Mume Anataka kuvunja ndoa yetu Nifanyeje?

SWALI:

Asalamu aleikum nashukuru sana kupata hii site. nina swali moja lina nitatiza sana. Mimi nimeoelewa sasa ni mwaka na miezi hivi. Mume ameniambiya ameswali swalah ya isitihara ameonyesha ishara kama hakuna kheri katika ndoa. hivi sasa tu mbali mbali. Huwa ana nipigiya simu week mara moja lakini hanitizami kwa masurufu yoyote. Nasema yeye hati ndoa ivunjike sasa na naomba msaada kwenu ni fanye nini mimi. Naomba majibu kwa haraka.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa muulizaji swali. Hakika tumekuwa tukikariri mara nyingi kuwa uchaguzi kabla ya ndoa ni muhimu sana. Hukutuelezea mume wako alikuwa vipi katika mas-ala ya Dini. Je, yeye alikuwa ni mtu wa kuswali, kufunga na kufuata maagizo mengine au ni vipi? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana tuchaguane katika misingi ya kidini na pindi tukikosa kufanya hivyo basi tunakuwa katika matatizo ya daima.

 

Inaonyesha huyo kwa sababu anazozijua yeye alikuwa hakutaki tena akaona afadhali asingizie Swalah ya Istikhaarah. Kawaida Swalah hiyo inaswaliwa kabla ya kufanya jambo sio baada yake.

 

Bila kurefusha suala hilo, kitu ambacho unatakiwa kufanya sasa ni kuzungumza na mumeo kinagaubaga ili atoe uamuzi wake wa mwisho. Je, bado anakutaka au hakutaki tena? Ikiwa anakutaka basi akuweke kama mke na ikiwa hakutaki basi akuache kwa njia nzuri na hapo ukae eda ili baada ya eda ukipata kheri uweze kuolewa na mume mwingine.

 

Ikiwa yeye amesema ameswali Istikhaarah ambayo imemuelekeza kukuacha basi anafaa kufanya hivyo na sio kukutesa. Kwa sababu sasa hajakutamkia kuwa amekutaliki bado wewe ni mkewe na anafaa akutazame kwa kila kitu mpaka atakapoamua. Akiwa amekuacha basi anafaa kukutazama katika wakati wako wa eda mpaka imalizike kwa kila kitu.

 

Kwa hivyo, nasiha yetu ni kuwa usikae tu hivi hivi bali tetea haki yako kwa mwanzo kuzungumza naye na ikiwa njia hiyo imeshindikana basi ita wazazi wako na wake ili mtatue suala hilo.

 

Tunakutakia mafanikio na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akusahilishie na Akutolee njia mufaka ya kutatua tatizo hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share