054-Al-Qamar: Utangulizi Wa Suwrah

 

054-Al-Qamar: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 55

 

Jina La Suwrah: Al-Qamar

 

Suwrah imeitwa Al-Qamar (Mwezi), na yanayodalilisha, ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila na Faida. Na pia kwa kutajwa mwanzo kabisa Suwrah, Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ukumbusho wa neema ya Qur-aan kuwa ni nyepesi, na yaliyomo (kwenye Qur-aan) ambayo ni Aayaat (Ishara, Dalili, Miujiza, Hoja) na maonyo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Mazungumzo kuhusu Desturi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Viumbe Vyake, ambao katika madhwhari yake ya wazi kabisa, ni kuwapa ushindi Waumini, na kuwafedhehesha na kuwaangamiza makafiri.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa tanabahisho na uhakikisho wa kukaribia Qiyaamah, na ishara yake ni kupasuka kwa mwezi.

 

2-Imetajwa upingaji wa washirikina kuhusu Aayaat (Ishara, Miujiza, Dalili) za Allaah zinapowajia, kwa kukengeuka na kupuuza  na kuipachika sifa ovu Qur-aan kama vile kusema ni sihri (uchawi) ambayo wamezoea kuisikia.

 

3-Amri na liwazo kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwapuuza washirikina mpaka iwajie hukumu ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Siku ya Qiyaamah, na matukio yake watakapotoka makaburini mwao, wajute na waione siku hiyo ni ngumu mno!

 

4-Imetajwa visa vya Rusuli akianziwa Nabiy Nuwh (عليه السّلام) na kaumu yake waliomkadhibisha na kumpachika sifa ovu kumwita majnuni. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Muujiza Wake wa kufungua mbingu na ardhi, yakamiminika maji wakagharakishwa makafiri wote. Na Akamwamrisha Rasuli Wake aunde jahazi apande yeye na walioamini, wakaokolewa na gharka.

 

5-Kisha kila mwisho wa kisa cha Rasuli, Allaah (سبحانه وتعالى) Amekumbusha maonyo Yake, na Ameahidi kuiwepesisha Qur-aan kwa mwenye kutaka kuisoma na kuihifadhi na kuifahamu.

 

6-Kisha wametajwa kina ‘Aad, kaumu ya Nabiy Huwd (عليه السّلام) na kukadhibisha kwao Risala ya Allaah, na ikatajwa maangamizi yao ya upepo mkali wa dhoruba, na sauti kali iliyoendelea mfululizo hadi wakafilia mbali!

 

7-Kisha wametajwa kina Thamuwd, kaumu ya Nabiy Swaalih (عليه السّلام), na kukadhibisha kwao Risala ya Allaah, kumpachika sifa ovu Rasuli wao kuwa ni muongo mkubwa, mfidhuli na mwenye kutakabari! Juu ya hayo, walipoletewa muujiza wa ngamia jike, ambaye walitaka wenyewe wateremshiwe iwe ni Ishara ya Allaah, waliamrishwa wasimguse kwa uovu, na wafanye zamu kunywa maji ya hodhi; siku moja wao, siku moja ngamia, lakini walikataa hayo na wakamchinja ngamia wa Allaah! Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza kwa ukelele angamizi. (na tetemeko la ardhi kama ilivyotajwa katika Suwrah nyenginezo. Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye uchambuzi kuhusu nyumati za awali na aina za maangamizi yao.

 

8-Kisha wametajwa kaumu ya Nabiy Luutw (عليه السّلام) waliokadhibisha Risala ya Allaah, na kutenda machafu. Ikatajwa maangamizi yao ya kupelekewa tufani ya mawe siku moja asubuhi mapema.

 

9-Kisha ametajwa Firawni na watu wake, na kukadhibisha kwao Risala ya Allaah, na maangamizi yao (ya kugharakishwa baharini).

 

10-Imewakemea na kuwaonya washirikina kwa kutozingatia haya maonyo, na kuahidiwa adhabu dhalilifu ya kuburutwa motoni kifudifudi.

 

11-Imebainishwa Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Hikma Yake iliyokamilika, na kwamba kila kitu ni kwa Hukmu na Qadr Yake.

 

12-Imebainisha Qudra Adhimu ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uwezo  Wake wa kusimamisha Qiyaamah kwa muda wa upepeso wa jicho tu!

 

13-Imewakumbusha washirikina maangamizi ya nyumati za nyuma, na kwamba kila jambo linarekodiwa katika Kitabu cha matendo; kubwa na dogo.

 

14-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwabashiria Waumini wenye taqwa, kuwa wataingizwa katika Jannaat za mito, ambako Yuko Mfalme Adhimu, Mwenye Nguvu na Uwezo mkubwa kabisa; Allaah (عزّ وجلّ).

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiisoma katika Swalaah za ‘Iyd:

 

عَنْ أَبِي وَاقِدٍ اللَّيْثِيِّ قَالَ: { كَانَ اَلنَّبِيُّ ‏- صلى الله عليه وسلم ‏-يَقْرَأُ فِي اَلْأَضْحَى وَالْفِطْرِ بِـ (ق)‏, وَ (اقْتَرَبَتْ)‏.   أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ  

Amesimulia Waaqid Al-Laythiyy (رضي الله عنه)Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alikuwa akisoma katika (‘Iyd) Alfitwri na Al-Adhwhaa ق (Suwrah 50) na اقْتَرَبَتْ  (Suwrah 54). [Muslim]

 

Faida:

 

عَنْ أَنَسٍ، قَالَ سَأَلَ أَهْلُ مَكَّةَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم آيَةً فَانْشَقَّ الْقَمَرُ بِمَكَّةَ مَرَّتَيْنِ فَنَزَلَت: ((‏اقتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانْشَقَّ الْقَمَرُ)) ‏  إِلَى قَوْلِهِ ‏:‏ ‏ ((‏سحْرٌ مُسْتَمِرٌّ))  يَقُولُ ذَاهِبٌ ‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ ‏.

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Watu wa Makkah walimuomba  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) awaletee Aayah (Ishara, Muujiza), basi mwezi ukapasuka Makkah mara mbili (yaani sehemu mbili), kisha ikateremka:

 

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ ﴿١﴾

“Saa imekaribia na mwezi umepasuka.”

 

Mpaka Kauli Yake:

سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ ﴿٢﴾

“Sihiri ya siku zote, tumeizoea.”

[Atw-Twabaraniy na Al-Haafidhw Ibn Kathiyr amesema katika Al-Bidaayah Wan-Nihaayah:  Isnaad yake ni Jayyid]

 

 

 

 

Share