Walioacha Kuswali Wakidhi? Je, Hawafai Kuswali Sunnah?

   

SWALI:

 

Asalam alaekum warahamatullah wabarakatu. Mimi nauliza hivi:  baadhi ya watu kuna baadhi ya swala ambazo hawakuziswali yaani walikuwa wanaswali na kuacha na hawana uhakika ni swalah gani na gani na ngapi. suala langu ni hivi (1) eti hawawezi kusali swalah za sunah?

(2) Sasa wafanye nini kukamilisha swala zao ili waweze kuswali swala za sunnah? Naomba ufanunuzi wenu. Wabillahi tawfiq. Mwenyezi Mungu awajaalie kila kheri hapa duniani na kesho akhera Amin.

 


 

 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwako ndugu yetu kwa swali lako kuhusu mas-ala ya kulipiza Swalah ulizoziacha. Wanazuoni wana rai mbili zenye kutofautiana:

 

Awali, ni kuwa kwa mtu ambaye hakuswali kwa sababu moja au nyengine anapoamua kuswali na hasa ikiwa kumepita muda mwingi ataleta toba kwa masharti yake yote. Hiyo ni kuwa atajuta, atajiondoa katika maasiya hayo na kuazimia kutorudia tena dhambi hilo la kutoswali. Pindi anapotubia na kujirekebisha basi huwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amemsamehe kwani hakuna haki ya binaadamu iliyoingia kati. Hayo ndio masharti yaliowekwa na kama Imaam an-Nawaawiy ambaye amesema katika Riyaadh asw-Swaalihiin, Mlango wa 2 kuwa wanazuoni wamesema hivyo.

 

Rai ya pili, ni ile inayosema kuwa ukiwa na deni la mwanaadamu mwenzio unatakiwa ulilipe ukiwa umesahau kufanya hivyo hata baada ya kupita muda wake. Deni la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) lina haki zaidi ya kulipwa. Hivyo, ukiwa umeghafilika kuswali Swalah yoyote ile, unatakiwa uiswali pindi unapokumbuka hata kama wakati wake umepita. Kwa mfano, umeona kuwa umeswali Swalah ya Alfajiri kwa kusahau ukakaa mpaka inafika saa sita mchana unakumbuka kuwa kumbe ulikuwa hujaswali inatakiwa hapo hapo uswali Swalah hiyo uliyosahau. Na ikiwa umepita muda basi utakisia muda wenyewe na kuweza kukidhi Swalah zenyewe. Hiyo itakuwa baada ya kuswali kwa mfano Swalah ya Adhuhuri utachukua muda kwa kuswali Adhuhuri kadha za siku zilizopita na hivyo hivyo Swalah nyingine kama Alasiri na kadhalika. Jambo litafanyika mpaka muda uliokisia kuwa umeacha Swalah utakapofika.

 

Wanazuoni wengine wanachukulia rai ya kwanza ndio yenye nguvu na wengine rai ya pili. Kwa kila hali kuwa katika tahadhari zaidi ni bora kuchukua rai ya pili kwani hilo litaonyesha kuwa uko kweli na hima ya kutaka kujirekebisha na kutaka msamaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).  

 

Ikiwa itachukuliwa hii rai ya pili basi itabidi uache Sunnah kwa ule wingi wa Swalah ambazo unafaa ukidhi lakini ikiwa itachukuliwa rai ya kwanza utahitajika uswali Sunnah zaidi ili zikuongezee thawabu.

 

 Na Allaah Anajua zaidi

Share