18-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Jeshi La Usaamah

Wakati haya yakitokea, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliona ni bora kulianzisha tena jeshi la Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu), jeshi lililoundwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mwenyewe chini ya uongozi wa Usaamah bin Zeid (Radhiya Allaahu ‘anhu), na jeshi hilo lilikuwa limekwishapiga kambi nje ya Madiynah likijitayarisha kwenda kupigana na Warumi, lakini kutokana na kushtadi kwa maradhi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo halikuondoka.

Baada ya kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo lilirudi tena Madiynah, na Waislamu wakahitilafiana juu ya kulianzisha tena jeshi hilo.

Baadhi ya Waislamu akiwemo 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliona kuwa si fikra nzuri kulianzisha tena jeshi hilo hasa wakati huu ambapo mji wa Madiynah umo katika hatari ya kuvamiwa na makundi ya waliortadi.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Lianzisheni tena jeshi la Usaamah, kwani Wallahi hata kama mbwa wa mwitu wataninyakua basi nitalianzisha tena kama alivyofanya Mtume wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)."

Alipoona kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameshikilia jambo hilo, 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Kwa vile Usaamah ni kijana mdogo sana, basi angalau ungemweka mtu mzima aliongoze jeshi hilo".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliruka kutoka pale aliposimama na kuzishika ndevu za 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamwambia;

"Ole wako ewe Ibnil Al-Khatwtwaab! Amepewa uongozi na Mtume wa Allaah na wewe unanitaka mimi nimuondoe?"

Ndani ya jeshi hilo walikuwemo masahaba wakubwa kama vile 'Umar, 'Uthmaan na wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum), na lilipokuwa likiondoka mjini Madiynah, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa analisindikiza huku akitembea kwa miguu na Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa amepanda farasi.

Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye umri wake haukuzidi miaka kumi na nane wakati ule akasema;

"Ewe Khaliyfah wa Waislamu, bora wewe panda juu ya mnyama huyu na mimi nitakwenda kwa miguu".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;

"Wa-Allaahi utabaki juu ya farasi na mimi nitatembea kwa miguu, kwani nitakuwa nimefanya jambo kubwa sana ikiwa nitaitia miguu yangu vumbi angalau kidogo katika njia ya Allaah?."

Kwa vile Abu Bakr alikuwa akiuhitajia ushauri na msaada wa 'Umar katika uendeshaji wa mambo ya Waislamu, na kwa vile 'Umar alikuwa miongoni mwa wanajeshi chini ya uongozi wa Usaamah, ilimbidi Abu Bakr amuombe Usaamah ili amruhusu 'Umar abaki naye Madiynah. Akamnong'oneza sikioni pake na kumwambia;

"Itakuwa vizuri kama utakubali kuniachia 'Umar, maana namhitajia katika kuendesha mambo ya Ummah".

Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akakubali.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) angeweza kumuamrisha Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) juu ya jambo hilo, lakini hakufanya hivyo kwa sababu Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mkuu wa jeshi hilo na mwenye haki ya kutoa ruhusa hiyo, na kama Usaamah angelikataa, basi asingemlazimisha.

Na jambo hili la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuliunda tena jeshi la Usaamah lilisaidia sana kuyavunja nguvu makundi ya waliortadi na kuingiza uoga nyoyoni mwao, maana waasi hao walipoliona jeshi hilo likitoka nje ya Madiynah kuelekea Sham, walisema:

"Wa-Allaahi ungekuwa mji wa Madiynah uko katika udhaifu na hitilafu kama tunavyosikia, basi wasingeweza kulitoa nje jeshi kubwa kama hili kupambana na Warumi".

Baada ya kuwasindikiza mpaka nje kidogo ya mji wa Madiynah, Abu Bakr akalikhutubia jeshi hilo na kulijulisha juu ya misingi ya jeshi la Kiislamu linavyotakiwa liwe.

Baada ya kumshukuru na kumpwekesha Allaah, akasema:

"Msifanye khiyana wala msishambulie bila taarifa (ghadran), wala msikate kate maiti za adui, wala msiue mtoto wala mzee wala mwanamke, wala msiunguze mtende wala msikate mti unaotoa mazao wala msichinje mbuzi wala n'gome wala ngamia isipokuwa kwa ajili ya kula.

Na mtakutana na watu waliojitenga ndani ya hekalu zao kwa ajili ya ibada, basi waacheni hivyo hivyo walivyo."

Kisha akasema: "Nendeni kwa jina la Allaah."

Haya ndiyo maamrisho ya Kiislamu, na hivi ndivyo alivyofundishwa Abu Bakr na Mwalimu wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na hivi ndivyo majeshi ya Kiislamu yalivyokuwa yakifanya kupitia karne zote.

Na waisome historia ya ufunguzi wa Kiislamu kama watakuta yale waliyofanya wao huko Algeria, Bosnia Kosovo, Afghanistan na hivi sasa Palestina. Waislamu wanachinjwa kama mbuzi na kukatwa katwa maiti zao na wengine wamezikwa wakiwa wazima, na wake zao wameingiliwa kwa nguvu na kuharibiwa, kisha wanajidai kuwa wao ni mabingwa wa kugombania haki za binadamu.

 

Share