Anaweza Kumuoa Akiwa Anaishi Mbali Naye?

 

SWALI:

 

“ASSALAM ALAKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH”

Wana alhidaaya kheri, mafanikio mema, uvumilivu, ufahamu, uongozi mwema na yote mazuri akupeni M/Mungu mola wa ulimwengu wote. Na sala na salam ziwe juu ya kipenzi chetu mtume Muhammad (saw) na ahli zake na wote waja wema.

Sheikh:Kama nitakosea ni wajibu wenu kunirekebisha. Kuna hadith ya mtume

(saw) inasema  “enyi vijana mwenye kuweza harakati za ndoa miongoni mwenu basi na aoe” Na Allaah a’zza wa jalla anasema katika qur-ani tukufu “…..wao wanawake ni vazi kwenu nanyi ni vazi kwao”(2:187). Ni kwamba nina mchumba nategemea kufunga nae ndoa mara nikipata ufahamu kutoka kwenu. Kwa mujibu wa ndoa inatakiwa kua pamoja mke na mume, na mimi nimesafiri na huku niliko nafanya kazi. Kutokana na mkataba wangu, kila baada ya mwaka mmoja kuna likizo ya mwezi mmoja na umri wa kuzawij umefika. Kwa mujibu wa aya na hadith, pamoja na kuogopa kuja kumuasi M/Mungu. Na hali ya kiuchumi hairuhusu. Je niende nikaoe na na kumuacha mke wangu huko na tuwe tunakutana baada ya mwaka au tutapojaaliwa kukutana?

Nawaombeni mnionee huruma kwa kunipatia  majibu ya haraka ili kuninusuru ndugu yenu na ufafanuzi wenu M/Mungu aujaalie uwe ndo njia ya kutujengea familia bora kwa ndugu wote wa kiislam AMIN “ma’assalam”

                    Wabillahi tawfiq wa asalam alikum warahmatullahi wabarakatuh.

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kutokana na hali yako uliyoielezea na matakwa yako ya kufunga ndoa ukiwa unaishi mbali na mkeo, inafaa kufunga ndoa katika hali hiyo.

Ingawa sio jambo la kupendekezeka kwani kuishi mbali na mkeo ni jambo gumu linalotaka subira kubwa sana. Ikiwa nyote wawili mtaweza kuvumilia hali hiyo ya kutengana muda wa mwaka kama ulivyosema na kila mmoja ataweza kuchunga sitara na kujihifadhi basi hakuna makatazo ya jambo hili. Na pindi mkiweza kuvumilia basi mtakuwa miongoni mwa wa waliosifiwa na Allaah (Subahanahu wa Ta'ala) na ujira wake ni malipo ya Pepo.

  ((وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ))

 (( إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ))

  (( فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ))  

((Na ambao wanahifadhi tupu zao))

((Isipokuwa kwa wake zao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao hawalaumiwi)) 

 ((Lakini wanaotaka kinyume ya haya, basi hao ndio wanao ruka mipaka))   [Al-Ma'aarij 29-31]

Aqd inakamilika kwa kukamilika kwa masharti yafuatayo:

a) Idhini ya Walii.

b) Kuridhika kwa bibi harusi mtarajiwa.

c) Kutimia kwa tamko la ndoa yaani Ijaab na Qabuul (yaani Ijaab na Qubuul iliyounganishwa kwa tamko la ndoa au yenye kufidisha maana hiyo).

d) Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

e) Kubalighi na kuwa na utambuzi baina ya wanandoa, hivyo haifai kuwepo kwa ndoa ikiwa mmoja wapo ni mwendawazimu au mdogo kwa umri na bado hajabaleghe.

Kwa hiyo ikiwa utafunga ndoa nawe ukiwa mbali na huna nafasi au uwezo wa kwenda kufunga Nikaah, basi unaweza kumuwakilisha jamaa yako kukufungia hiyo ndoa baada ya kutoa muwafaka wako.

Kisha baada ya ndoa la muhimu ni umtimizie masurufu na mahitaji yake yote kama vile angelikuwa anaishi nawe.

Tunakuombea ndoa ya kheri yenye Baraka na tunakuombeeni nyote subira na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akufanyieni wepesi na Akukutanisheni muishi pamoja kwa Uwezo Wake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share