26-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Wanawake Walioharamika Kwa Muda: viii-Mke Wa Tano Ikiwa Mtu Ana Wake Wanne Tayari

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

  

Alhidaaya.com 

 

 

 

26-Wanawake Walioharamika Kwa Muda:  viii-Mke Wa Tano Ikiwa Mtu Ana Wake Wanne Tayari:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ"

 

“Basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne”.  [An-Nisaa: 03]

 

Idadi ya mwisho aliyoruhusiwa Muislamu kuoa ni wanawake wanne tu, haruhusiwi kuongeza zaidi ya hapo.  Kuoa zaidi ya wanawake wanne kwa wakati mmoja, au kuoa bila mahari, kumeruhusiwa kwa sifa mahsusi kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tu.

 

Ikiwa mushrik atasilimu naye ana wake zaidi ya wanne, basi ataamuriwa awaache awatakao ili idadi ibakie wanne tu.  Ibn ‘Umar amesema:

 

"أَنَّ غَيْلَانَ بْنَ سَلَمَةَ أَسْلَمَ وَلَهُ عَشْرُ نِسْوَةٍ، فَأَسْلَمْنَ مَعَهُ، فَأَمَرَهُ اَلنَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ‏أَنْ يَتَخَيَّرَ مِنْهُنَّ أَرْبَعًا"

 

“Kwamba Ghiylaan bin Salamah Ath-Thaqafiy alisilimu akiwa na wake kumi aliowaoa enzi ya ujahiliya, na wake zake hao walisilimu pamoja naye.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru achague wanne tu kati yao ili abaki nao”.  [Maimamu wameitia kasoro pamoja na mwonekano wa kuwa ni sahihi.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1128), Ibn Maajah (1953), Ahmad (2/13) na wengineo]

 

Atakayeoa mke wa tano wakati anao wanne tayari, ndoa yake hiyo ya tano itakuwa ni batili.  Na kwa mujibu wa kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy, mtu huyo atastahiki adhabu ya kisharia ikiwa anajua uharamu wa kufanya hivyo.  Az-Zuhriy amesema:  “Atapigwa mawe kama atakuwa anajua hilo, na kama hajui, basi atapewa adhabu ndogo zaidi kati ya mbili ambayo ni kuchapwa mbati, na mwanamke huyo ni lazima alipwe mahari, watatenganishwa kati yao, na hawatakusanyika tena pamoja milele”.   

 

 

Share