10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: (Vinywaji) Kuvuta Sigara

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الأَشْرِبَةُ

 

Vinywaji 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

010- Vinywaji: Kuvuta Sigara:

 

Sigara (tumbaku) ilipoingia mwanzoni mwa karne ya 11  Hijria, na baadhi ya watu wakaanza kuitumia, Fuqahaa walikhitalifiana kuhusiana na hukmu yake.  Kuna waliosema kuwa ni haramu, wengine wakasema ni makruhu, na wengine wakasema ni halali.

 

Lakini kiufupi, tunasema kwamba sigara ni haramu, kwa kuwa sababu zote za kuiharamisha zipo na za kutosha.  Sababu zenyewe ni:

 

1-  Inasababisha viungo kuchoka na mwili kupooza.  Na Rasuli amekataza kutumia kitu kama hicho. 

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ نَهَى عَنْ كُلِّ مُسْكِرٍ وَمُفَتِّرٍ "

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila chenye kulewesha, na kila chenye kupoozesha nguvu za viungo vya mwili”.  [Isnaad yake ni dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3686) na Ahmad (6/254)].  

 

2-  Sigara ni katika vitu vichafu na hususan tunapokuta kwamba tumbaku yake ni lazima iloweshwe kwa pombe kiwandani katika mchakato wa kuitengeneza.  Kwa picha hii, mtu mwenye akili zake hawezi kuona kwamba sigara ni katika vitu vizuri.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ"

 

Na Anawaharamishia vilivyo vibaya”.  [Al-A’araaf: 157].

 

3-  Madhara ya sigara kwa mwili wa mwanadamu yameshaonekana kutokana na mada za sumu zilizomo ndani yake kama nicotine, lami na nyinginezo ambazo husababisha saratani ya mapafu na koo.  Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لاَ ضَرَرَ وَلاَ ضِرَارَ"

 

“Ni marufuku kujidhuru au kusababishiana madhara”.  [Hadiyth Hasan].

 

4-  Ni israfu na upotezaji wa mali.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kuchukizwa kwake na suala la utumiaji vibaya wa mali. 

 

"كَرِهَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِضَاعَةَ الْمَالِ ‏"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anachukizwa na ufujaji wa mali”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (477) na Muslim (1715)].

 

Hakuna tofauti katika ufujaji kati ya kutupa mali baharini au kuichoma moto.

 

·        Faida:

 

Jarida la “La Vest” la tiba lilichapisha makala kuhusu uvutaji sigara.  Makala hiyo inasema:  “Utafiti wa kisasa uliofanywa nchini Marekani, umefikia matokeo yale yale waliyoyafikia wataalamu nchini Uingereza.  Ni kwamba akina mama wanaovuta sigara wana hatari ya kufikia mapema mno umri wa kukatikiwa na hedhi, na majaribio waliyofanyiwa wanawake 3500 nchini Marekani walio katika umri wa kati (kuanzia miaka 40 kwenda juu), yamethibitisha pia matokeo hayo.

 

 

 

Share