065-Atw-Twalaaq: Utangulizi Wa Suwrah

 

065-Atw-Twalaaq: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 12

 

Jina La Suwrah: Atw-Twalaaq

 

Suwrah imeitwa Atw-Twalaaq (Talaka), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (5).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha hukmu za Talaka na kuiheshimu mipaka (sharia) yake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha hukumu zinazofungamana na talaka, na yanayoambatana juu yake; eda ya talaka, kunyonyesha, matumizi na makazi ya mtaliki na mwana.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuelezewa talaka ya kisharia katika kubainishwa muda unaopaswa kumtaliki mke, na amrisho la kutokuwatoa majumbani mwao, na kutokuvuka mipaka ya Sharia za Allaah.

 

2-Imetolewa amri ya kuwafanyia wema wataliki na kushuhudisha mashahidi katika talaka, na katika kurejea.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Ameahidi kuwafanyia wepesi Waumini mambo yao, na kuwaruzuku ikiwa watamcha Yeye, na watatawakali Kwake na Amewaahidi kuwafutia madhambi yao.

 

4-Imeendelea kubainisha baadhi ya hukmu za talaka za kuwahudumia wataliki mpaka kumaliza kunyonyesha.

 

5-Imetajwa mwisho mbaya wa nyumati za nyuma waliopinga Amri za Rabb wao kuwakanusha Rusuli Wake. 

 

6-Waumini wamekumbushwa Fadhila ya Allaah ya kuwatumia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), ambaye amewasomea Aayaat za Allaah zinazofafanua haki na kutenga ubatilifu, wakaongoka na wakatolewa kutoka kizani na kuingizwa katika nuru, na wakamuamini Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Kisha yakatajwa malipo mazuri ya kuingizwa Jannaat na kuruzukiwa humo neema.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitisha Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola; Uumbaji, Uendeshaji na kadhaalika) na kubainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na upana wa Ilimu Yake.

 

 

 

 

 

 

Share