095-At-Tiyn: Utangulizi Wa Suwrah

 

095-At-Tiyn: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 8

 

Jina La Suwrah: At-Tiyn

 

Suwrah imeitwa At-Tiyn (Tini), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Fadhila na Faida, na kutajwa katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaneemesha wanaadam kwa kuwafanya wawe na tabia na maumbile yaliyonyooka, na kwa kukamilisha Risala ya mwisho. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha Unabii na Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji, Uendeshaji na kadhaalika) na marejeo ya viumbe Kwake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia matunda yenye faida tele kwa mwanaadam nayo ni tini na zaytuni. Na kuapia kwa mlima wa Twuur ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Alimsemesha Nabiy Muwsaa (عليه السلام). Na kuapia kwa mji mtukufu wa Makkah ambao ni mji aliozaliwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akajaaliwa kuwa Nabiy wa mwisho, na ukawa Makkah ni mji wa chimbuko la Uislamu. Kisha ikatajwa uhakikisho wa kiapo kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amemuumba binaadam umbo zuri kabisa lenye viungo vinavyoonekana na vilivyofichika, na kila kiungo kimeumbwa na kuwekwa sehemu ya mwili wa mwanaadam kwa hikma. Basi inampasa binaadam amshukuru Muumba Wake kwa neema hii. Lakini wengi wamemkufuru na hawakumwamini Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Hivyo basi, yeyote yule aliyekufuru Allaah (سبحانه وتعالى) Atamteremsha cheo afikie moto wa chini kabisa ambako ni mahali pa makafiri na wanafiki waliomuasi Rabb wao. Ama walioamini na wakatenda mema, wakajipamba na khulqa njema, hawa watapata ujira usiokatika, nao ni kuingizwa mahali wanapostahiki, napo ni Jannah, ambako kuna neema tele za  raha na starehe za kudumu milele.

 

2-Suwrah imekhitimishwa kwa swali la mshangao kwa makafiri wanaokanusha kufufuliwa kwamba kwani Allaah Hawezi Kuwafufua? Bali Naam! Anaweza kuwafufua kwa sahali kabisa. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Hakuumba wanaadam bila ya makusudio, au bila ya kuwekwa amri au makatazo. Au bila ya kuweko malipo mema na mabaya. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Ameiweka Siku hiyo tukufu ya Qiyaama Atoe uamuzi kati ya watu, Naye ni Muadilifu zaidi kuliko mahakimu wote wale.   

Fadhila Za Suwrah: 

 

عَنْ عَدِيِّ بْنِ ثَابِتٍ، قَالَ سَمِعْتُ الْبَرَاءَ بْنَ عَازِبٍ، قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَرَأَ فِي الْعِشَاءِ بِالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ ‏.‏ فَمَا سَمِعْتُ أَحَدًا أَحْسَنَ صَوْتًا مِنْهُ ‏.‏

 

Amesimulia ‘Adiyy Bin Thaabit (رضي الله عنه): Nimemsikia Al-Baraa (رضي الله عنه) akisema: Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma katika Swalaah ya ‘Ishaa:

وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ ﴿١﴾

“Naapa kwa tini na zaytuni.” [At-Tiyn (95)]

 

Na sijapatapo kumsikia mtu yeyote yule mwenye sauti nzuri kama yeye. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Faida:

 

Pindi mara moja, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa safarini, aliisoma Suwrah hii tukufu:

 

عَنْ عَدِيٍّ، قَالَ سَمِعْتُ الْبَرَاءَ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ فِي سَفَرٍ فَقَرَأَ فِي الْعِشَاءِ فِي إِحْدَى الرَّكْعَتَيْنِ بِالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ‏.‏

Amesimulia ‘Adiyy (رضي الله عنه): Nimemsikia Al-Baraa (رضي الله عنه)  akisema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa safarini akaisoma Suwrah:

 

وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ ﴿١﴾

“Naapa kwa tini na zaytuni.” [At-Tiyn (95)]

 

katika Rakaa mojawapo ya Swalaah ya ‘Ishaa. [Al-Bukhaariy na wengineo]

 

 

Share