Anatamani Kuoa Lakini Hana Mali

 

SWALI:

Assalaam Alaykum Warhamatullaahi Wabarakaatuh,

Sheikh mie natamani kuoa sana, na sababu kubwa ya kutaka kuoa ni kujiepusha na zinaa. Lakini sina mali. Tayari kuna msichana muadilifu amekubali nimuoe lakini ninafahamu ni wajibu kwa mwanamume awe ndiye mlinzi wa mwanamke na ahakikishe kuwa mwanamke huyu anapata kila kitu anachokihitaji katika maisha yake mathalan, nguo, chakula na kadhalika. Tafadhalini ninasihini katika sula hili. Allah awajaze kheri nyingi.

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu aliyeuliza swali lake zuri. Hii inaonyesha jinsi gani vijana wanakuwa na hadhari pamoja na kutaka kufuata njia ya wema.

Hakika ndoa ni miongoni mwa ‘Ibaadah njema anayotakiwa kuifanya kijana mwanamme na mwanamke. Na wakati wa kuoa au kuolewa unapofika basi haifai kuchelewesha kwani haijulikani utaaga lini kabla ya kutekeleza hilo. Lakini pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewanasihi vijana ambao hawajakuwa na uwezo wa kuoa wafunge ili wasiingie katika zinaa kwani funga ni kinga (al-Bukhaariy na Muslim).

Ama kuhusu suala lako hilo tunasema yafuatayo:

Hiyo sababu yako ya kujiepusha na zinaa ni sababu kubwa na nzuri sana. Kwa ajili hiyo ya nia yako nzuri Allaah Aliyetukuka hatokutupa mkono bali Atakupatia kila aina ya usaidizi na kukusahilishia jambo lako hilo. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Mwenye kumcha Allaah Humtengenezea njia yake ya kutokea” (65: 2).

Na pia: “Na anayemcha Allaah, Allaah Humfanyia mambo yake kuwa mepesi” (65: 4).

Kuwa na mali ni njia moja muhimu ya kupata mke, lakini si njia pekee. Jambo ambalo halijaeleweka ni usemi wako kuwa yupo tayari dada muadilifu aliyekubali kuolewa nawe. Suali letu kwako ni je, ulimjua vipi kuwa yeye ni muadilifu? Je, umewahi kuzungumza naye kwa njia yoyote? Je, mnakutana ili kujitayarisha katika ndoa? Je, ushawahi kwenda kwao? Mbali na yote hayo ambayo lau yatakuwa yamefanyika basi utakuwa umeanza kwa njia ambayo ni haramu. Pindi ukianza na njia kama hiyo utakuwa mbali na rehema ya Allaah Aliyetukuka.

Hakika ni kuwa ni wajibu wa mume kumlisha, kumvisha na kumtazama mke na watoto katika hali zote za maisha ya ndoa. Lakini inatakiwa tufahamu kuwa hakuna ubaya kwa mke akiwa na uwezo kumsaidia mumewe katika baadhi ya majukumu ya nyumbani kwa sharti ya kuwa ule uongozi wa nyumba ubakie kwa mume. Mume kusaidiwa na mke si ajabu kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mwenye kusaidiwa sana na mkewe, Bi Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa kila hali hata alipopata Utume Da‘wah alikuwa akiiendesha kwa pesa za mkewe. Pia Swahaba mtukufu, ‘Abdullaah bin Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akisaidiwa na mkewe, Zaynab (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye alikuwa ni tajiri zaidi kuliko mumewe mpaka akausiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ampe Zakaah zake mumewe na atapata thawabu mara mbili (al-Bukhaariy na Muslim).

Ikiwa mke kwa ajili ya kutoa kwake atakuwa ndiye mume na anafanya atakalo, mume atakuwa ameingia katika udayuthi

Ikiwa utaliangalia suala hilo kwa kina basi swali Swalah ya Istikhaarah kumtaka ushauri Allaah Aliyetukuka. Ikiwa jibu la Swalah yako ni ndiyo basi itakuwa huna budi kwenda rasmi kwa wazazi wa mke ili kumposa na mpange tarehe ya jambo hilo jema. Na ushauri ulio mzuri zaidi badala ya yeye kukusaidia kila siku kwa masrufu awe ni mwenye kukupatia mtaji wa kuanzisha biashara au kazi yoyote unayoiweza ili uweze kuchukua jukumu lako la kinyumba.

Na kuanza ndoa kwa maisha duni au ya kimaskini, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Huongeza Baraka na kheri nyingi katika ndoa kama Anavyosema:

 

((وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ إِن يَكُونُوا فُقَرَاء يُغْنِهِمُ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ((

((Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Allaah ni Mwenye wasaa Mwenye kujua)) [An-Nuur: 32]

 

Tunakutakia kila la kheri katika suala hilo na tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie na Akuwafikishie. Tunakuombea na kukutakia kila la kheri na fanaka.

Na Allah Anajua zaidi

 Share