Wanawake Wanaweza Kufanya I'tikaaf?

 

Wanawake Wanaweza Kufanya I'tikaaf?

  www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Mimi ni Muislamu mpya na niko katika wasiwasi wa kufahamu  kuhusu I'itikaaf kwa wanawake. Je, wanawake wanaruhusiwa kufanya I'itikaaf kukiweko vyumba mbali mbali vya wanaume na wanawake msikitini?  Na kama wanawake wanaruhisiwa, siku ngapi wakae I'itikaaf? (siku tatu au wiki moja au siku kumi zote)?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

 

AlhamduliLLaah Ambaye Amekuongoza katika Uislamu. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akuongezee iymaan na taqwa. na  

 

Na'am anaruhusiwa mwanamke kufanya I'itikaaf Msikitini, hakika I'itikaaf ni Sunnah ya wote wanaume na wanawake.

 

Ni bora kufanya I'tikaaf siku zote kumi, kwa sababu hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Hadiyth ya kutoka kwa  'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akifanya I'tikaaf siku kumi za mwisho za Ramadhwaan mpaka kufa kwake.  Kisha wake zake wakaendeleza I'itikaaf baada ya kufa kwake)) [Al-Bukhariy 2026 na Muslim 1172]

 

Kama Muislamu hawezi kufanya I'itikaaf siku zote kumi, basi afanye zile siku anazoweza kama ni siku mbili au tatu au zaidi au chini ya hizo hata ikiwa ni siku moja tu.

 

Sheikh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema: 

 

I'itikaaf ina maana kukaa Msikitini kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   ikiwa ni kwa muda mrefu au muda mfupi, kwa sababu hakuna dalili nijuavyo inayoonyesha kwamba kuna muda maaluum kama ni siku au siku mbili au zaidi.

[Fataawaa Shaykh Ibn Baaz, 15/441].

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share