Mwanamke Mwenye Hedhi Afanye Nini Masiku Ya Mwisho Kupata Laylatul-Qadr?

 

 Mwanamke Mwenye Hedhi Afanye Nini Masiku Ya Mwisho Kupata Laylatul-Qadr?

 

 www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Nilikuwa nawaza mwanamke mwenye hedhi afanye nini usiku wa Laylatul-Qadr ili aweze kupata thawabu zaidi kwa kujishughulisha na ibada? Na kama inafaa, ibada ya aina gani inaruhusiwa afanye usiku huo?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Mwanamke mwenye hedhi anaweza kufanya vitendo vyote vya ibada isipokuwa kuswali, kufunga, kuzunguka Ka'bah na kukaa I'tikaaf Msiktini.

 

Imesimuliwa kwamba Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم  alikuwa akikesha usiku katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan.

 

(Al-Bukhaariy 2401) na (Muslim 1174) wamesimulia kwamba Mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنها amesema ((Zinapoingia siku kumi za mwisho katika Ramadhaan, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hujiepusha na wake zake, na hukesha usiku na kuwaamsha 'aila (familia) yake))

 

Kukesha usiku haina maana kwamba ni kwa kuswali pekee, bali ni kwa kila aina ya vitendo vya ibada, na hivi ndivyo walivyofasiri 'Ulamaa.

 

Al-Haafidh kasema: "Kukesha usiku ina maana kwamba kufanya aina za vitendo vya ibada"

 

An-Nawawy kasema:  "Kukesha usiku kwa kusimama kuswali na kadhalika",  akasema katika 'Awn al-Ma'abuud' kwamba ni kuswali, kufanya dhikr na kusoma Qur-aan.

 

Kuswali kwa kusimama ni kitendo bora kabisa Muislamu anaweza kufanya usiku wa Laylatul-Qadr kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :((Yeyote atakayesimama  kuswali  usiku wa Laylatul-Qadr kwa imani na kutaraji malipo atafutiwa madhambi yake ya nyuma)) Al-Bukhaariy 1901 na Muslim 760

 

Kwa sababu mwanamke mwenye hedhi haruhusiwi kuswali, ila anaweza kukesha usiku kwa kufanya aina ya vitendo vya 'Ibaadah zingine mbalimbali kama vile:

 

1) Kusoma Qur-aan

 

2) Kumdhukuru Allaah  kama kusema Subhaan-Allaah, La ilaaha illa Allaah, al-Hamdu Lillaah, anaweza kurudia kusema Subhaana-Allaah wal-Hamdu Lillaah, wa laa ilaaha illa Allaah, wa Allaahu Akbar na vile vile Subhaana Allaah wa bihamdihi, Subhaana Allaahul-‘Adhiym.

 

3) Istighfaar kwa kurudia kusema "Astaghfiru-Allaah"

 

4) Kuomba Du'aa.  Anaweza kumuomba Allaah anayohitaji ya duniani na Akhera kwani Du'aa ni kitendo bora kabisa cha 'Ibaadah. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Du'aa ni 'Ibaadah))  At-Tirmidhiy, 2895; na imesemwa kuwa ni  Swahiyh na Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy, 2370

 

Mwanamke mwenye hedhi anaweza kufanya vitendo vyote hivi usiku wa Laylatul-Qadr. 

 

 Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share