02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Kivazi Cha Mwanamke: Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Kwanza

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

لِبَاسُ المَرْأَةِ

Kivazi Cha Mwanamke 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

002-Masharti Ya Kivazi Cha Mwanamke Wa Kiislamu, Sharti La Kwanza:

 

 

Sharti la kwanza: 

 

Kisitiri mwili wake wote, isipokuwa ‘Ulamaa wamekhitilafiana kwa upande wa uso na viganja viwili.  Allaah Amesema:

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

 

31.  Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika.  Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake.  Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao.  Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu.  [An-Nuwr: (31)].

 

 

Na Amesema tena Ta’aalaa:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

 

59.  Ee Nabiy!  Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao.  Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe.  Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.  [Al-Ahzaab: (59)].

 

Jua kwamba ‘Ulamaa wamekubaliana kwamba ni lazima mwanamke asitiri mwili wake wote, lakini wamekuja wakakhitilafiana kwa vigezo kwa upande wa uso na viganja.

 

Kundi ambalo linaona kuwa ni lazima asitiri pia uso na viganja lina dalili zifuatazo:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ"

 

“Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia”.  [Al-Ahzaab: (53)].

 

Aayah hii iliteremka wakati Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa Zaynab bint Jahsh.  Akaalika watu, wakala, kisha wakatoka wengi wao na wakabakia baadhi wachache ambao walikaa kwa muda mrefu kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Kisha Rasuli akatoka pamoja na Zaynab na kuingia naye (chumbani) mara kadhaa ili watoke.  Na hapo ndipo iliposhuka aayah hii, na Rasuli akapiga pazia kati yake na wao.  [Sababu hii ya kuteremshwa aayah imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4791) na Muslim (1428) kutoka kwa Hadiyth ya Anas, kwa maana yake].

 

Wanasema kwamba kauli hii inawahusu wanawake wote kwa kuwa wanashirikiana wote katika sababu ya hijabu, nayo ni utwahara wa moyo.

 

2-  Kauli Yake Ta’aalaa:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

 

Ee Nabiy!  Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao.  Hivyo kunapelekea karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe.  Na Allaah daima Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [Al-Ahzaab: (59)].

 

Wamefasiri “kuteremsha jilbaab” kwenye aayah hii kwa maana ya kufunika uso na kuacha jicho moja tu wazi ili kuonea kwalo.

 

3-  Hadiyth ya Ibn Mas-‘uwd kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الْمَرْأَةُ عَوْرَةٌ فَإِذَا خَرَجَتِ اسْتَشْرَفَهَا الشَّيْطَانُ"

 

“Mwanamke ni uchi, na anapotoka nje, basi shetani humpamba (kwenye macho ya wanaume).  [At-Tirmidhiy (1173), Ibn Maajah (3/95), na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (10115).  Ni Hadiyth Swahiyh].

 

4-  Hadiyth ya kuzushiwa Bibi ‘Aaishah zinaa ambapo anaeleza:

 

"وَكَانَ صَفْوَانُ بْنُ الْمُعَطَّلِ السُّلَمِيُّ مِنْ وَرَاءِ الْجَيْشِ، فَأَصْبَحَ عِنْدَ مَنْزِلِي فَرَأَى سَوَادَ إِنْسَانٍ نَائِمٍ فَأَتَانِي فَعَرَفَنِي حِيْنَ رَآنِي، وَكَانَ يَرَانِي قَبْلَ الْحِجَابِ فَاسْتَيْقَظْتُ بِاسْتِرْجَاعِهِ عَرَفَنِي فَخمَرِتُ وَجْهِي بِجِلْبَابِي .."

 

Swafwaan bin Al-Mu’attwal As-Sulamiy alikuwa nyuma ya jeshi.  Akapambaukiwa asubuhi akiwa mbele ya hema langu, akaona weusi wa kivuli cha mtu aliyelala, akanijia, akanitambua aliponiona.  Yeye alikuwa ananiona kabla ya kuteremka amri ya kuvaa hijaab, nikaamka kutokana  na tamshi lake la kusema “Innaa LiLLaahi wa Innaa ilayhi raaji’uwn” baada ya kunitambua. Nikajifunika uso wangu kwa jilbabu yangu.”  [Al-Bukhaariy (4141) na Muslim (2770)].

 

 

5-  Hadiyth ya Asmaa bint Abiy Bakr:

 

"كُنَّا نُغَطِّيْ وُجُوْهَنَا مِنَ الرِّجَالِ ، نَمْتَشِطُ قَبْلَ ذلِكَ فِي الإحْرَامِ"

 

“Tulikuwa tunazifunika nyuso zetu wanaume wasituone, na kabla ya kufanya hivyo, tulikuwa tunachana nywele zetu katika ihraam”.  [Mustadrakul Haakim (1/454) kwa Sanad Swahiyh].

 

Ama kundi la pili la ‘Ulamaa wanaosema kwamba inajuzu kwa mwanamke kuacha wazi uso wake na viganja, na kwamba kuvisitiri viwili hivi ni jambo la sunnah na si waajib, hawa dalili zao ni hizi zifuatazo:

 

1-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا"

 

“Na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika”.  [An-Nuwr: (31)].

 

Wamesema “yanayodhihirika” ni uso na viganja.  At-Twabariy amekhitari rai hii katika tafsiyr yake (18/84).  Lakini pia kuna rai nyingine kuhusiana na hili ambapo baadhi wengine wamesema ni vile vinavyodhihiri bila mwanamke kukusudia, wengine wamesema ni nguo, wengine wanja, pete, bangili na kadhalika.

 

2-  Hadiyth (Dhwa’iyf) ya ‘Aaishah:

                         

"أَنَّ أَسْمَاءَ بِنْتَ أَبِي بَكْرٍ دَخَلَتْ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَعَلَيْهَا ثِيَاب رقاق فَأَعْرَضَ عَنهُ وَقَالَ: يَا أَسْمَاءُ إِنَّ الْمَرْأَةَ إِذَا بَلَغَتِ الْمَحِيضَ لَنْ يَصْلُحَ أَنْ يُرَى مِنْهَا إِلَّا هَذَا وَهَذَا . وَأَشَارَ إِلَى وَجْهِهِ وَكَفَّيْه"ِ

 

“Kwamba Asmaa bint Abiy Bakr aliingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa nguo nyepesi.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akageuka asimwone na akamwambia:  Ee Asmaa!  Mwanamke anapofikia umri wa kutokwa na hedhi, basi haifai aonekane chochote isipokuwa hii na hii, akaashiria uso wake na viganja vyake viwili”.  [Hadiyth Dhwa’iyf:  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4104), na kwenye sanad yake kuna kasoro nne].

 

Wametoa dalili kadhaa pia zinazogusia kwamba wanawake wa Kiislamu walikuwa wakifunua nyuso au viganja viwili mbele ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye hakuwakataza.  Kati yake ni:

 

3-  Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah kuhusu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwatolea mawaidha wanawake siku ya ‘Iyd.  Sehemu ya Hadiyth inaeleza: 

 

"فَقَامَتْ امْرَأَةٌ مِنْ سِطَةِ النِّسَاءِ سَفْعَاءُ الْخَدَّيْنِ فَقَالَتْ لِمَ يَا رَسُولَ اللَّه"

 

“Akasimama mwanamke mmoja aliyesawijika mashavu toka katikati ya wanawake akauliza:  Kwa nini ee Rasuli wa Allaah?!”   [Muslim (885), An-Nasaaiy (1/233) na Ahmad (3/318)].

 

Wamesema:  Kauli ya Jaabir “aliyesawijika mashavu”, ni dalili kwamba alikuwa hakuyafunika mashavu yake.

 

4-   Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ambapo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpandisha Fadhli bin ‘Abbaas nyuma ya mnyama wake katika Hijjah ya kuaga, na mwanamke akamuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Sehemu ya Hadiyth inasema:

 

"...فَأَخَذَ الْفَضْلُ بْنُ عَبَّاسٍ يَلْتَفِتُ إِلَيْهَا وَكَانَتِ امْرَأَةً حَسْنَاءَ ، فَأَخَذَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِذَقْنِ الْفَضْلَ ، فَحَوَّلَ وَجْهَهُ مِنَ الشِّقِّ الآخَرِ"

 

“…Al-Fadhl bin ‘Abbaas akaanza kugeuka kumwangalia, naye alikuwa mwanamke mrembo wa sura, na Rasuli akakishika kidevu cha Al-Fadhl, akaugeuza uso wake upande mwingine”.  [Al-Bukhaariy (6228) na Muslim (1218)].   ‏

 

Katika riwayaah nyingine ya Hadiyth ya ‘Aliyy bin Abiy Twaalib ni kwamba hilo lilikuwa wakati wa kuchinja baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutupia vijiwe Jamarah, kwa maana kwamba swali la mwanamke huyo lilikuwa baada ya tahallul ya ihraam (tahallul ndogo).

 

Ibn Hazm amesema:  “Na lau kama uso ungelikuwa ni uchi unaolazimu kufunikwa, basi Rasuli asingelimruhusu kuufunua mbele ya watu, na badala yake angelimuamrisha auteremshie ushungi toka juu.  Na kama uso wake ulikuwa umefunikwa, basi Ibn ‘Abbaas asingelijua kama ni mrembo wa sura au mwenye sura ya kawaida”. 

 

5-  Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

"كُنَّ نسَاءُ المؤْمِنَاتِ يَشْهَدْنَ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الصُّبْحَ مُتَلَفِّعَاتٍ بِمُرُوطِهِنَّ ، ثُمَّ يَنْقَلِبْنَ إِلَى بُيُوْتِهِنَّ حِيْنَ يَقْضِيْنَ الصَّلَاةَ ، لا يَعْرِفُهُنَّ أَحَدٌ مِنَ الْغَلَسِ"

 

“Wanawake Waumini walikuwa wakihudhuria Swalatul Fajr pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakiwa wamejitanda shungi zao, kisha huondoka haraka kurudi majumbani mwao wakati swalah inapomalizika, hawatambui yeyote sura zao kutokana na kiza”.  [Al-Bukhaariy (578) na Muslim (645)].

 

Wamesema:  Tunafahamu hapa kwamba lau si kiza, basi wangelitambulika, na kwa kawaida hutambulikana kutokana na nyuso zikiwa wazi.

 

6-  Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas pale Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowatolea wanawake mawaidha Siku ya ‘Iyd ambapo aliwahimiza watoe swadaqah.  Sehemu ya Hadiyth inasema:

 

"...وَأَمَرَهُنَّ بِالصَّدَقَةِ ، فَرَأَيْتُهُنَّ يُهْوِينَ إِلَى آذَانِهِنَّ وَحُلُوقِهِنَّ يَدْفَعْنَ إِلَى بِلَالٍ ، ثُمَّ ارْتَفَعَ هُوَ وَبِلَالٌ إِلَى بَيته"

 

“….na akawaamuru kutoa swadaqah, hapo nikawaona wakipeleka mikono kwenye masikio yao na koo zao (kutoa hereni na mikufu) na kumkabidhi Bilaal, kisha akanyanyuka yeye na Bilaal wakaenda nyumbani kwake”.  [Al-Bukhaariy (977), Abu Daawuwd (1143) na An-Nasaaiy (1/227)].

 

7-  Hadiyth ya ‘Aaishah:

 

"أَنَّ امْرَأَةً أَتَتِ النَّبِيَّ تُبَايِعُهُ، وَلَمْ تَكُنْ مُخْتَضِبَةً، فَلَمْ يُبَايِعْهَا حَتَّى اخْتَضَبَتْ"

 

“Kwamba mwanamke mmoja alimjia Rasuli wa Allaah kupeana naye ahadi  ya fungamano na Uislamu (bay-‘a), mwanamke huyo hakuwa amejipaka hina, na Rasuli hakuchukua ahadi kwake mpaka alipojitia hina”.  [Abu Daawuwd (4166) na Al-Bayhaqiy kutoka kwake (7/86).  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].  

 

Wametoa dalili vile vile kwa jumla ya aathaar zinazoelezea kufanyika matukio ambapo wanawake walikuwa hawafuniki nyuso zao wala viganja vyao baada ya enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  [Angalia kitabu cha “Jilbaabul- Mar-atil Muslimati” cha Al-Albaaniy (uk. 96)].

 

Na ijulikane kwamba kila kundi katika makundi haya mawili lina hoja pingamizi dhidi ya kila dalili ya kundi jingine, na hapa hatuna nafasi ya kuziweka kwa mapana yake, kwani ni ndefu sana.  Lakini unaweza ukaona minakasha hiyo kwa mapana zaidi katika kitabu cha “Al-Hijaab, Adillatul Muwjibiyna” cha Shaykh Mustwafa Al-‘Adawiy, kitabu cha “ ‘Awdatul Hijaab” cha Shaykh Muhammad bin Ismaa’iyl, na kitabu cha “Jilbaabu Al-Mar-atil Muslimati” cha Sheikh Al-Albaaniy.

 

Na hapa nimeleta makundi mawili pamoja na dalili zao nyingi ili kuonyesha kwamba ‘Ulamaa wamekhitilafiana kwalo tangu zamani na hadi sasa, na kwamba makhitilafiano haya si ya kihasama kiasi cha kulifanya kundi moja kulishadidia kundi jingine na kuliona limepotoka, bali kila kundi linaheshimu hoja za kundi jingine.

 

Na hapa pia tunachukua nafasi ya kuhadharisha umma na kundi la tatu ambalo Maulamaa wake si lolote si chochote, bali ni wababaishaji tu ambao wanasema kwamba mwanamke kusitiri uso wake ni bid’a na uchupaji mipaka ya dini.  Bali ujinga wa baadhi yao umefikia kutunga kitabu ambapo wanasema kwamba kusitiri uso wa mwanamke ni haramu!

 

Tunamalizia mada hii kwa kuelezea faida hizi:

 

-  ‘Ulamaa kwa pamoja wamekubaliana kwamba ni lazima mwanamke aliye huru asitiri mwili wake wote isipokuwa uso na viganja.

 

-  Kuna makhitilafiano kuhusu uso na viganja kama ilivyoelezwa.

 

-  Wenye kusema kwamba si lazima kusitiri uso, wanaona kwamba ni bora kusitiriwa na hususan katika zama za fitnah.

 

 

Share