16-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mimi Si Mbora Wenu

Siku ya mwanzo ya utawala wake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)alipanda juu ya Mimbari ya Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwakhutubia Ummah aliopewa jukumu la kuwaongoza. Baada ya kupanda ngazi mbili alishindwa kuzikamilisha ngazi zote tatu alizokuwa akizipanda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), maana aliona kuwa akizikamilisha ngazi zote atakuwa amejiweka daraja moja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Baada ya kuzipanda ngazi hizo akaanza kuhutubia kwa kusema;

"Enyi watu!

'Mimi nimepewa uongozi juu yenu, lakini si mbora wenu.

Nikihukumu sawa, nisaidieni.

Nikihukumu vibaya nirekebisheni.

Hakika aliye dhaifu miongoni mwenu, kwangu mimi ni mwenye nguvu mpaka nimpatie haki yake, na hakika mwenye nguvu miongoni mwenu, kwangu mimi ni dhaifu mpaka niichukue haki ya watu iliyo kwake.

Nitiini iwapo nitamtii Allaah na Mtume Wake, ama nikiasi (amri ya Allaah) basi msinitii.

Umma unapoiacha Jihaad, hudhalilika.

Inukeni mswali, Allaah Akurehemuni".

Hii ndiyo khutbah ya mwanzo ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); khutbah fupi iliyoweka wazi jinsi gani atakavyohukumu.

Alisema;  

'Mimi nimepewa uongozi juu yenu, lakini si mbora wenu'.

 

Aliyasema haya ili kuujulisha Ummah kuwa yeye si Mfalme juu yao bali ni Kiongozi tu, na hivi ndivyo uhusiano utakavyokuwa baina yake na Ummah wake, Kiongozi, Mwalimu, Jemadari, Khaliyfah wao na Mwenzao.

Kwa njia hii aliwajulisha Ummah wake juu ya Dhamana aliyopewa na juu ya kiongozi mwaminifu, vipi anatakiwa awe.

Pia alitaka kuondoa katika fikra zao kwamba, anayehukumu, yupo juu ya shari'ah, na kwamba anaweza akafanya atakavyo, na kwamba hakosi na wala hakosolewi.

Alitaka kuwajulisha kuwa Uongozi si cheo cha kujivunia bali ni dhamana, na Ukhalifa alopewa ni kazi na si kitu cha kujitakabaria mbele ya watu.

"Lakini si mbora wenu"

Katika kitabu chake kiitwacho 'Khulafaa Rrasuul' Mwandishi maarufu Khalid Muhammad Khaalid (Allaah Amrehemu) alisema;

"Huenda akawa Kweli si mbora wao kwa vile yeye ni mwenye kuhukumu, lakini alikuwa mwenye hekima kupita wao na hii ni kwa sababu yeye ni Asw-Swiddiyq, Aliyesadiki ambaye ndani yake amekusanya Kusadiki, Imani, Uaminifu na Uongofu ulomfanya astahiki kuwa Swahibu yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa pangoni.

Alikuwa mwenye hikima kwa sababu alijua kuwa hatokuwa huru mpaka Ummah wake kwanza uwe huru.

Hatokuwa na nguvu mpaka Ummah wake kwanza upate nguvu.

Hatokuwa na Amani mpaka Ummah wake kwanza  upate amani"

 

Share