029-Al-‘Ankabuwt: Utangulizi Wa Suwrah

 

029-Al-‘Ankabuwt: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah:  69

 

Jina La Suwrah: Al-‘Ankabuwt

 

Suwrah imeitwa Al-‘Ankabuwt (Buibui), na inayodalilisha ni kutajwa katika ayah namba (41).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Maamrisho juu ya kuvuta subira na kuthibiti wakati wa mitihani na fitnah, na kubainisha mwisho wa hayo yote. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutajwa kwamba Muumini lazima apitie mitihani ili athibitishe imaan yake, na kubainisha hali zao duniani na Aakhirah, na kubainisha kati ya Waumini wa kweli na waongo na wanafiki

 

3-Kuamrisha mema na kukataza munkari (maovu), na kujadiliana na Ahlul-Kitaab kwa njia bora.

 

4-Kuwaahidi Waumini ushindi, na kuwaahidi washirikina adhabu na kuwadhalilisha na kuwatolea mfano washirikina kuchukua walinzi wasiokuwa Allaah, ambao ni utando wa buibui, na hapa kuna marejeo ya wale wanaotegemea juu ya nguvu za sanamu.  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha ikabainishwa uhakika wa imaan, na Desturi ya Allaah ya Kuwapa mitihani Waja Wake, na kubainisha mwisho mwema wa Waumini, na mwisho mbaya wa makafiri na wanafiki.

 

2-Imetaja sehemu fulani ya nyumati za nyuma na adhabu zao. Miongoni mwao ni kaumu ya Nuwh, Ibraahiym, Luutw, Shu’ayb, Huwd, Swaalih na Muwsaa (عليهم السلام). Kisha ikabainisha aina za adhabu za kila mmoja wao na mwisho wao mbaya kwa kuwakadhibisha Rusuli hawa.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Amewapigia mfano hali ya washirikina kuwa ni sawa na buibui ambae amejijengea nyumba ambayo ni dhalili mno kuliko zote, haimkingi kwa jua wala mvua. Basi ni sawa na hao wanaowaabudu pasi na Allaah.  

 

4-Maamrisho ya kuisoma Qur-aan na kusimamisha Swalaah.

 

5-Makatazo ya kujadiliana na Ahlul-Kitaabi isipokuwa kwa njia nzuri.

 

6-Imesimamisha baadhi ya hoja na dalili ya kwamba Qur-aan imetoka kwa Allaah.

 

7-Imebainisha mapungufu ya washirikina, kwani wao wanakiri kuwa Allaah ndio Muumba wa mbingu na ardhi, lakini pamoja na hayo bado wanaendelea kumshirikisha.

 

8-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwaahidi Waumini ambao wamepigana Jihaad kwa ajili ya Allaah, watapata uongofu na watakuwa na mwisho mwema.

 

 

 

 

Share