01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji: Vyombo Na Yanayohusiana

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَطْعِمَةِ وَالأَشْرِبةِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِمَا

 

 Kitabu Cha Vyakula Na Vinywaji Na Yanayohusiana Na Viwili Hivi

 

 

الآنِيَةُ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهَا

 

Vyombo Na Yanayohusiana 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

001- Vyombo Na Yanayohusiana

 

1-  Asili katika vyombo ni halali kuvitumia ila vile ambavyo vimeharamishwa na Aayah au Hadiyth.  Na hii ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

" هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا"

 

Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbieni vyote vilivyomo ardhini”.  [Al-Baqarah: 29]. 

 

2-  Hairuhusiwi kulia au kunywea chombo cha dhahabu au fedha (silver)

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"لَا تَشْرَبُوا فِي آنِيَةِ الذَّهَبِ والْفِضَّةِ، وَلَا تَلْبَسُوا الحَرِيْرَ وَالدِّيْبَاجَ، فَإِنَّهَا لَهُمْ فِي الدُّنْيَا، وَلَكُمْ فِي الْآخِرَةِ "

 

“Msinywe kwa kutumia vyombo vya dhahabu na fedha, na wala msivae hariri nyepesi na nzito, kwa sababu hivyo ni vyao hapa duniani, na ni vya kwenu akhera”.  [Al-Bukhaariy (5633) na Muslim (2067)].

 

Na amesema tena:

 

"الَّذِي يَشْرَبُ فِي إِنَاءِ الْفِضَّةِ إِنَّمَا يُجَرْجِرُ فِي بَطْنِهِ نَارَ جَهَنَّمَ "

 

“Yule ambaye ananywea kwenye chombo cha fedha, hakika si vinginevyo, anangurumisha ndani ya tumbo lake Moto wa Jahannam”.  [Al-Bukhaariy (5634) na Muslim (2065)].

 

3- Vyombo vya makafiri, kama havikupatikana vinginevyo, basi vitaoshwa tu na kutumiwa kwa kulia

 

Ni kwa neno la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia Abu Tha-’alabah Al-Khushaniy:

 

"أمَّا مَا ذَكَرْتَ مِنْ أَنَّكَ بِأَرْضِ قَوْمِ أَهْلِ كِتَابٍ تَأْكُلُ في آنِيَتِهِمْ ، فَإِنْ وَجَدْتُمْ غَيْرَ آنِيَتِهِم فَلَا تَأْكُلُوا فِيهَا ، وَإِنْ لَمْ تَجِدُوا فَاغْسِلُوْهَا ثُمَّ كُلُوا فِيهَا"

 

“Ama uliyoeleza kuhusu kwamba wewe uko kwenye nchi ya Watu wa Kitabu na unakula kwa kutumia vyombo vyao, ikiwa mtapata vyombo vingine visivyo vyao, basi msile kwa kutumia vyao, lakini kama hamkupata vingine, basi viosheni na kisha mvilie”.  [Al-Bukhaariy (5488) na Muslim (1930)].

 

4-  Ni muhimu na vizuri sana kufunika vyombo, kuziba midomo ya viriba, vyungu na mfano wake na kupigia Bismil Laah kabla ya kulala.

 

 Ni kwa neno lake (Rasuli Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"إِذَا كَانَ جُنْحُ اللَّيْلِ، أَوْ أَمْسَيْتُمْ، فَكُفُّوا صِبْيَانَكُمْ، فَإِنَّ الشَّيَاطِينَ تَنْتَشِرُ حِينَئِذٍ، فَإِذَا ذَهَبَ سَاعَةٌ مِنَ اللَّيْلِ فَحُلُّوهُمْ، فَأَغْلِقُوا الأَبْوَابَ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ، فَإِنَّ الشَّيْطَانَ لاَ يَفْتَحُ بَابًا مُغْلَقًا، وَأَوْكُوا قِرَبَكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ، وَخَمِّرُوا آنِيَتَكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ ، وَأَطْفِئُوا الْمَصَابِيْحَ عِنْدَ الرَّقَادِ ، فَإِنَّ الْفُوَيْسِقَةَ رُبَّمَا اجْتَرَّتِ الفَتِيْلَةَ ، فَأَحْرَقَتْ أّهْلَ البَيْتِ ْ"

 

“Sehemu ya usiku inapoanza kuingia -au mnapoingiliwa na jioni- basi wafungieni watoto wenu ndani, kwa sababu mashetani wakati huo hutawanyika.  Na wakati kidogo wa usiku ukipita, basi waachilieni.  Na fungeni pia milango na lidhukuruni Jina la Allaah (wakati wa kufunga), kwani shetani hawezi kufungua mlango uliofungwa.  Na fungeni viriba vyenu na lidhukuruni Jina la Allaah (wakati wa kufunga).  Na funikeni vyombo vyenu na litajeni Jina la Allaah (wakati wa kufunika).  Na zimeni vibatari wakati wa kulala, kwa sababu vinyama viovu vinaweza kuchomoa utambi na kuuburura ukawachomea watu nyumba”.  [Al-Bukhaariy (6295) na Muslim (2012) na Abu Daawuwd (5103].

 

 

Share