Kuufanya Usiku Wa Ijumaa Kuwa Ni Maalum Kwa Ibada Ya Qiyaamul-Layl

 

Kuufanya Usiku Wa Ijumaa Kuwa Ni Maalum Kwa Ibada Ya Qiyaamul-Layl

 www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Naomba kueleweweshwa kuhusiana na kusimama usiku wa kuamkia ijumaa kwa ajili ya kiamulaili inaruhusiwa? kuna hadith ambayo niliwahi kuisikia ambayo inakataza kufanya hivyo ambayo ipo ktk kitabu cha bulugh l-maramy.

Naomba nifahamishwe in Shaa Allaah

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Haifai kuupwekesha usiku wa Ijumaa kwa ‘ibaadah ya aina yoyote. Hii kutokana na dalili ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( لا تَخْتَصُّوا لَيْلَةَ الْجُمُعَةِ بِقِيَامٍ مِنْ بَيْنِ اللَّيَالِي وَلَا تَخُصُّوا يَوْمَ الْجُمُعَةِ بِصِيَامٍ مِنْ بَيْنِ الْأَيَّامِ إِلا أَنْ يَكُونَ فِي صَوْمٍ يَصُومُهُ أَحَدُكُمْ ))  مسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiufanye usiku wa Ijumaa kuwa ni mahsusi kwa Qiyaam (Kisimamo cha kuswali usiku) baina ya masiku mengine na wala msiifanye siku ya Ijumaa ni makhsusi kwa kufunga baina ya siku nyingine isipokuwa ikiwa ni miongoni mwa siku anazofunga mmoja wenu)) [Muslim]

 

Masiku yote yako sawa isipokuwa siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhwaan ambamo humo kuna usiku wa Laylatul-Qadr ambao ‘ibaadah yake ni bora kuliko ibada ya miezi elfu.

 

Muislamu anaweza kuamka usiku wowote kufanya ‘ibaadah na kuomba atakacho bila ya kupwekesha siku maalumu kwani kila siku katika thuluthi ya mwisho ya usiku Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huteremka kwa namna inayolingana na Utukufu Wake, katika mbingu ya kwanza na kuwakidhia waja haja zao kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

   عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Kwa hiyo Muislamu asiache fursa hii ya kuomba kila siku anachokitaka na khaswa kwa vile wana Aadam tuna mengi tunayoyahitajia kila siku katika maisha yetu ya dunia na Aakhirah. Hivyo asisubiri mtu siku maalumu ambayo haina dalili ya fadhila zake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share