02-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Safari Ya Shaam

 

Aliposafiri kwenda Shaam (Syria) akifuatana na wafanya biashara wenzake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyakuta yale yale yaliyoko Makkah.

Watu na akili zao, mashujaa, wafasihi wa lugha, washairi wakubwa, walikuwa wakiyaporomokea masanamu na kuyasujudia. Na hali hii ndiyo ilivyokuwa Bara ya Arabuni kote.

Na huko Shaam pia walikuwepo wachache waliokuwa wakizungumza juu ya dini ya Nabii Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) na juu ya kumuabudu Mungu wa kweli asiye na mshirika.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anawaendea watu hao na kusikiliza maneno ya Imani kutoka kwao.

Walikuwepo wengine waliokuwa wakisoma Taurati na Injili mfano wa Waraqah bin Nawfal kule Makkah. Hawa walikuwa wakizungumza juu ya dini mpya ambayo muda wake umeshakaribia na juu ya Mtume mpya ambaye wakati wa kuja kwake umeshawadia, na kwamba Mtume huyo atatokea katika nchi ambayo Nabii Ibrahim aliijenga Al-Ka'abah.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anawaza;

Ni kweli Mtume atatokea katika nchi ile iliyojaa watu wanaoabudu masanamu, walevi, wacheza kamari na wauwaji wa watoto wachanga wa kike? Hivyo Kweli anaweza akatokea mtume mahali kama pale penye watu wenye tabia ovu kama zile? 

Alikuwa akijiuliza hivyo nafsini mwake kisha akijijibu mwenywe;

Na kwa nini asitokee Mtume wakati daktari haitwi mpaka pawepo na mgonjwa?

Isitoshe, watu wa Makkah juu ya kuwa na mabaya yote hayo, lakini walikuwa na sifa nyingi njema.

Walikuwa maarufu kuwa ni wasema kweli, na uwongo kwao ulikuwa ni aibu kubwa sana. Ukarimu ulikuwa ni moja ya sifa zao, walikuwa wakiwaambia watumwa wao;

"Atakayeweza kuniletea wageni wengi nitampa uhuru wake".

Watu wenye tabia kama hizi kwa nini asitokee Mtume miongoni mwao?"

Akawa anaikumbuka siku ile Qussa bin Saaida alipoingia ndani ya msikiti wa Al Kaaba bila ya kuwaogopa washrikina huku akisema;

"Labayka Mola wa kweli, Labayka Mola wa kweli, najikinga kwa yule aliyejikinga kwake Ibraahiym".

Yote haya yaliyokuwa yakimpitikia akilini mwake alipokuwa huko Shaam yaliujaza moyo wake shauku kubwa ya kumsubiri Mtume huyu mpya atakayeujaza ulimwengu Nuru ya dini ya Haki na kuwaondolea Makureshi na watu wote balaa hili la kuwasujudia masanamu.

Share