014-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Pambo La Nywele

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

014-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:  Pambo La Nywele:

 

 

 

Inapendeza kwa mwenye nywele azihifadhi kwa kuzisafisha na kuziweka kwenye mwonekano mzuri, azienzi, azichane, azipake mafuta na kadhalika.

 

Bibi ‘Aaishah amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا كَانَ لأَحَدِكُمْ شَعْرٌ فَلْيُكْرِمْهُ"

 

“Mmoja wenu akiwa na nywele, basi azienzi na kuzitunza”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4163) na An-Nasaaiy (8/183)].

 

Haitakikani mtu aziachilie nywele zake mpaka ziwe kwenye hali mbaya, bali azipake mafuta, azilainishe kwa maji na mfano wake na azichane.   Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu mmoja nywele zake zimemsimama akasema:

 

"أَمَا كَانَ يَجِدُ هَذَا مَا يُسَكِّنُ بِهِ شَعْرَهُ"

 

“Je hawezi huyu kupata chochote cha kulainishia nywele zake?”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4062) na An-Nasaaiy (8/183)].

 

Imesuniwa mtu anapochana nywele zake aanzie upande wa kulia wa kichwa chake kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia.

 

"كَانَ اَلنَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ‏يُعْجِبُهُ اَلتَّيَمُّنُ فِي تَنَعُّلِهِ، وَتَرَجُّلِهِ، وَطُهُورِهِ، وَفِي شَأْنِهِ كُلِّهِ"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa kunampendeza kuanza kwa kulia akivaa viatu, akichana nywele, akijitwaharisha, na katika mambo yake yote”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (426) na Muslim (268)]

 

Na ikiwa anazitunza vyema nywele zake, basi itapendeza aziwache ziwe ndefu na aziteremshie hadi kwenye mabega yake.  Anas amesema:

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَضْرِبُ شَعْرَ رَأْسِهِ مَنْكِبَيْهِ"

 

“Kwamba nywele za Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zikigusa mabega yake mawili”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5904)].

 

‘Aaishah kasema:

 

"كَانَ لِرَسُوْلِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ شَعْرٌ دُونَ الْجُمَّةِ وَفَوْقَ الوَفْرَةِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na nywele zilizoning’inia juu kidogo ya mabega mawili, na chini kidogo ya ndewe za masikio”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Maajah (3635) na At-Tirmidhiy (1755)].

 

Haitakikani nywele kuwa ndefu zaidi ya kipimo hiki, na hii ni kwa sababu mbili:

 

Ya kwanza:  Kunamuingiza mtu katika duara la kujifananisha na wanawake.

 

Ya pili:  Ni kwa yaliyopokelewa toka kwa Sahl bin Al-Handhwaliyyah, amesema:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"نِعْمَ الرَّجُلُ خُرَيْمٌ الْأَسْدِيُّ ، لَوْلَا طُولُ جُمَّتِهِ وَإِسْبَالِ إِزَارِهِ ، فَبَلَغَ ذَلِكَ خُرَيْمًا ، فَأَخَذَ شَفْرَةً فَقَطَعَ بِهَا جُمَّتَهُ إِلَى أُذُنَيْهِ ، وَرَفَعَ إِزَارَهُ إِلَى أَنْصَافِ سَاقَيْهِ"

 

“Khuraym Al-Asdiyyu angelikuwa ni mtu bora kabisa lau kama si kurefusha nywele zake chini ya ndewe na kuburuza izari yake. Khuzaym akasikia habari hiyo, hapo hapo akachukua mkasi akakata nywele zake hadi kufikia masikioni, na akanyanyua izari yake hadi kwenye miundi”.  [Isnaad Layyin.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4089), Ahmad (4/179), na At-Twabaraaniy (6/94)]. 

 

·        Angalizo:

 

Ama yaliyothibiti kwamba:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنِ التَّرَجُّلِ إِلاَّ غِبًّا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuchana sana nywele isipokuwa muda baada ya muda”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (8/132), At-Tirmidhiy (1756) na Abu Daawuwd (4159).  Iko kwenye Swahiyhul Jaami’u (6870)].

 

Makusudio ya hili ni mtu asipumbazike sana na nywele na kupoteza wakati mwingi kuzishughulikia.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

·        Kunyofoa Mvi Ni Haramu:

 

Toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb, toka kwa baba yake toka kwa babu yake toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا تَنْتِفُوا الشَّيْبَ ، فَإِنَّهُ نُورُ الْمُسْلِمِ يَوْمَ القِيَامَةِ"

 

“Msinyofoe mvi, kwani mvi ni nuru ya Muislamu Siku ya Qiyaamah”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4202) na At-Tirmidhiy (2821)].

 

Toka kwa Anas: 

 

"كُنَّا نَكْرَهُ أَنْ يَنْتِفَ الرَّجُلُ الشَّعْرَةَ الْبَيْضَاءَ مِنْ رَأْسِهِ وَلِحْيَتِهِ"

 

“Tulikuwa hatupendi mwanaume kunyofoa mvi za kichwa chake na ndevu zake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2341)].

 

·        Kutia Rangi Nywele:

 

Inaruhusiwa kubadili rangi ya mvi, lakini si kwa rangi nyeusi.  Toka kwa Jaabir, amesema: 

 

"أُتِيَ بِأَبِي قُحَافَةَ يَوْمَ فَتْحِ مَكَّةَ وَرَأْسُهُ وَلِحْيَتُهُ كَالثُّغَامَةِ بَيَاضًا ، فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: غَيِّرُوا هَذَا بِشَيْءٍ وَاجْتَنِبُوا السَّوَادَ"

 

“Abu Quhaafah aliletwa Siku Makkah ilipokombolewa kichwa chake na ndevu zake zikiwa nyeupe mithili ya hisopo.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:  Badilisheni hizi kwa kitu chochote, lakini epukeni rangi nyeusi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2102), An-Nasaaiy (5076) na Abu Daawuwd (4204)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kwenda kinyume na Mayahudi na Manaswara akisema:

 

"إِنَّ الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى لاَ يَصْبُغُونَ فَخَالِفُوهُمْ"

 

“Hakika Mayahudi na Manaswara hawatii rangi nywele (wala ndevu), basi nendeni kinyume nao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5899) na Muslim (2103)].

 

Rangi inabadilishwa kwa kutumia hina, “katam” (mimosa flava) na mfano wake.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ أَحْسَنَ مَا غُيِّرَ بِهِ الشَّيْبُ الْحِنَّاءُ وَالْكَتَمُ"

 

“Hakika kitu bora zaidi cha kubadilishia rangi mvi ni hina na “katam (mimosa flava)”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Asw-Swahiyhah (1509).  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1573), An-Nasaaiy (8/139), na Ibn Maajah (3622).  Kuna mvutano kwenye Sanadi yake].

 

Ama kutia rangi nyeusi, hili haliruhusiwi, ni marufuku kabisa.  Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) aliyesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"يَكُونُ فِي آخِرِ الزَّمَانِ قَوْمٌ يَخْضِبُونَ بِالسَّوَادِ كَحَوَاصِلِ الْحَمَامِ ، لَا يَرِيحُونَ رَائِحَةَ الْجَنَّةِ"

 

“Watakuja watu zama za mwisho, watatia nywele zao (na ndevu) rangi nyeusi mithili ya vifua vya njiwa, hao hawatainusa harufu ya Pepo”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4212), An-Nasaaiy (8/138), na Ahmad (1/273).  Iko katika Swahiyhul Jaami’i (8153)].

 

Na pia kwa Hadiyth nyingine iliyotangulia:

 

"غَيِّرُوا هَذَا بِشَيْءٍ وَاجْتَنِبُوا السَّواد"

 

“Badilisheni hizi kwa kitu chochote, lakini epukeni rangi nyeusi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2102), An-Nasaaiy (5076) na Abu Daawuwd (4204)].

 

Faida:

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kunyofoa mvi lakini hakukataza kuzitia rangi, kwa kuwa kunyofoa kunabadili umbile lake la asili kinyume na kutia rangi ambako hakugeuzi umbile kwa mwenye kuziangalia.

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kwamba sharia imeruhusu kuzificha mvi kwa kuzitia rangi kwa ajili ya maslaha mengine ya kidini, nayo ni kuwavunja nguvu maadui na kuwaonyesha ukakamavu na ungangari mbele yao.  [‘Awnul Ma’abuwd (11/171)].

 

·        Ni Haramu Kunyoa Ndevu:

 

Kunyoa ndevu kwa wanaume ni haramu kwa ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa.  Kwa kuwa kuzinyoa ni kubadili uumbaji wa Allaah, kumtii shetani, kukhalifu agizo la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuzifuga na kuziachilia, kujifananisha na makafiri, na kujifananisha pia na wanawake.  Dalili juu ya hayo zimetajwa kwenye Kitabu Cha Twahara.

 

·        Kukata Sharubu Na Kulipunguza:

 

Kukata sharubu na kulipunguza ni katika sunnah za maumbile asilia, lakini pia ni ukamilisho wa pambo la mwanaume.  Abu Hurayrah amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الْفِطْرَةُ خَمْسٌ : الْخِتَانُ، وَالاِسْتِحْدَادُ، وَنَتْفُ الإِبْطِ، وَتَقْلِيمُ الأَظْفَارِ، وَقَصُّ الشَّارِبِ"

 

“Maumbile asili ni katika (mambo) matano:   Kutahiriwa, kunyoa kinena, kunyofoa kikwapa, kukata kucha na kukata sharubu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5891) na Muslim (257)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَحْفُوا الشَّوَارِبَ" 

 

“Punguzeni sharubu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5892) na Muslim (259)].

 

Na katika riwaayah:

 

"جُزُّوا الشَّوَارِبَ"

 

“Kateni masharubu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (260)].

 

Pia amesema:

 

"مَنْ لَمْ يَأْخُذ مِنْ شَارِبِهِ فَلَيْسَ مِنَّا"

 

“Yeyote ambaye hapunguzi chochote katika sharubu lake, basi si katika sisi”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (1/15), At-Tirmidhiy (2761) na Ahmad (4/368).  Iko kwenye Swahiyhul Jaami’i (6533).

 

Makusudio hapa ni kukata sharubu zenye kuota juu ya mdomo wa juu na si kuzifyeka zote, na pia kuzikata kabisa toka kwa juu zile zinazoangukia kwenye wekundu wa mdomo kwa namna isiyosababisha kero kwa mlaji wala kukusanyika uchafu.

 

Imesemwa pia kwamba makusudio ni kuondosha nywele zote ziotazo kwenye mdomo wa juu.  Kauli zote mbili zinabebwa na dalili, na pia hupatikana kwazo lengo la kuwakhalifu Wamajusi, mbali na  kusalimika mlaji na adha ya nywele na kukusanyia uchafu.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Muislamu anatakikana asiache sharubu kwa zaidi ya siku 40.  Na hii ni kwa Hadiyth ya Anas aliyesema:

 

"وُقِّتَ لَنَا فِي قَصِّ الشَّارِبِ وَتَقْلِيمِ الْأَظْفَارِ وَنَتْفِ الْإِبِطِ وَحَلْقِ الْعَانَةِ أَنْ لَا تُتْرَكَ أَكثر من أَرْبَعِينَ لَيْلَة"

 

“Tumewekewa sisi muda katika kukata sharubu, kukata kucha, kunyofoa nywele za kwapa, na kunyoa kinena kwamba visiachwe hivyo zaidi ya siku 40”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (257)].

 

·        Ni Marufuku Kunyoa Denge (Panki)

 

Ibn ‘Umar amesema: 

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kunyoa denge”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5920) na Muslim (113)].

 

Denge ni kunyoa sehemu ya kichwa na kuacha nyingine.  Vijana wengi wa Kiislamu wameingia kwenye mtihani huu wakiwaiga kibubusa Mayahudi na Manaswara. 

 

 

 

Share