Zakaatul-Fitwr: Kiwango Gani Cha Kutoa Zakaatul-Fitwr? Nani Nipasaye Kumlipia?

 

Kiwango Gani Cha Kutoa Zakaatul-Fitwr? Nani Nipasaye Kumlipia?

 

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

swali langu ni kutoa zakaa  kwa mtu mmoja ni shilingi ngapi? je naweza nikawatolea nyumba nzima je lazima nitoe pesa? au kitu kingine?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu Swalaah na salamu zimshukie kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Unayepaswa kumtolea ni kila mtu katika familia yako ambao ni jukumu lako kuwahudumia kama mke, watoto, wazazi wawili, bibi na babu. Ama ikiwa hao wanacho kipato chao cha pesa, inabidi wajitoleee wenyewe.

 

Zakaatul-Fitwr haipasi kutolewa pesa bali ni kutoa chakula kinachotumika na watu katika mji ambao wanapewa masikini na wenye kuhitaji. Na kiwango chake ni swaa’ moja (swaa’ moja inasemwa ni kilo mbili na nusu, au viganja viwili vya mikono kwa pamoja viwe mara nne) kwa kiasi chetu tunachopima. 

 

 

Hii ni kutokana na dalili zifuatazo:

Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliifanya kutoa swaa’ ya tende au swaa’ ya shayiri (ngano) kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa Waislamu wote, mtumwa aliye huru, mwanamke na mwanamume, kijana na mzee, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd) [Al-Bukhaariy 1503]

Abu Sa'iydil-Khudriyyi (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukilipa Zakaatul-Fitwr swaa’ moja ya chakula, au swaa’ ya shayiri (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama hizo) au swaa’ ya tende au swaa’ ya aqit (mtindi mkavu) au swaa’ ya zabibu" [Al-Bukhaariy].

 

Kutolewa pesa haipasi ila tu ikiwa katika huo mji ulioko hakuna masikini au wanaohitaji kupokea Zakaatul-Fitwr, basi utatafuta watu waaminifu kama misikiti inayopokea Zakaatul-Fitwr ambao hukusanya pesa hizo za Zakaatul-Fitwr na kuzituma nchi ambazo zina masikini na zenye kuhitaji zaidi.

 

Na ikiwa hali ni hiyo basi kiwango chake kitakuwa ni sawa na thamani ya swaa’ moja ya chakula kinachotumika katika mji huo ulioko wewe.

 

Kwa maelezo zaidi soma katika kiungo kifuatacho Fataawa mbalimbali ambazo ALHIDAAYA imewatayarishia ile mpate majibu ya mas-ala yote mnayohitaji kuuliza na mzidishe elimu yenu.  Tafadhali  bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na faidi zaid:

 

Fataawaa: Za Zakaatul-Fitwr

Fataawaa: Mukhtasari Wa Fataawaa Za Zakaatul-Fitwr

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share