13-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Hukumu Ya Wudhuu Huu (Wa Baada Ya Kitendo Cha Ndoa Kabla Ya Kulala)

Wudhuu huu sio fardhi lakini unasisitizwa sana na umependekezwa kufanyika. Kuwa si fardhi ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na 'Umar رضي الله عنه:

عن عُمرُ أنه سَأل رسول الله صلى الله عليه وسلم:  أَيَنامُ أحدُنا وهوَ جُنبٌ؟ قال: ((نَعَمْ، وَيَتَوَضَّأُ إِنْ شاءَ)) 

 

Imetoka kwa 'Umar رضي الله عنه ambaye alimuuliza Mtume "Je, tunaweza kulala katika hali ya janaba?" Mtume alijibu "Ndio na ufanye wudhuu ukipenda"[1]

 
Hii pia inaungwa mkono na Hadiyth nyengine iliyosimuliwa na mama wa waumini ‘Aaishah رضي الله عنها ambaye amesema,

كَانَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم يَنَامُ وَهُوَ جُنُبٌ مِنْ غَيْرِ أنْ يَمَسَّ مَاء ً[حَتَّى يَقُوم بَعْد ذَلِكَ فَيَغْتَسِلْ] 

"Mtume alikuwa akilala katika hali ya janaba bila ya kuwa amegusa maji" [mpaka anapoamka baadaye na kukoga].[2]

 
Katika riwaya nyingine, mama wa waumini ‘Aaishahرضي الله عنها amesema:

 

كَانَ يَبِيتُ جُنُباً فَيَأتِيهِ بِلاَلْ، فَيُؤذِّنُه بالصَّلاة، فَيَقُومُ فَيَغْتَسِلْ، فَأَنْظُرْ إِلَى تحدر الْمَاءَ مِنْ رَأسِهِ، ثُمَّ يَخْرُجْ فَأَسْمَعْ صَوْتُهُ فِي صَلاة الْفَجْر، ثُمَّ يظِلُّ صَائِماً. قَال مُطَرِّفْ: فَقُلْت لِعُامِر: فِي رَمَضَانْ؟ قَال: نَعَمْ، سَوَاء رَمَضَان أَوْ غَيْره

"Alikuwa akipitisha usiku wake katika hali ya janaba mpaka Bilaal alipokuwa anakuja asubuhi kuadhini. Kisha alikuwa akiinuka na kukoga na huku nikiona maji yanavyomtiririka kutoka kichwani mwake, kisha akitoka na husikia sauti yake katika Swalah ya Alfajiri. Kisha hubakia amefunga". Mutwarrif akasema: 'Nikamuuliza 'Aamir: Katika mwezi wa Ramadhaan?' Akajibu: "Ndio, katika Ramadhaan na pia katika miezi mingine".[3]

 

 

 

[1] Ibn Hibbaan: Swahiyh

[2] Ibn Abi Shaybah, At-Tirmidhiy, Abu Daawuud na wengineo: Swahiyh

[3] Ibn Abi Shaybah, Ahmad na wengineo: Swahiyh

Share