006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Kuvaa Mavazi Mahsusi Kwa Wanawake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

006-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Kuvaa Mavazi Mahsusi Kwa Wanawake:

 

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba ni haramu mwanaume kujifananisha na mwanamke katika mavazi ambayo ni mahsusi kwa wanawake na kinyume chake.  Kuna Hadiyth kadhaa zilizothibiti ambazo zinaharamisha kiujumla kila jinsia kujifananisha na nyingine katika mambo maalum yanayohusiana na kila upande.  Na hii inajumuisha kujifananisha katika mavazi, mapambo, uzungumzaji, utembeaji na mfano wa hayo.   Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

1-  Ibn ‘Abbaas amesema:

 

"لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمُتَشَبِّهِينَ مِنَ الرِّجَالِ ِبِالنِّسَاءِ ، والْمُتَشَبِّهَاتِ مِنَ النِّسَاءِ بِالرِّجَالِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake, na wanawake wanaojifananisha na wanaume”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5885), At-Tirmidhiy (2784), Abu Daawuwd (4097) na Ibn Maajah (1904)].

 

2-  Abu Hurayrah:

 

" أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَعَنَ الرَّجُلَ يَلْبَسُ لِبْسَ الْمَرْأَةِ ، وَالْمَرْأَةَ تَلْبَسُ لِبْسَ الرَّجُلِ"

 

“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanaume anayevaa kivazi cha kike, na mwanamke anayevaa kivazi cha kiume”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4098) na Ahmad (2/325)].

 

Na laana haiwi isipokuwa kwa jambo lililoharamishwa, na hii ni kauli ya Jumhuwr.

 

Ash-Shaafi’iy amesema:  “Haikatazwi, bali ni makruhu!!  Lakini Hadiyth tajwa zinamjibu kauli yake hii.  Na kwa ajili hiyo, An-Nawawiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Lililo sawa ni kwamba wanawake kujifananisha na wanaume na kinyume chake ni haramu kutokana na Hadiyth Swahiyh”.  [Al-Majmuw’u (4/335)].

 

·        Kushusha Nguo Chini Ya Vifundo Vya Miguu Na Kuiburura Kwa Kiburi Ni Haramu

 

1-  Ibn ‘Umar:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يَنْظُرُ اَللَّهُ إِلَى مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلَاءَ" 

 

“Allaah Hamwangalii mwenye kuiburura nguo yake kwa kiburi na kujiona”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5784) na Muslim (2085)].

 

Abu Hurayrah:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يَنْظُرُ اَللَّهُ يَوْمَ القِيَامَةِ إِلَى مَنْ جَرَّ إِزَارَهُ بَطَرًا"

 

“Allaah Hatomwangalia Siku ya Qiyaamah mwenye kuburuza kikoi chake kwa kiburi”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5788) na Muslim (2087)].

 

Abu Hurayrah (pia):  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"بَيْنَمَا رَجُلٌ يَمْشِي فِي حُلَّةٍ، تُعْجِبُهُ نَفْسُهُ مُرَجِّلٌ جُمَّتَهُ، إِذْ خَسَفَ اللَّهُ بِهِ، فَهُوَ يَتَجَلَّلُ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ"

 

“Katika wakati ambapo mtu mmoja alikuwa anatembea akiwa amevalia maridadi kabisa, akijiona yeye ndiye yeye hakuna zaidi yake, amezichana vizuri kabisa nywele zake, mara ghafla Allaah Akamzamisha chini.  Naye anadidimia na kuendelea kuzama mpaka Siku ya Qiyaamah”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5789) na Muslim (2088)].

 

Hadiyth hizi zote pamoja na nyinginezo, zinaashiria uharamu wa kuburuza nguo kwa kiburi na kujiona, na kwamba mwenendo huo ni katika madhambi makubwa.

                                                                       

·        Hukmu Ya Kuteremsha Nguo Chini Ya Vifundo Vya Miguu Bila Kukusudia Kiburi:

 

Abu Hurayrah:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَا أَسْفَلَ مِنَ الْكَعْبَيْنِ مِنَ الْإِزَارِ فِي النَّارِ"

 

“Sehemu ya kikoi (nguo) iliyo chini ya vifundo viwili vya miguu, itaadhibiwa motoni”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5787), An-Nasaaiy (5331), Abu Daawuwd (4093) na Ibn Maajah (3573)].

 

Al-Khattwaabiy amesema:  “(Rasuli) anamaanisha hapa kwamba sehemu ambayo inafikiwa na kikoi (nguo) baada ya vifundo viwili vya miguu, ndiyo ambayo itakuwa kwenye moto.  Nguo imefanywa kinaya kwa mwili wa mvaaji.  Na maana yake ni kuwa sehemu hiyo ya mguu iliyo chini ya vifundo viwili ndiyo itakayounguzwa motoni..  ”.  [Fat-hul Baariy (10/257)].

 

Ibn ‘Umar:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلَاءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَة"، فَقَالَ أَبُو بَكْرٍ : يَا رَسُولَ اللَّهِ ، إِنَّ أَحَدَ شِقَّىْ إِزَارِي يَسْتَرْخِي، إِلاَّ أَنْ أَتَعَاهَدَ ذَلِكَ مِنْهُ، فَقَالَ: "إِنَّكَ لَسْتَ مِمَّنْ يَفْعَلُ ذلِكَ خُيَلَاء"َ

 

“Mwenye kuiburuza nguo yake kwa kiburi na kujiona, Allaah Hatomtazama Siku ya Qiyaamah”.  Abu Bakr akasema:  Ee Rasuli wa Allaah,  upande mmoja wa izari yangu unateremka chini, nami nalichunga hilo kwa kuupandisha.  Akasema:  “Lakini wewe si katika ambaye anafanya hivyo kwa kiburi na kujiona”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5784), An-Nasaaiy (3553) na Abu Daawuwd (4085)].

 

Kundi la baadhi ya ‘Ulamaa limeshika msimamo wa kuharamisha kuteremsha nguo chini ya mafundo mawili ya mguu ikiwa ni kwa kiburi na kujiona, na kama itakuwa kwa jingine, basi ni makruhu.  Wanasema kwamba Hadiyth zilizokuja kuhusiana na katazo la kushusha nguo chini ya vifundo ni “Mutwlaq” (yaani hazikuainisha kama ni kwa kibr au la), hivyo basi ni lazima ziainishwe kwa kufungamanishwa na kuteremsha nguo kwa kiburi na kujiona tu!!  Hivi ndivyo Ash-Shaafi’iy  alivyoeleza juu ya makundi.  [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (14/62)].

 

Lakini wengine wameshika mrengo wa kwamba haijuzu kwa mwanaume kuishusha nguo yake chini ya vifundo, halafu adai na kusema:  “Mimi siibururi kwa ajili ya kiburi na kujiona, mimi sina sifa hiyo”.  Madai haya hayakubaliki, bali hata kurefusha tu nguo yake ikagusa chini kunaonyesha kwamba ana kibr”.     [Fat-hul Baariy (10/263)].

 

Ninasema:  “Mrengo huu wa mwisho una nguvu zaidi, nao unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Jaabir bin Sulaym At-Twawiyl ambapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"وَارْفَعْ إِزَارَكَ إِلَى نِصْفِ السَّاقِ ، فَإِنْ أَبَيْتَ فَإِلَى الْكَعْبَيْنِ ، وَإِيَّاكَ وَإِسْبَالَ الإِزَارِ فَإِنَّهَا مِنَ الْمَخِيلَةِ، وَإِنَّ اللَّهَ لاَ يُحِبُّ الْمَخِيلَةَ"

 

“Na nyanyua izari yako hadi kwenye nusu ya muundi, na kama huwezi, basi hadi kwenye vifundo vya miguu.  Na tahadhari na kuteremsha izari chini ya vifundo vya miguu, kwani kufanya hivyo ni kiburi na kujiona, na Allaah kwa hakika Hapendi kiburi na mtu kujiona”.  [Swahiyh Bituruqihi.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4084), Ibn Hibaan (522), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (9691) na Ahmad (5/63)].

 

Hapa Rasuli amekufanya kule tu kushusha nguo chini ya vifundo ni kiburi na kujiona kulikoharamishwa.  Hivyo basi, ujumbe hapa ni kuwa, kuteremsha nguo chini ya vifundo viwili vya mguu ni haramu, na afanyaye hivyo, atastahiki kuadhibiwa sehemu iliyo chini ya vifundo vya miguu miwili motoni (kama ilivyoeleza Hadiyth ya Abu Hurayrah).  Lakini pamoja na hivyo, kitendo hiki hakiingii ndani ya duara la madhambi makubwa ambayo yatamkosesha mtu kuangaliwa na Allaah Siku ya Qiyaamah isipokuwa tu kama atakusudia kiburi na kujiona kwa kufanya hivyo. 

 

Ama Hadiyth ya Abu Bakr, inavyoonekana ni kuwa, yeye hakuwa anaiteremsha izari yake chini ya vifundo, bali ilikuwa yenyewe inashuka na yeye anaipandisha,  hivyo Hadiyth haiwezi kuleta utata kwa yaliyotangulia.

 

·        Je, Kurefusha Mikono Ya Kanzu Zaidi Ya Kipimo Kunaingia Kwenye Hukmu Ya Kushusha Izari Chini Ya Vifundo?

 

Inavyoonekana ni kwamba mwenye kurefusha mikono ya kanzu (nguo) ikapitiliza kuliko ilivyozoeleka, basi anaingia ndani ya hukmu ya kushusha nguo chini ya vifundo vya miguu.  ‘Ayyaadh amenukuu toka kwa ‘Ulamaa wakisema kwamba ni karaha kwa kila kilichopitiliza ada, pamoja na urefu na upana uliozoeleka kwenye mavazi.

 

Ninasema:  “Haya yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar, kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"الْإِسْبَالُ فِي الْإِزَارِ وَالْقَمِيصِ وَالْعِمَامَةِ ، مَنْ جَرَّ مِنْهَا شَيْئًا خُيَلَاءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ"

 

“Kuteremsha nguo zaidi ya mpaka unaotakiwa (isbaal), kunajumuisha izari, kanzu (shati) na kilemba.  Basi yeyote atakayeburuza chochote katika hivi kwa kiburi na kujiona, basi Allaah Hatomwangalia Siku ya Qiyaamah”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4094), An-Nasaaiy (5334), na Ibn Maajah (3576).  Angalia Al-Mishkaat (4332)]. 

 

Na Ibn Al-Qayyim ameeleza kwamba haikuwa katika mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuvaa mikono mipana na mirefu kupitiliza, kamwe hakuvaa yeye wala yeyote katika Maswahaba wake.  Kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Sunnah yake, kama ambavyo kujuzisha hilo hakubebi vigezo vyovyote imara, hiyo ni sehemu ya kiburi na kujiona tu na si vinginevyo, lakini pia ni upotezaji mali, kwani anaweza kushona nguo nyingine kutokana na ziada za mikono hiyo.

 

 

 

Share