Zingatio: Kuwa Na Pupa .....Ya Kutenda Mema!

 

Zingatio: Kuwa Na Pupa….. Ya Kutenda Mema!

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ee ndugu yangu wa Kiislamu, unatambua ya kwamba unaye ndugu yako ambaye unaghafilika kumkumbuka na kumtayarishia ukarimu wako? Kumbuka kwamba ndugu yako mwengine yupo karibu na wewe. Tambuwa kuwa utakutana naye tu hata kama hujatoka naye tumbo moja bado atabaki ni sehemu ya damu yako na utakutana naye akiwa amefurahi au ameghadhibika.

 

Nduguyo Mawt daima utakutana naye.

Ukiamka asubuhi yupo anakuangalia weye.

Jana, leo, kesho zinapita bado yupo nawe.

Yundani maishani kwani ni amri ya Manani.

Uwendee wema kabla hajakukuta tayari kwa ajiliye.

 

Uwendee wema na jiepushe na maovu. Angalia litakalopendeza sikio lako watu kusema juu yako basi liendelee hilo kwa pupa. Angalia ambalo sikio lako litachukizwa kulisikia watu kusema juu yako basi jiepushe nalo haraka. Ukikaa na muuza kahawa utapata harufu ya kahawa. Ukikaa na wenye maneno mema maridhawa utapata utamu wao. Ukikaa na wenye kufitinisha na ukashiriki kumfitinisha nduguyo wa Kiislamu, hakika utakapoinuka kuondoka kwenye hicho kikao utaanza kufitinishwa wewe. Utakapokaa na wenye kusengenya, wakimaliza kusengenya wengine watakusengenya wewe nyuma ya mgongo wako. Kinachokwenda duara hurudi kwenye mzunguko wake.

 

Kila uamkapo asubuhi kuwa ni mwenye kushukuru hujakutana na nduguyo Mawt. Kwani huo ni mtihani na Muislamu hatakiwi kuomba kukutana na mtihani. Kila pumzi zinapodunda kutoka kwenye mapafu yako basi tambuwa kuwa utaulizwa kila sekunde uliyoitumia ama kwenye kheri ama kwenye shari.

 

Nakunasihi tena ewe ndugu wa Kiislamu.

Sio swala, zaka, funga umekamilika Uislamu.

Ni Iymaani yakini moyoni hadi khatamu.

Kwa kumuamini Rabb ili uipate Jannah tamu.

Hiyo ndiyo bendera kamili ya Mkweli Muislamu.

Jannah inapatikana kwa kuwa nayo hamu.

Fungasha anza leo kufanya pupa ya mema kwa kujilazimu.

 

Share