Mume Amenitenga Miaka Mitatu Bila Ya Kunihudumia Je, Nimeachika?

 

SWALI:

 

As alykum namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa muongozo wa kufungua tofuto yenu. Swali langu: Hakuna mawasiliano na mume wangu huu mwaka wa tatu sasa kuna huduma yoyote kwangu na yuko hapahapa dar es salaam. Je ni bado mume wangu

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kukutenga kwa miaka mitatu.

 

 

Hakika tumekuwa tukikariri mara nyingi jinsi gani wanawake wanavyodhulumiwa na waume zao kwa njia moja na nyingine na hasa wakiwa katika ndoa.

 

Na dhulma hii inatokea kwa kuwa wanawake wenyewe pamoja na wazazi wenyewe wameshindwa kufuata mwongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika uchaguzi wa mume. Kwa minajili hii tunakuta kuwa matatizo yanatokea pindi tu mume na mke wanapooana. Hata hivyo, hilo ni jambo lishatokea tutakalofanya ni kukupatia nasaha kwa utakalofanya ili ujitoe katika dhulma hiyo. Awali ya yote ni kuwa bado wewe uko katika ndoa maadamu mumeo hajakupatia talaka.

 

Kwa hiyo, la kufanya ni kama ifutavyo:

 

  1. Jaribu kuzungumza na mumeo kwa njia nzuri umuulize msimamo wake kuhusu wewe. Je, anakutaka au anaona hawezi kuishi nawe tena? Ikiwa humpati inabidi utumie watu wako ili wakusaidie katika hilo.

 

  1. Ikiwa hakuna natija yoyote ile itabidi uitishe kikao baina yako, mumeo, wazazi wako (au wawakilishi wako) na wake ili mulizungumze suala hilo kwa kina na kupata ufumbuzi wa hilo.

 

 

 

  1. Ikiwa kwa hilo hakukupatikana lolote itabidi upeleke mashitaka yako kwa Qaadhi au Shaykh anayeaminika ili awasikilize nyote wawili na kutoa uamuzi. Kwa hali ilivyo ni kuwa Qaadhi itabidi aivunje ndoa ila tu mume aahidi kutekeleza majukumu yako.

 

 

Itabidi uchukue hatua ya haraka ili kupatikane ufumbuzi wa tatizo lako hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share