27-Imaam Ibn ‘Uthaymiyn: Masikini Wanapendekeza Kupewa Pesa Badala Ya Chakula Cha Zakaatul-Fitwr

 

Masikini Wanapendekeza Kupewa Pesa Badala Ya Chakula Cha Zakaatul-Fitwr

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

 SWALI:

 

Masikini wengi siku hizi wanasema kuwa wanapendekezea kupokea Zakaatul-Fitwr katika mfumo wa pesa badala ya chakula kwa sababu zina manufaa zaidi kwao. Je, inaruhusiwa kutoa pesa kwa ajili ya Zakaatul-Fitwr?

 

JIBU:

 

Tunavyodhani ni kwamba hairuhusiwi kutoka Zakaatul-Fitwr katika mfumo wa pesa kwa hali yoyote bali lazima itolewe kama ni chakula. Ikiwa mtu masikini anataka kuuza chakula na kutumia thamani yake anaweza kufanya hivyo. Lakini yule anayetoa inampasa atoe chakula. Hakuna neno ikiwa ni chakula kilichokuwa kilichojulikana zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa aalihi wa sallam) au ni aina ya chakula kinachotumika sasa. Mchele siku hizi huenda ukawa na manufuaa zaidi kuliko ngano, kwa sababu mchele hauhitaji mashaka ya kusagwa na kufanywa unga n.k. Kusudio ni kumnufaisha masikini. 

 

Imesimuliwa katika Swahiyh al-Bukhaariy kwamba Sa'iyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa aalihi wa sallam) tulikuwa tukitoa (kama Zakaatul-Fitwr) swaa’ ya chakula, na chakula chetu zama hizo kilikuwa ni tende, shayiri, zabibu na mtindi mkavu". 

 

Hivyo ikiwa mtu atatoa kwa mfumo wa chakula, basi achague chakula ambacho kina manufaa zaidi kwa masikini. Hii itabadilika kulingana na zama na mahali (nchi unayotolea Zakaatul-Fitwr).

 

Kuhusu kutoa Zakaatul-Fitwr kwa pesa, nguo, fanicha au vifaa, hii haitoshi na haitimizi ilivyowajibika kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetenda ‘amali isiyokuwa  yetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa))"

 

 

[Imaam Ibn ‘Uthayiyn Majmuw' Fataawa (18/191)]

 

 

Share