067-Al-Mulk: Utangulizi Wa Suwrah

 

067-Al-Mulk: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 30

 

Jina La Suwrah: Al-Mulk

 

Suwrah imeitwa Al-Mulk (Ufalme), na pia imeitwa Suwrah Tabaarak, na yanayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa chini katika Fadhila. Na pia kwa kutajwa kwake katika Aayah namba (1). 

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kudhihirisha ukamilifu wa Ufalme wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Nguvu Zake, jambo ambalo linapelekea kumkhofu na kuchukua tahadhari na Adhabu zake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha Uwezo Wake Mkubwa Allaah (سبحانه وتعالى) na ukamilifu wa Ufalme Wake unaojulisha Tawhiyd Yake.

 

3-Kubainisha adhabu Alizoziandaa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa wale wanaojizuia kutafakari ulimwengu. Basi hawa ndio wapotofu. Ama waliomcha Rabb wao, basi wao jazaa yao ni maghfirah, na thawabu na takrima na kuokoka na adhabu Siku ya Qiyaamah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kubainishwa Utukufu wa Allaah (تبارك وتعالى)  na Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola: Uumbaji, Uhuishaji na Ufishaji, Uendeshaji ulimwengu na kadhaalika) na pia kubainishwa baadhi ya Sifa Zake Tukufu za Uwezo Wake juu ya kila kitu, Nguvu Zake na Wingi Wake wa Kughufuria. 

 

2-Imebainishwa hikma ya kuumbwa mauti na uhai, kwamba ni kwa ajili ya kuwajaribu waja, watambulike wepi watakaotenda amali njema.

 

3-Ametakwa mwanaadam atazame uonekano wa Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Tawhiyd Yake ya Kuumba ulimwengu uliofikia upeo wa juu kabisa, Uumbaji usiokuwa na dosari yoyote ile.  

 

4-Imebainishwa mwisho mbaya wa makafiri na adhabu kali walizoandaliwa za moto uwakao vikali mno na vitisho vyake, na hali itakavyokuwa huko motoni watakapokuwa wanahojiana na Walinzi wa moto. Na kukiri kwa makafiri hao ukanushaji wao duniani walipowajia Rusuli kuwaonya, na kukiri kwao madhambi yao na kudhihirisha majuto yao Siku hiyo.   

 

5-Imebainishwa upana wa Ilimu ya Allaah (سبحانه وتعالى), kwamba hakifichiki Kwake kitu chochote, ni sawa iwe siri au dhahiri, na kwamba wanaotambua hayo wanamkhofu Rabb wao na watapata maghfirah na ujira mkubwa.

 

6-Imekumbushwa neema ya kuumbwa ardhi hii, na kuifanya ni yenye kuendana na maisha ya watu, na kuwaamrisha watu kuhangaika ndani yake, na kunufaika na vile vilivyomo ndani yake katika upande wa neema.

 

7-Imetahadharishwa mateso na Adhabu za Allaah na ukumbusho wa yaliyowapata makafiri wa nyumati zilizotangulia.

 

8-Wanaadam wametakiwa wazingatie na kutafakari tukio la ndege wanaokunjua mbawa zao angani, na katika hali za nafsi zao, na kwamba hakuna mwenye kunusuru isipokuwa Allaah, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Akiizuia Rizki Yake, basi hakuna mwengine wa kuwaruzuku.  

 

9-Imepigwa mfano kwa watu wa imaan na watu wa kufru, na watu wa haki na watu wa baatwil.

 

10-Imetajwa ada mojawapo ya makafiri kuwahimiza Rusuli wao wateremshiwe adhabu, na kwamba Siku ya adhabu itakapofika wakaiona, watadhikika mno makafiri.

 

11-Imewakemea washirikina juu ya kukufuru kwao neema za Allaah, na kudharau kwao makemeo Yake, na kumuamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) awakumbushe Neema za Allaah juu yao, na kuziradd shubha zao (kauli zao zenye utata) na uongo wao kwa hoja zitakazozibatilisha Shubha zao.

 

12-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemwongoza Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na Waumini kutawakali Kwake Yeye Allaah Pekee.   

 

13-Suwrah imekhitimishwa kwa kukumbushwa wanaadam Neema za Allaah na kwamba hakuna awezaye kuwapatia neema hizo pindi zikitoweka isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Inazuia Adhabu Za Kaburi:

 

عن ابنِ مَسعودٍ رَضِيَ اللهُ عنه، قال: قال رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم:  ((سورةُ تَبَارَكَ هي المانِعةُ مِن عذابِ القَبْرِ))

Amesimulia Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Suwrah ya Tabaarak inazuia adhabu za kaburi.” [Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3643), Swahiyh Ibn Hibbaan (3/68)]

 

2-Inamuombea Maghfirah Anayedumisha Kuisoma:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: " إِنَّ سُورَةً فِي الْقُرْآنِ ثَلَاثُونَ آيَةً شَفَعَتْ لِرَجُلٍ حَتَّى غُفِرَ لَهُ وَهِيَ: ((تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ)) رَوَاهُ أَحْمَدُ وَالتِّرْمِذِيُّ وَأَبُو دَاوُدَ وَالنَّسَائِيُّ وَابْنُ مَاجَه

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Suwrah katika Qur-aan yenye Aayah thelathini, zilimuombea mtu mpaka akaghufuriwa, nayo ni Suwrah:

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾

“Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo Ufalme.”

[Imaam Ahmad, At-Tirmidhiy amesema Hadiyth Hasan, na ameipokea pia Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (1474)]

 

 

 

 

 

 

 

Share