43-Malaika: Kazi Za Malaika: (6)- Malaika Wa Tumbo La Uzazi

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

43:   Kazi Za Malaika

 

(6)- Malaika Wa Tumbo La Uzazi

 

Anas bin Maalik:  “Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ اللَّهَ ـ عَزَّ وَجَلَّ ـ وَكَّلَ بِالرَّحِمِ مَلَكًا يَقُولُ يَا رَبِّ نُطْفَةٌ، يَا رَبِّ عَلَقَةٌ، يَا رَبِّ مُضْغَةٌ‏.‏ فَإِذَا أَرَادَ أَنْ يَقْضِيَ خَلْقَهُ قَالَ أَذَكَرٌ أَمْ أُنْثَى شَقِيٌّ أَمْ سَعِيدٌ فَمَا الرِّزْقُ وَالأَجَلُ فَيُكْتَبُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ ‏"

 

“Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Amempa jukumu Malaika kushughulika na tumbo la uzazi.  Anasema:  Ee Mola wangu, ni tone la uzazi (niandike?). Ee Mola wangu, ni pande la damu (niandike?).  Ee Mola wangu, ni pande la nyama (niandike?).  Na Allaah Anapotaka kukamilisha umbo lake (kuwa binadamu kamili na kupuliziwa roho) Malaika huuliza:  Je, ni wa kiume (niandike) au wa kike?  Je, ni mwovu (niandike) au mwema?  Ni kiasi gani riziki yake (nyingi au kidogo niandike)?  Je, ataishi muda gani (umri mrefu niandike au mfupi)?  Na hapo huyaandika hayo kitoto kikiwa bado ndani ya tumbo la uzazi la mama”.  [Swahiyhul Bukhaariy (318)]

 

Rekodi ya mwanadamu kuhusiana na maisha yake yote imeanza kuandikwa akiwa bado ndani ya tumbo la mama na Malaika.  Akiwa tone la mbegu ya uzazi, halafu pande la damu, kisha pande la nyama, hayo yote yanasajiliwa na Malaika mwenye kazi hiyo. Likiingia tone la uzazi, anamuuliza Allaah: Hili tone la uzazi limeingia, je niandike?  Likibadilika na kuwa pande la damu anauliza hivyo hivyo na kuandika hadi pande la nyama.  Halafu yanaendelea mabadiliko, awamu kwa awamu, hadi anazaliwa mtoto kamili.  Huu ndio ukweli usiopingika.  Na kwa mujibu wa Hadiyth hii, inaonyesha Malaika wanaofanya kazi hii ni wengi sana, kwa kuwa idadi ya mimba za wanadamu zinazotunga kila wakati ni nyingi mno.  Nao huendelea kufuatilia hatua kwa hatua ukuaji wa mimba mpaka mtoto anapozaliwa.  Kisha huyu huyu mwanadamu, anakuja kuwa na kibri, anamwasi Mola wake bila kujali na anajisahau kule alikotoka!

 

 

Share