007-Al-A'raaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

007-Al-A’raaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 206

 

Jina La Suwrah: Al-A’raaf

 

Suwrah imeitwa Al-A’raaf (Mnyanyuko), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila. Na pia kutajwa Al-A’raaf katika Aayah namba (46-48). Nao ni mnyanyuko wa watu watakaokuwa baina ya Jannah na moto.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kushinda haki katika mapambano yake ya baatwili, na kubainisha mwisho wa watu wenye kiburi duniani na Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha na kuthibitisha ‘Aqiydah na suala la Tawhiyd na shirk.

 

3-Kubainisha ‘Aqiydah ya kufufuliwa na marejeo ya viumbe kwa Allaah na hesabu Siku ya Qiyaamah.

 

4-Kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na kukanushwa kwake na makafiri.

 

5-Kubainishwa hukmu na sharia kwa ujumla, na kwamba Mwenye kutunga sharia ni Mwenye Muumbaji Allaah (سبحانه وتعالى), kama mfano sharia ya kuchukua mapambo Misikitini na kula na kunywa vitu vizuri vilivyo halali, na kukemea mapambo yaliyoharamishwa. Na umuhimu wa kutafakari Aayaat na Ishara, Dalili zinazohusu Uumbaji Wake Allaah (سبحانه وتعالى) na fadhila Zake juu ya Waja Wake..

 

6-Kubainisha suala la Rusuli kuhusu kufikisha Risala (Ujumbe) ambao umeelezwa katika Suwrah iliyopita. Na suala la majibizano baina ya Rusuli na kaumu zao.

 

7-Kubainisha kuwa malipo ni kutokana na juhudi na matendo ya mwanaadam. Na kuthibitisha hoja za watu Jannah kwa watu wa motoni.  Na kuonya kwamba Siku ya Qiyaamah itakuja kwa ghafla, na Suwrah ilionya juu ya muda huo maalumu uliopangwa na kukadiriwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayah namba (4).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha ikabainisha Utukufu wa Kitabu cha Allaah na kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa asitie shaka katika kufikisha Risala kwa watu na kuwaonya, na kwamba ni ukumbusho kwa Waumini.

 

2-Kuna maharamisho ya kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى), na kuwasimamishia washirikina hoja ya kwamba Allaah ni Mmoja tu! Na kuwaonya washirikina kwamba, watakuwa na mwisho mbaya hapa duniani na Aakhirah, na kuelezea juu ya kile kitachowatokea washirikina na wale waliowakadhibisha Rusuli wa Allaah.

 

3-Imetajwa uzito wa mizani za matendo siku ya Qiyaamah, na kuwakumbusha watu juu ya neema ya kuumbwa ardhi, na kumfanya mwanaadam awe mnufaika namba moja wa kheri za ardhini.

 

4-Imeelezea kuumbwa kwa Aadam, na kukataa kwa Ibliys kumsujudia (Aadam), na Ibliys kuwatia wasiwasi na kuwashawishi Aadam (عليه السّلام) na mkewe ili wale mti waliokatazwa. Kisha muendelezo uliopo juu ya uadui wa shaytwaan kwa mwanaadam. Na watu kutahadharishwa wasijitie katika udanganyifu na hila za shaytwaan kutokana na kuwataka kwake wajinyime mambo ya kheri, na kutumbukia katika yale yanayowasukuma kwenye adhabu huko Aakhirah.

 

5-Kuna maelezo ya vitisho vya Siku ya Malipo kwa waovu, na Ukarimu wa Allaah kwa wamchao Yeye (سبحانه وتعالى).  

 

6-Kimetajwa Kisa cha Asw-haabul-Al-A’raaf (watu walio kati muinuko kati ya watu wa Jannah na watu wa motoni), na kuwakumbusha watu kufufuliwa na kukaribia ishara zake.

 

7-Kuna makatazo juu ya kufanya ufisadi katika ardhi. Ardhi ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameiweka kwa faida na maslahi kwa wanaadam.

 

8-Imetajwa sehemu ya visa vya Rusuli wa Allaah katika kulingania kaumu zao washirikina, na kauli za kila Rasuli kwa kaumu zao, na majibu ya washirikina ambayo ni ya ukaidi, inadi na upingaji Risala ya Allaah, na maudhi waliyopata Rusuli wa Allaah kutoka kaumu zao. Imeanza kisa cha Nabiy Nuwh (عليه السّلام). Kisha kisa cha Nabiy Huwd (عليه السّلام) na kuangamizwa kwa watu wa ‘Aad. Kisha kisa cha Nabiy Swaalih (عليه السّلام) na jeuri za watu wa Thamuwd. Kisha kisa cha Nabiy Luutw (عليه السّلام) na watu wake. Kisha kisa cha Nabiy Shu’ayb na watu wa Madyan.

 

9-Kuna vitisho kwa wanaojiaminisha na makri za Allaah (kwa kuwa Allaah Analipiza makri za waovu), na kuwaonya kwamba wasidanganyike kwa kuona Allaah Anawapa muhula wale wanaomuasi kabla adhabu haijawashukia. Hivyo basi ni fursa yao kuacha ukafiri na ukaidi wao kwani adhabu huwajia kwa ghafla baada ya muhula huo.

 

10-Imeelezewa sehemu ya kisa cha Muwsaa (عليه السّلام) kwa tafsili, yakiwemo maelezo ya wachawi na kuomba uokovu wana wa Israaiyl. Ametajwa Haruwn (عليه السّلام) ambaye ni ndugu wa Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na kuhusu pindi alipomwachia awaongoze wana wa Israaiyl, na Miyqaat (sehemu na wakati) ya Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) kukutana na Allaah. Ikafuatia maelezo ya kuabudiwa ndama na mtu aliyeitwa Saamiriyy ambaye aliwapotosha watu kumwabudu ndama.

 

11-Imetajwa bishara ya kutumwa kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)  na wasifu wa Ummah wake, na fadhila ya Dini hii tukufu.

 

12-Mna kisa cha As-Sabt; Mayahudi kuvua samaki siku ya Jumamosi ambamo walikatazwa lakini wakavua samaki kwa ujanja, basi Allaah Akawageuza manyani.

 

13-Kuna mawaidha kwa washirikina kugeuza kwao Tawhiyd ya Allaah na kuingia katika shirki. Allaah (سبحانه وتعالى) Anakumbusha watu kuhusu ahadi ya Alastu, ambayo kila binaadam alifungamana na Allaah wakati walikuwa katika Fitwrah (maumbilie ya asili ya kumpwekesha Allaah) kabla ya kuzaliwa kwao. Ni Ahadi ya kutokumshirikisha Allaah, basi wasije watu Siku ya Qiyaamah kudai kuwa hawakukumbushwa.

 

14-Ametajwa mtu aliyepewa ilimu lakini shaytwaan akamshawishi akafuata matamanio yake akapotoka. Basi ni hilo ni funzo kwa watu watafakari na watahadhari.

 

15-Kuna maelezo kuhusu shirki za washirikina, na kwamba waabudiwa wao hawawezi kuumba kitu wala hawawezi kuwanusuru au kuwaitikia wito wao. Hayo ni kinyume na Tawhiyd ya Allaah kwani Allaah Ana Majina Mazuri kabisa na Sifa Zake Zilotukuka ambazo Waumini wameamrishwa watumie katika duaa zao.

 

17-Kuna Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waislamu; wawe na subra na kuendeleza wito, na kuwaonya juu ya uchochezi wa shaytwaan.

 

18-Suwrah imekhitimiswa kwa amri ya kuomba kinga dhidi ya shaytwaan katika kuanza kusoma Qur-aan, na kuisikiliza kwa makini ili imteremkie msomaji, Rehma ya Allaah. Na kumcha Allaah kwa kumdhukuru kwa siri na dhahiri bila ya kughafilika Naye, na kuendelea kumwabudu. Na ikabainishwa kwamba Malaika hawafanyi kiburi kwa kuacha kumwabudu Allaah, bali wao wanaandamana na Amri Zake, wanamtakasa mchana na usiku, na wanamwepusha na mambo yasiyonasibiana na Yeye, na kwamba wanamsujuduia Yeye Peke Yake. Na hapo kuna alama ya Sajdah At-Tilaawa (Sijda ya kusoma Qur-aan).

 

Fadhila Za Suwrah:  

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Aliisoma Suwrah Al-A’raaf Katika Swalaah Ya Maghrib:

 

عن عائِشةَ رَضِيَ اللهُ عنهاأنَّ رَسولَ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسَلَّم قَرَأَ في صلاةِ الـمَغرِبِ بسورةِ الأعرافِ؛ فَرَّقَها في رَكعتَينِ

Amesimulia ‘Aaisha (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma katika Swalaah ya Maghrib Suwrah Al-A’raaf na akaigawa katika rakaa mbili. [An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy]

 

حَدَّثَنَا أَبُو عَاصِمٍ، عَنِ ابْنِ جُرَيْجٍ، عَنِ ابْنِ أَبِي مُلَيْكَةَ، عَنْ عُرْوَةَ بْنِ الزُّبَيْرِ، عَنْ مَرْوَانَ بْنِ الْحَكَمِ، قَالَ قَالَ لِي زَيْدُ بْنُ ثَابِتٍ مَا لَكَ تَقْرَأُ فِي الْمَغْرِبِ بِقِصَارٍ، وَقَدْ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ بِطُولِ الطُّولَيَيْنِ

Amesimulia Marwaan Bin Al-Hakam (رضي الله عنه): Zayd bin Thaabit aliniambia: “Kwa nini unasoma Suwrah fupi sana katika Swalaah ya Maghrib, ilhali nilimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Suwrah ndefu kati ya Suwrah mbili ndefu?” [Al-Bukhaariy]

 

 

Share