Mume Ana Mke Kisha Akafanya Urafiki Na Mwanamke Mwengine Na Akamuoa Kisiri

 

SWALI:

Mwanamke mmoja alimuona mume wangu kwenye mkutano na akampenda akawa anamwandikia mabaru pepe na anampigia simu za kumtongoza. Wakajenga urafiki wa mapenzi ingawa hawakuzini kwani walikuwa wanaishi mbali mbali.

Lakini wakawa wanaanidkiana barua za mapenzi kwa miezi sita ikisha mume wangu akamuoa huku akiwa ananificha mimi mkewe. hii inakubaliwa kisheria? 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Mahusiano baina ya mwanamke na mwanaume kabla ya ndoa hayafai kutendeka ikiwa kwa kuwasiliana kwa barua, au kuonana kwani hayo sio mafunzo tuliyopata katika dini yetu. Na kufanya hivyo ni kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Lakini mja anapotenda maasi kisha akatubia, Mola Humsamehe madhambi yake. Na katika hali hiyo ya mume wako ingawa ametenda maasi hayo, lakini madamu amefikia kumuoa huyo mwanamke, atakuwa amefanya jambo la kheri kuliko kuendelea kuwasiliana naye bila ya kuwa na nia ya kumuoa kwani hivyo ingelikuwa ni kumdanganya na kumharibia stara yake.

Fikiria dada yetu kama hali hiyo ingelikuwa imekufika wewe, mwanamue awasiliane nawe akidai anakupenda kisha ima akuachilie mbali na pengine baada ya kukuchezea akuharibie stara yako.

Wanaume wamepewa ruhusa ya kuoa zaidi ya mke mmoja madamu tu wataweza kutekeleza uadilifu baina yao. Na kufanya hayo kwa kukuficha wewe bila shaka ni ishara kuwa anakupenda bado mkewe na amekuheshimu ndio maana hakuweza kukujulisha mapema. Na ingelikwua hakupendi basi angeliamua kukupa talaka lakini hakufanya hivyo kwa kutaka bado awe na wewe.

Na madamu ametimiza masharti ya ndoa yafuatayo basi ndoa yake itakuwa imeswihi kisheria:

Aqd inakamilika kwa kukamilika kwa masharti yafuatayo:

a) Idhini ya Walii.

b) Kuridhika kwa bibi harusi mtarajiwa.

c) Kutimia kwa tamko la ndoa yaani Ijaab na Qabuul (yaani Ijaab na Qubuul iliyounganishwa kwa tamko la ndoa au yenye kufidisha maana hiyo).

d) Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

e) Kubalighi na kuwa na utambuzi baina ya wanandoa, hivyo haifai kuwepo kwa ndoa ikiwa mmoja wapo ni mwendawazimu au mdogo kwa umri na bado hajabaleghe.

Linalokupasa dada yetu ni kukubali majaaliwa hayo ambayo yameshatokea, na ingawa ni jambo gumu la uke wenza lakini utakapovuta subra malipo yake ni makubwa mno kwa Mola wako. Vile vile utakapoonyesha kuridhika na jambo hilo kwa mumeo ndipo atakapozidi kukupenda na kukuthamini.

Soma mada katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi ya hikma ya wanaume kuoa wake zaidi ya mmoja ili upate kuridhika na amri ya Mola wako.

 

Hikma Ya Ruhusa Ya Ukewenza

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share