Mume Amekasirika Hamgusi Mkewe Miezi 3 Kisha Alikuwa Na Niyah Ya Kumwacha, Je, Ni Talaka Hiyo?

SWALI:

Asalam aleikum warahma tuAllaahi wabarakatu,

Nawashukuru sana kuweka web hini mtu kuweza kuliza maswali rabana awatiliye kila la kheri na barka, mimi nina watoto wawili nina miyaka 23 mumewangu atatabiya ya kukasirika haraka na jambo dogo kuwa kubwa, akikasirika anatabiya kuwa hanigusi kwa miyezi mitatu kisha yuwaniambiya ilikuwa ataka kuniwata (talaka) jee yamanisha ameniwacha? manake ashafanya mara nyingi na tuko pamoja 5 yrs (niya ilikuwa anayo), nawaomba munijibu kwa haraka na kwenye email yangu. shukran jazaka Allaahu kheir.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hasira ya mume na kutokugusa kwa muda wa miezi mitatu.

Niyah ya kukuacha haiwi ni talaka kabisa. Talaka kishari’ah ni lazima itamkwe au iandikwe. Kuwa ana Niyah ya kukuacha huwa bado kwani hilo ni tendo la baadaye, yaani mustakbali.

Hata hivyo, si tendo zuri kwa mume kumfanyia hivyo mkewe. Wanandoa wanatakiwa wawe ni wenye kusikilizana, kuheshimiana na kutakiana mema. Hivyo, ikiwa mke amefanya makosa inabidi mume amkalishe chini na kuzungumza kiutu uzima na kwa njia bora. Na mume akifanya makosa mke anatakiwa afanye hivyo hivyo kwa kumuweka chini na kuelezana kuhusiana na hilo. Kuwa na hasira ni tabia ambayo inaweza kuvuruga familia na ndoa. Mume anatakiwa apatiwe ushauri nasaha kwa tabia hiyo aliyo nayo.

Kwa kufanya hivyo mwanzo kabisa anza kuzungumza naye kwa njia nzuri hisia zako na tatizo linalokukabili kuhusiana na hilo. Ikiwa hakuna natija basi inabidi kuitishwe kikao baina yako, mumeo, wawakilishi wako na wale wa mumeo ili mtatue tatizo hilo ili lisiharibu ndoa yenu. Ikiwa hamkufanikiwa itabidi basi mpate ushauri kutoka kwa Shaykh au Qaadhi wa hapo mlipo.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie tatizo hilo ulilo nalo.

 Bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

Talaka Ziko Aina Ngapi Na Wakati Gani Zinasihi?

Mas-ala Ya Talaka Mbali Mbali

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share