018-Al-Kahf: Utangulizi Wa Suwrah

 

018-Al-Kahf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 110

 

Jina La Suwrah: Al-Kahf

 

Suwrah imeitwa Al-Kahf (Pango), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila. Na imeitwa Al-Kahf kutokana na kisa cha Aswhaabul-Kahf (watu wa pangoni) waliotaja kuanzia Aayah namba (9).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Manhaj (njia) ya kuamiliana na fitnah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwajibika Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى) na kumshukuru kwa Neema Zake tele, kuwa na imaan na matendo mema, kuthibitisha Tawhiyd Yake (Kumpwekesha) na haramisho la kumshirikisha kwa ibaada na riyaa-a (kujionyesha).  

 

3-Kuthibitisha kufufuliwa, na adhabu za wenye kukanusha.

 

4-Mwongozo wa ‘Aqiydah sahihi na tabia njema, na mwongozo juu ya fikra salama ambayo inamfanya mtu aishi maisha mazuri ya duniani na Aakhirah.

 

5-Kubainisha Hikma ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Ujuzi Wake, na kwamba wanaadam wanatofautiana ilimu na maarifa waliyojaaliwa na Allaah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuteremsha Kitabu kwa Mja Wake Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), na kukisifu kuwa ni Kitabu kitukufu kisicho na dosari, na kwamba kinabashiria Waumini watendao mema kuwa watapata ujira mzuri, na kinawaonya wanaomsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ana mwana.

 

2-Imebainishwa kwamba vilivyopo juu ya ardhi ni pambo lake na kwamba limewekwa na Allaah (سبحانه وتعالى) ikiwa kama mtihani kwa waja.

 

3-Imetajwa kisa cha Aswhaabul-Kahf (Watu wa pangoni) ambao walithibitika katika Tawhiyd ya Allaah.

 

4-Imeamrishwa kusema In Shaa Allaah pindi mtu akitaka kufanya jambo kesho au hata baada ya muda fulani.

 

5-Imetahadharishwa fitnah ya mali kwa kutajwa kisa cha mwenye bustani mbili aliyemkufuru Rabb wake akakanusha Siku ya Qiyaamah, na adhabu yake.

 

6-Umepigwa mfano wa maisha ya dunia; mfano unaojulisha kumalizika kwake na kuondoka starehe zake.

 

7-Imetajwa baadhi ya adhabu za moto kwa madhalimu na makafiri Siku ya Qiyaamah na mateso yao na baadhi ya matukio ya Siku hiyo ya Mwisho.

 

8-Waumini wamekumbushwa kwamba, mali na watoto ni mapambo ya dunia, lakini al-baaqiyaatu asw-swaalihaatu ndio bora zaidi mtu kutarajia malipo mema kutoka kwa Allaah. Rejea Aayah (46).

 

9-Imebainishwa uadui wa Ibliys kwa Aadam na kizazi chake.

 

10-Imetajwa kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السلام) pamoja na kijana wake Yuwsha’ Bin Nuwn pamoja na kisa chake na mja aliyepewa ilimu zaidi naye ni Al-Khidhwr.

 

11-Imetajwa kisa cha Dhul-Qarnayni na kutajwa kwa Yaajuwj na Maajuwj ambao ni mmojawapo ya alama kubwa za Qiyaamah.

 

12-Suwrah imekhitimishwa kwa makemeo ya ushirikina na kubatilisha shirki, na kubainisha mazuri ya kudumu milele, Aliyoyaahidi Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waumini.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Kuhifadhi Aayah kumi za mwanzo wa Suwrah ni kinga ya Masiyh Dajjaal:

 

عن أَبي الدرداءِ رضي اللهُ عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : مَنْ حَفِظَ عَشْرَ آيَاتٍ مِنْ أَوَّلِ سُورَةِ الكَهْفِ ، عُصِمَ مِنَ الدَّجَّالِ  . رواه مسلم

Amesimulia Abuu Dardaa (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Mwenye kuhifadhi Aayah kumi mwanzo wa Suwrah Al-Kahf   ataepushwa na (Masiyh) Dajjaal.” [Muslim]

 

Na katika riwaayah nyengine Hadiyth ndefu ambayo:

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimtaja Ad-Dajjaal siku moja…. Akasema:

 

فَمَنْ أَدْرَكَهُ مِنْكُمْ فَلْيَقْرَأْ عَلَيْهِ فَوَاتِحَ سُورَةِ الْكَهْفِ إِنَّهُ خَارِجٌ خَلَّةً بَيْنَ الشَّأْمِ وَالْعِرَاقِ فَعَاثَ يَمِينًا وَعَاثَ شِمَالاً

"Atakayesalia miongoni mwenu na kumwona, amsomee Aayah za mwanzo za Suwrah Al-Kahf kwani atatokea njia baina ya Sham na Iraq na atafanya ufisadi pande za kuliani na kushotoni.” [Muslim]

 

وفي رواية :  مِنْ آخِرِ سُورَةِ الكَهْفِ  رواه مسلم

Na riwaayah nyengine: “Mwisho wa Suwrah Al-Kahf.” [Muslim]

 

 

2-Kuisoma inateremsha sakiynah (Utulivu):

 

حَدَّثَنِي مُحَمَّدُ بْنُ بَشَّارٍ، حَدَّثَنَا غُنْدَرٌ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، سَمِعْتُ الْبَرَاءَ بْنَ عَازِبٍ ـ رضى الله عنهما ـ قَرَأَ رَجُلٌ الْكَهْفَ وَفِي الدَّارِ الدَّابَّةُ فَجَعَلَتْ تَنْفِرُ فَسَلَّمَ، فَإِذَا ضَبَابَةٌ ـ أَوْ سَحَابَةٌ ـ غَشِيَتْهُ، فَذَكَرَهُ لِلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏ "‏ اقْرَأْ فُلاَنُ، فَإِنَّهَا السَّكِينَةُ نَزَلَتْ لِلْقُرْآنِ، أَوْ تَنَزَّلَتْ لِلْقُرْآنِ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abuu Is-haaq (رضي الله عنه): Nimemsikia Al-Baraa Bin ‘Aazib (رضي الله عنهما) akisema: Mtu mmoja alisoma Suwrah Al-Kahf (katika Swalaah yake), na ndani ya nyumba yake mlikuwa na mnyama. (Mnyama) akawa anaogopa na huku anarukaruka. Akatoa Salaam (kumaliza Swalaah) basi ghafla ukamfinika ukungu au wingu. Akamwelezea kisa hicho Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) basi akasema: “Soma ee fulani, kwani hiyo ni as-sakiynah (utulivu) umeteremka kwa sababu ya Qur-aan.” Au “Unateremka kwa ajili ya Qur-aan.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

3-Inamwangazia Nuru kati ya Ijumaa mbili, atakayeisoma siku ya Ijumaa:

 

 عَنْ أَبِي سَعِيدٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَمن قَرَأَ سُورَة الْكَهْف فِي يَوْم الْجُمُعَة أَضَاء لَهُ النُّور مَا بَيْنَ الْجُمْعَتَيْنِ

 

Amesimulia Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kusoma Suwrah Al-Kahf Siku ya Ijumaa, basi itamwangazia nuru ya kati ya Ijumaa mbili.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (2/368) na Al-Bayhaqiy (3/249) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (6470)]

 

Tanbihi: Baadhi ya ‘Ulamaa wameona kuwa hii ni Hadiyth dhwaiyf ila kuna ambao wameona si vibaya kuisoma kama Imaam Ibn Baaz (رحمه الله) aliposema: “Ina udhaifu lakini mtu akiisoma kutaraji fadhila zake, basi ni vizuri kwani alifanya hivo Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما).

 

Faida:

 

1-Suwrah Al-Kahf (18) ni miongoni mwa Suwrah tano zinazoanzia kwa AlhamduliLlaah. Nyenginezo ni Al-Faatihah (1), Al-An’aam (6), Saba-a (34) na Faatwir (35).

 

2-Rejea faida katika Aayah namba (23) kujua sababu ya kuteremshwa kisa cha Aswhaabul-Kahf.

 

3-Suwrah Al-Kahf ni miongoni mwa Suwrah zilizotangulia kuteremshwa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akazitaja kuwa ni pato lake la mwanzo:

 

حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، قَالَ سَمِعْتُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ يَزِيدَ، سَمِعْتُ ابْنَ مَسْعُودٍ، يَقُولُ فِي بَنِي إِسْرَائِيلَ وَالْكَهْفِ وَمَرْيَمَ وَطَهَ وَالأَنْبِيَاءِ إِنَّهُنَّ مِنَ الْعِتَاقِ الأُوَلِ وَهُنَّ مِنْ تِلاَدِي‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Yaziyd (رضي الله عنه): Nimemsikia  ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) akisema: Suwrah Bani Israaiyl, Al-Kahf, Maryam, Twaahaa na Al-Anbiyaa ndio miongoni mwa pato langu la kwanza na mali yangu kongwe, na (hakika ni) ndio mali yangu kongwe.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

 

 

Share