Talaka Ya Mume Aliyeniacha Wakati Wa Hasira

 

SWALI:

Assalam alaykum warahmatu llah wabarakatu. niliteta na mume wangu katika wakati wa hasira na kujibizana nikamwambia niache nae akanijibu basi nimekuacha. usiku ule ule tukapatanishwa na wazee na tukaregea kama kawaida kwa hivyo niliuliza kama yale matamshi ya talaka yamepita shekhe mmoja akasema kama ilikuwa wakati wa hasira basi haikupita lakini nina mushkil sije ikawa si hivyo, tafadhali nitumieni majibu kwa urefu ili nijue kuwa niko katika njia ya sawa.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa dada yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa suala la talaka halina mchezo kabisa. Kwa ajili hiyo ikawekewa mambo mengi kama hufai kumuacha mkeo akiwa katika ada ya mwezi, pia akiwa katika twahara ambayo tayari mume amemuingilia mpaka aingie katika hedhi kisha atwahirike na kadhalika.

Tatizo ni kuwa, kwa kutofuata kanuni hizi ndio tunakuwa katika matatizo ya kudumu katika ndoa na vurugu chungu nzima. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana tusiwe ni wenye kughadhibika. Na ikiwa tumekasirika basi tubadili mkao kwa jinsi kuwa ikiwa tumesimama tukae, ikiwa tumekaa tujilaze. Akatueleza tena hasira zinatokana na shetani ambaye ameumbwa na moto na moto huzimwa na maji. Hivyo akausia kuwa ikiwa mmoja wenu amekasirika basi achukue wudhuu. Wakati akikasirika pia anaweza kutoka nyumbani akaenda akazunguka mpaka zikatulia ndio akarudi na hapo kuweza kuzungumza na mke au mume kwa njia muafaka. Pia kumuomba Allaah Akuepushe na shetani kwa kusema, ‘A‘udhu biLlaahi minash-Shaytwaanir Rajiym

Ikiwa hayo hayakufanywa ndio kunapatikana natija hii mbaya ya kutoa talaka ambayo ilikuwa haipasi kabisa. Kuna rai mbalimbali kuhusu suala hili, lakini yenye nguvu ni kuwa ikiwa mume alikuwa na hasira ambayo ilimfanya asijitambue akili yake na akawa anasema asichokijua, basi haijatuka talaka hapo, ama akiwa na hasira na akawa anajua anachosema akiwa na akili zake timamu hapo talaka itakuwa imepita. La kufanya ni kumuuliza vizuri mumeo kama wakati huo alikuwa akili yake iko timamu au alikuwa hakujitambua anachosema? 

Ikiwa amejitambua na imehasibika kuwa ni talaka ya kwanza au ya pili, mume anaweza kumrudia mkewe katika kipindi cha eda bila kufungwa ndoa mpya. Ikiwa hiyo ilikuwa ni talaka ya tatu, mume hawezi kufanya hivyo mpaka mke aolewe na mume mwingine kisha aachwe.

Pia ikiwa ameachwa mke akakaa eda mpaka ikamalizika, wawili hao wakitaka kurudiana, kutatakikana kufungwe ndoa upya na mume atoe mahari watakayoafikiana.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awapatie tawfiki muweze kuvumiliana na jambo kama hilo lisitokee tena. Wasiya wetu kwako ni kuwa ukiwa umekasirika jaribu kuzima hasira zako na lisikutoke neno la ‘basi niache’.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share