Kukidhi Swalaah: Wakati Gani Wa Kukidhi Swalaah Uliyoisahau?


SWALI:

A. alaykum Warahmatullahi Wabarakatu.

Swali langu hili? Ikiwa umesahau kuswali kipindi kimoja cha swala, mathalan alfajiri ama adhuhur, na ukikumbuka pengine ni usiku wakati wa kulala, je utafanyaje? Ama hukmu yake ni nini?




JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako hilo muhimu sana. Hiyo ni kuwa Swalah ni nguzo muhimu sana na ya kwanza kukaguliwa Siku ya Qiyaamah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameusahaulishia Ummah huu wa mwisho kwa kutowafanyia mambo kuwa magumu kwao na hata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametumwa kuondoa mizigo mizito na minyonyoro iliyokuwa hapo mbeleni na shingoni mwa wanaadamu, kama Asemavyo Allaah:

 

“Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomuamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye hao ndio wenye kufanikiwa.” (7: 157).

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatutakii magumu kama Alivyosema: “Hakuweka uzito wowote katika Dini mila ya baba yenu Ibraahim” (22: 78).

 

Kwa minajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatueleza kuwa yapo mambo yanapofanywa na Muislamu katika nyakati hizo huwa haandikiwi. Baadhi yake ni:

 

 

    • Kutenzwa nguvu kufanya la makosa.
    • Kabla ya mtoto kubaleghe.
    • Mwenda wazimu.
    • Aliyelala hadi aamke.
    • Aliyesahau mpaka akumbuke.

    •  

Hivyo, ukiwa umesahau kikweli kutekeleza Ibaadah Fulani kwa mfano Swalah ya Alfajiri, au nyingine yoyote utakuwa huna dhambi. Lakini pindi unapokumbuka unatakiwa uiswali hiyo Swalah hata kama ni usiku na wakati wake umepita. Naye hatakuwa na dhambi kwani ana udhuru wa kisheria kwa kusahau kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka: “Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu” (2: 286).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kulala bila kuswali kwa kusahau aswali pindi anapokumbika na hapana kafara kwa hilo”.

 

Kwa muhtasari anatakiwa aliyesahau aswali pale anapokumbuka bila kuchelewa.

Na Allah Anajua zaidi

Share