013-Ar-Ra'd: Utangulizi Wa Suwrah

 

013-Ar-Ra’d: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa. Rejea Faida.
 

Idadi Za Aayah: 43

 

Jina La Suwrah: Ar-Ra’d

 

Suwrah imeitwa Ar-Ra’d (Radi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (13) kuwa radi inamsabihi (Allaah) na kumhimidi, na Malaika pia (wanamsabihi) kwa sababu ya kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwaraddi wanaopinga Wahy na Unabii kwa kuwabainishia mambo yanayoonyesha Uadhimu wa Allaah (سبحانه وتعالى). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Suwrah inathibitisha nguzo tatu za ‘Aqiydah katika nyoyo za Waumini; Allaah (Mtumaji Risala), Rasuli (Mfikishaji Risala kwa watu) na Risala yenyewe (Qur-aan).

 

3-Suwrah inatoa hoja mbali mbali kwa makafiri kwa dalili na ushahidi wa wazi kabisa za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na uumbaji wa ulimwengu na viliomo. Na ikatoa baadhi ya dalili kwa mifano kadhaa.

 

4-Kubainisha haki na baatwil; kwamba haki imeimarika na yenye nguvu hata ikifichwa. Na baatwil ni dhaifu haina nguvu wala thamani hata kama ikidhihirika kwa wingi ikatanda na kuenea. Basi baatwil itatoweka tu na haki itahakiki na kuthibitika.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa ya kwamba Qur-aan ni ya kweli na imetoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) lakini watu wengi hawaiamini.

 

2-Zimetajwa dalili za wazi kudhihirisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Qudra Yake; kuumba mbingu na ardhi, jua na mwezi, usiku na mchana, Mwenye kujaalia mazao ya aina mbali mbali yanayonyeshewa kwa maji ya aina moja tu! Rejea Aayah namba (4) ya Suwrah hii kwenye maelezo bayana. Na kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Muumbaji Pekee wa kila kitu, na Mwenye Kuhuisha na Kufisha na Mweza kwa kuleta manufaa na madhara.  
 

3-Imeelezea yanayohusu kauli za washirikina yanayoungamana na kufufuliwa, pamoja na kuwaraddi.

 

4-Imebainishwa ukamilifu wa Ilimu ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba Yeye (سبحانه وتعالى) ni Mjuzi wa kila kitu, ya dhahiri na ya siri.

 

5-Imethibitishwa kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayestahiki kuabudiwa na kuombwa duaa. Na kwamba waabudiwa wa washirikina na duaa zao kwao haziwafai chochote kwani waabudiwa hao hawawaitikii chochote.

 

6-Imepigwa mifano miwili ya haki na baatwil, na kuweka mafungamano kati ya mwisho wa wafuasi wa haki na wafuasi wa baatwili, pamoja na sifa zao.

 

7-Kuna amri ya kutimiza ahadi, kuunga ambayo Ameyaamrisha Allaah (سبحانه وتعالى), kumkhofu Rabb, kuogopa malipo mabaya, kuvuta subra kwa kutaka Wajihi wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa mali kwa siri na dhahiri, kulipiza mema baada ya uovu. Basi jazaa yake ni Jannah (Pepo) na maamkizi ya Salaam kutoka kwa Malaika. Na katazo la kuvunja ahadi na kutokuunga ambayo Ameyaamrisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kufanya ufisadi katika ardhi. Basi jazaa yake ni laana ya Allaah (سبحانه وتعالى) na makazi mabaya Aakhirah. Rejea Aayah (21-25) na faida zake.

 

8-Imeelezea baadhi ya rai za makafiri na matakwa yao ya kiburi na fitnah, na kuwaraddi.

 

9-Imebainishwa mwisho mwema kwa wenye taqwa, na mwisho mbaya kwa wanaomkadhibisha Allaah (سبحانه وتعالى).

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kumliwaza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na kukanushwa kwake na watu wake; washirikina wa Makkah. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Anamthibitishia kwamba Yeye Anamtosheleza kuwa Shahidi wake juu ya urongo wao, na ushahidi wa wenye ilimu ya Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Manaswara walioamini Unabii wake, wakatoa ushahidi bila kuuficha.

 

Faida:

 

1-‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu wapi kuteremka kwake. Wapo wanaosema imeteremka Makkah kutokana na maudhui na sifa za Suwrah zilizoteremshwa Makkah ambazo zinataja shirki, makafiri kutokuamini kufufuliwa, kukadhibisha Risala ya Allaah na jazaa zao motoni. Na baadhi ya ‘Ulamaa wamesema imeteremka Madiynah.

 

2-Ni Suwrah mojawapo inayotaja dalili za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kina zaidi.

 

3-Imetajwa Jina la Suwrah (Radi) kuwa inamsabihi (Allaah) na kumhimidi na Malaika pia (wanamsabihi) kwa sababu ya kumkhofu. Na kusoma duaa mtu anaposikia radi nayo ni:

 

سُبْـحانَ الّذي يُسَبِّـحُ الـرَّعْدُ بِحَمْـدِهِ، وَالملائِكـةُ مِنْ خيـفَته.

Rejea Suwrah Ar-Ra’d (13:13)

 

 

Share