05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Haijuzu Kumiliki Pombe Wala Kummilikisha Mwingine

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

005-  Vinywaji: Haijuzu Kumiliki Pombe Wala Kummilikisha Mwingine:

 

Ni haramu kwa Muislamu kumiliki au kumilikisha pombe kwa sababu yoyote kati ya sababu za umiliki wa kihiari au wa mtu mwenyewe kutaka.  Ni kama kuuza, au kununua, au kutunuku na mfano wake.  Ni kutokana na neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إِنَّ الَّذِي حَرَّمَ شُرْبَهَا حَرَّمَ بَيْعَهَا ‏"

“Hakika Yule Aliyeharamisha kuinywa, Ameharamisha (pia) kuiuza”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1579), An-Nasaaiy (4664) na Ad-Daaramiy (2103)].

 

Jaabir kasema:  “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"إِنَّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ حَرَّمَ بَيْعَ الْخَمْرِ وَالْمَيْتَةِ وَالْخِنْزِيرِ وَالْأَصْنَامِ"

 

“Hakika Allaah na Rasuli Wake Wameharamisha kuuza pombe, mfu, nguruwe na masanamu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2236) na Muslim (1581)].

 

·        Mtu Akiharibu Pombe Ya Mtu, Je, Atalipa?

 

Fuqahaa wamekubaliana kwamba ikiwa pombe ni mali ya Muislamu, basi atakayeiharibu halipi.  Lakini wamekhitalifiana kuhusu aliyeharibu pombe ya asiye Muislamu anayeishi chini ya utawala wa Kiislamu (dhimmiy).  Mahanafiy na Wamaalik wamesema atalipa!!  Na Mashaafi’iy na Mahanbali wamesema hatalipa, kwa kuwa haina sifa ya kutiwa thamani kama zilivyo najisi nyinginezo.

 

 

Share