010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa: Nguo Ya Rangi Ya Zafarani

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

010-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Vivazi Vilivyokatazwa Kwa Wanaume Kuvivaa:  Nguo Ya Rangi Ya Zafarani:

 

 

 

‘Abdullaah bin ‘Amri amesema: 

 

"رَأَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَىَّ ثَوْبَيْنِ مُعَصْفَرَيْنِ فَقَالَ ‏: "‏إِنَّ هَذِهِ مِنْ ثِيَابِ الْكُفَّارِ فَلاَ تَلْبَسْهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nimevaa nguo mbili za rangi ya zafarani.  Akaniambia:  Hakika hizi ni katika nguo za makafiri, basi usizivae”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2077)].

 

Na katika riwaayah amesema: 

 

 "أَأُمُّكَ أَمَرَتْكَ بِهَذَا؟"‏ قُلْتُ أَغْسِلُهُمَا‏.‏ قَالَ: ‏"‏بَلْ أَحْرِقْهُمَا"

 

“Je, ni mama yako amekuamuru kufanya hivi?!  Nikasema:  Nitazitoa rangi.    Akasema:  Bali zichome moto”. 

 

Maana ya swali la (Rasuli): Je, ni mama yako aliyekuamuru kufanya hivi?!, ni kuwa haya ni katika mavazi ya wanawake, mapambo yao na tabia zao.  Ama amri ya kuzichoma moto, ‘Ulamaa wamesema ni adhabu na shadidio ili aonyeke na waonyeke wengineo kufanya mfano wa kitendo hicho.  [Sharhu Muslim].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib: 

 

أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَى عَنْ لُبْسِ الْقَسِّيِّ ، والمُعَصْفَرِ، وَعَنْ تَّخَتُّمِ الذَّهَبِ ، وَعَنْ قِرَاءَةِ القُرْآنِ في الرُّكُوْعِ"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kuvaa nguo iliyotengenezwa kwa kitani na hariri, nguo ya rangi ya zafarani, kuvaa pete ya dhahabu, na kusoma Qur-aan kwenye rukuu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2078), At-Tirmidhiy (264) na An-Nasaaiy (1041)].

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu suala la nguo ya zafarani, nayo ni ile yenye rangi ya kinjano.  Jumhuwr ya ‘Ulamaa wamejuzisha  kuvaa akiwemo Shaafi’iy, Maalik na Abu Haniyfah!!  Ama kundi jingine la ‘Ulamaa, wao wamesema ni makruhu karaha hafifu “tanziyh” kutokana na yaliyothibiti toka kwa Ibn ‘Umar akisema:

 

"رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَصْبُغُ بِالصُّفْرَةِ"

 

“Nilimwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitia rangi ya kinjano”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5851) na Muslim (1187)].

 

Ama Al-Khattwaabiyy, yeye amesema katazo linaelekezwa kwenye nguo iliyotiwa rangi hiyo baada ya kufumwa.  Ama ile ambayo nyuzi zake zimetiwa rangi kisha ikafumwa, basi hiyo haiingii kwenye katazo.

 

Kadhalika, ‘Ulamaa wengine wamelichukulia katazo kwa aliyehirimia Hajji au ‘Umrah ili liowane na Hadiyth ya Ibn ‘Umar kuhusiana na yaliyoharamishwa kuvaa kwa aliyehirimia.  [Sharhu Muslim (14/54)].

 

Ninasema:  “Linaloonekana kuwa na nguvu, ni kwamba haijuzu kuvaa nguo iliyotiwa rangi ya kinjano kutokana na Hadiyth zilizothibiti na hususan ikiwa rangi yenyewe imekoza sana hadi kufanana na nguo za akina mama.  Na kwa ajili hiyo, Al-Bayhaqiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Lau kama Hadiyth hizi zingelimfikia Ash-Shaafi’iy, basi angelizisema..”. 

 

Ama Hadiyth ya Ibn ‘Umar, Hadiyth hii haikutaja ni kitu gani alichokitia rangi Rasuli, je ni nguo, au nywele au ndevu.  Hivyo, inaweza kuchukulika kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitia rangi nywele zake au nguo zake.  Lakini pia, unjano unaozungumziwa kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Umar unaweza kuchukuliwa kuwa si ule wa kukoza wa kufanana na nguo za wanawake.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

 

Share