwe siku ya kumi na nne, na hii nayo ikipita, basi iwe siku ya ishirini na moja.  Wameyasema haya Mahanbali na Is-haaq.  Kadhalika, limesimuliwa hili toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa).

  

Wengine wamesema kuwa ikiwa atachinjiwa kabla ya siku saba au baada yake, basi itatosheleza, kwa kuwa makusudio yanapatikana.

 

Nao Mashaafi’iy kwa upande wao, wanasema kwamba ‘aqiyqah haipiti kwa kuichelewesha, lakini imestahabiwa kuwa isicheleweshwe zaidi ya umri wa kubaleghe.  Kama itacheleweshwa mpaka akabaleghe, basi hukumu yake itadondoka kwa baba wa mtoto, naye mtoto atakuwa na khiyari ya kujichinjia mwenyewe.  [Al-Mughniy (9/364) na Al-Mawsuw’ah (30/278)].

 

2-  Kuchinja Mnyama Ni Bora Zaidi Kuliko Kutoa Thamani Yake:

 

Kwa kuwa tendo la kuchinja na kumwagika damu ndilo linalokusudiwa, kwani tendo hilo ni ‘ibaadah iliyofungamanishwa pamoja na Swalaah kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:

 

"فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ"

 

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja”.  [Al-Kawthar: 02].

 

Isitoshe, kuchinja ni mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini pia ni Sunnah yake ambayo hatutakiwi tujiengue nayo.

 

3-  Haiswihi Kushirikiana Mnyama Mmoja Katika ‘Aqiyqah:

 

Mnyama mmoja hatoshelezi isipokuwa kwa mtu mmoja tu.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَعَ الْغُلاَمِ عَقِيقَتُهُ ، فَأَهْرِيقُوا عَنْهُ دَمًا ، وَأَمِيطُوا عَنْهُ الأَذَى‏"

Sambamba na kila mtoto (anayezaliwa), pana mnyama wake wa ‘aqiyqah.  Basi mwageni damu kwa niaba yake, na mwondosheeni adha”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma].

 

Na kauli yake nyingine:

 

 "كُلُّ غُلاَمٍ رَهِينَةٌ بِعَقِيقَتِهِ ، تُذْبَحُ عَنْهُ يَوْمَ سَابِعِهِ ، وَيُحْلَقُ ، وَيُسَمَّى"

 

“Kila mtoto ni rehani kwa mnyama wake wa ‘aqiyqah, huchinjiwa siku yake ya saba, hunyolewa, na hupewa jina”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma kidogo].

 

Kwa mujibu wa Hadiyth hizi, ni kuwa kila mtoto achinjiwe mnyama wake anayemhusu yeye tu, na hakuna ruhusa yoyote iliyowekwa ya kushirikiana watu mnyama mmoja kama ilivyo kwenye wanyama wa kuchinja kwenye Hijja au udhwhiyah.

 

4-  Hakuna Hadiyth Yoyote Swahiyh Inayozuia Kuvunja Mifupa Ya Mnyama Wa ‘Aqiyqah:

 

Hakuna pia hata ukaraha wa hilo, hakuna lolote lililothibiti kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala hata amri ya kumtuma mwanaume aende kwa mkunga (kupeleka nyama).

 

5-  Kichanga Hakigusishwi Chochote Katika Damu Ya Mnyama:

 

Hili ni katika ada na desturi za kijahilia ambalo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilikataza, na akalibadili hilo kwa kumnyoa kichwa, na kutoa swadaqah ya fedha kwa uzito wa nywele zake.  Al-Buraydah (Radhwiya Allaah ‘anhu amesema:

 

"كُنَّا فِي الْجَاهِلَيَّةِ إِذَا وُلِدَ لِأَحَدِنَا غُلَامٌ ، ذَبَحَ شاةً وَلَطَّخَ رَأْسَهُ بِدَمِهِ ، فَلَمَّا جَاءَ الْإِسْلَامُ كُنَّا نَذْبَحُ الشَّاةَ يَوْمَ السَّابِعِ ، وَنَحْلِقُ رَأْسَهُ ، وَنُلَطِّخُهُ بِزَعْفَرَانٍ"

 

“Tulikuwa wakati wa ujahilia, anaporuzukiwa mmoja wetu mtoto, anachinja kondoo na kukipaka kichwa chake (mtoto) damu yake (kondoo).  Na Uislamu ulipokuja, tukawa tunachinja kondoo siku ya saba (ya kuzaliwa mtoto), tunanyoa kichwa chake, na tunakipaka zafarani”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2843), At-twahhaawiy (1/460) na Al-Haakim (4/238)].

 

‘Aaishah (katika Hadiyth ya ‘aqiyqah) amesema:

 

"وَكَانَ أَهْلُ الجَاهِلِيَّةِ يَجْعَلُوْنَ قُطْنَةً فِي دَمِ العَقِيْقَةِ ، وَيَجْعَلُوْنَهُ عَلَى رَأْسِ الصَّبِي ، فَأَمَرَ رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُجْعَلَ مَكَانَ الدَّمِ خَلُوْقًا"

 

“Watu wa enzi ya ujahilia, walikuwa wakichovya pamba kwenye damu ya mnyama wa ‘aqiyqah, kisha huipaka juu ya kichwa cha mtoto.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja kuamuru liwekwe nukato lolote zuri mahala pa damu (kichwani)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Hibaan (1057) na Al-Bayhaqiy (9/303)].

 

6-  Inapendeza Kuipika Nyama Badala Ya Kuitoa Mbichi:

 

Sababu ya hili ni kuwaondoshea masikini na majirani gharama za kupika.  Na hii ni nyongeza ya ihsani kwao sambamba na kuishukuru zaidi neema hii, mbali na kuwa kielelezo cha tabia njema na utoaji.

 

                                               

Share