08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Hukmu Ya Vinywaji Viwili Vilivyochanganywa

 

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

 

Alhidaaya.com 

 

           

 

 

008- Vinywaji: Hukmu Ya Vinywaji Viwili Vilivyochanganywa:

 

Haijuzu kuchanganya vitu viwili vinavyolowekeka ndani ya maji kama “busr” na “rutwab”, au “tamr” (tende kavu) na zabibu kavu, hata kama havitakuwa na ukali.  Ni kwa Hadiyth ya Abu Qataadah aliyesema:

 

"نَهَى النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُجْمَعَ بَيْنَ التَّمْرِ وَالزَّهْوِ، وَالتَّمْرِ وَالزَّبِيبِ، وَلْيُنْبَذْ كُلُّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا عَلَى حِدَةٍ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuchanganya kati ya tende mbivu na mbichi, na tende mbivu na zabibu kavu.  Kila kimoja cha viwili kitayarishwe kivyake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5173) na Muslim (1987)].

 

“Rutwab” ni awamu na nne ya tunda la mtende kabla ya kukomaa na kuwa “tamr”.

 

Jaabir bin ‘Abdullaah:

 

"َأَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى أَنْ يُخْلَطَ الزَّبِيبُ وَالتَّمْرُ ، والْبُسْرُ وَالتَّمْرُ "

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuchanganya zabibu kavu pamoja na tende kavu (tamr mbivu), na “busr” pamoja  na tende kavu (mbivu)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1986)].

 

“Busr” ni tunda na mtende kati ya “Balah” na “Rutwab”.

 

Mantiki ya kukataza mchanganyo huo ni kwamba nguvu ya kulewesha huzalikana haraka sana kabla ya kutaghayuri, na hapo mnywaji atadhani kwamba kinywaji hakileweshi, hali ya kuwa kinalewesha.  Kwa ajili hiyo, Rasuli amekataza hilo ili kuziba njia ya kuingia humo.

 

Maalik ameharamisha mchanganyo huo wa vitu viwili hata kama hauleweshi.  Pia ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq na Ibn Hazm ambaye amehusisha hilo na aina zilizotajwa tu pasi na nyinginezo.

 

Ama Jumhuwr, wao wanasema kwamba ni makruhu madhali kinywaji hakijafikia nguvu ya kulewesha, lakini kama kitafikia nguvu hiyo, basi hapo kinakuwa ni haramu.  Na Mahanbali wameiawilisha kauli ya Ahmad (Rahimahul Laah) isemayo: “Michanganyo miwili ni haramu” kuwa kwa maana ya: “Kinywaji kikiwa kikali na chenye nguvu ya kulewesha”.

 

Ama Abu Haniyfah, yeye anaona kwamba hakuna ubaya wowote wa kunywa mchanganyo wa vitu viwili madhali haukufikia nguvu ya kulewesha, kwa kuwa kila kimoja kinayeyuka chenyewe, na kwa hivyo si makruhu.  Maneno yake yametolewa dalili na yaliyosimuliwa toka kwa Hadiyth Dhwa’iyf ya ‘Aaishah aliyesema:

 

"كُنَّا نَنْبِذُ لِرَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سِقَاءٍ ، فَنَأْخُذُ قَبْضَةً مِنْ تَمْرٍ أَوْ قَبْضَةً مِنْ زَبِيبٍ فَنَطْرَحُهَا فِيهِ ، ثُمَّ نَصُبُّ عَلَيْهِ الْمَاءَ فَنَنْبِذُهُ غُدْوَةً فَيَشْرَبُهُ عَشِيَّةً ، وَنَنْبِذُهُ عَشِيَّةً فَيَشْرَبُهُ غُدْوَةً"

 

“Tulikuwa tukimtengenezea Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kinywaji cha zabibu (au tende) katika kiriba cha ngozi.  Tunachukua teko moja la tende mbivu au teko moja la zabibu kavu tukalitupia humo, kisha tunamiminia maji.  Tunatengeneza hivyo asubuhi mapema, na yeye akanywa jioni, au tunatengeneza hivyo jioni, na yeye akanywa asubuhi”.  Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, imekharijiwa na Ibn Maajah (3398), na haifai kutolewa hoja.

 

Ninasema:  “Katazo linahukumia uharamisho madhali hakuna kauli nyingine ya kuondosha uharamisho huo.  Halafu, kila mtu anajua kwamba ukiwemo ulewesho, basi kinywaji ni haramu, ni sawa kikiwa kimetengenezwa kutokana na mchanganyo wa vitu viwili, au kitu kimoja peke yake”.

 

 

Share