Muda Wa Swalaah ya Istikhaarah

 

Muda Wa Swalaah ya Istikhaarah

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Asalaamu A'aleikum
Nataka kuuliza swali kuhusu swala ya istikara ! Kama naswali swala hii for how long should i pray mpaka nipate jawabu cos najuwa silazima kuoteshwa lakini what i dont understand is for how long niendele.
 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

AlhamduliLlaah tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa Kutujaalia kheri nyingi katika Dini yetu. Mojawapo ni kheri kama hii ya kuweza kufanya Istikhaarah katika mambo yetu na kumwachia Yeye Allaah  (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  Atuongoze katika lilokuwa la kheri kulitenda kwani Yeye Ndiye Mwenye kujua mambo ya 'ghayb' (yaliyofichikana), na hajuti mwenye kutaka mwongozo wa Allaah ('Azza wa Jalla).  

 

Swalaah ya Istikhaarah hakika pia ni zawadi kubwa tuliyopewa sisi Waislamu, kwa hivyo inatupasa tuitumie kwa kila jambo linalotutia shaka kuamua kama walivyokuwa wakifanya Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum Jamiy’an) kutokana na mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ جَابِرٍ رضي الله عنه قَالَ : كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُعَلِّمُنَا الاسْتِخَارَةَ  فِي الأُمُورِ كُلِّهَا كَمَا يُعَلِّمُنَا السُّورَةَ مِنْ الْقُرْآنِ يَقُولُ : إذَا هَمَّ أَحَدُكُمْ بِالأَمْرِ فَلْيَرْكَعْ رَكْعَتَيْنِ مِنْ غَيْرِ الْفَرِيضَةِ ثُمَّ لِيَقُلْ

Jaabir Bin ’Abdillaah  (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah  (صلى الله عليه وسلم) alikuwa akitufundisha Swalaah ya Istikhaarah kama vile anavyotufunza Suwrah ya Qur-aan, akisema: ((Akikusudia mmoja wenu kufanya jambo, aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme:

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْتَخيـرُكَ بِعِلْمِك، وَأسْتَقْـدِرُكَ بِقُـدْرَتِـك، وَأَسْـألُـكَ مِنْ فَضْـلِكَ العَظـيم، فَإِنَّـكَ تَقْـدِرُ وَلا أَقْـدِر، وَتَـعْلَـمُ وَلا أَعْلَـم، وَأَنْـتَ عَلاّمُ الغُـيوب، اللّهُـمَّ إِنْ كُنْـتَ تَعْـلَمُ أَنَّ هـذا الأمْـرَ  (وَيُسَـمِّي  حاجته)  خَـيْرٌ لي في دينـي وَمَعـاشي وَعاقِـبَةِ أَمْـري،  عَاجِلِهِ و آجِلِه , فَاقْـدُرْهُ لي وَيَسِّـرْهُ لي ثـمَّ بارِكْ لي فيـه، وَإِنْ كُنْـتَ تَعْـلَمُ أَنَّ هـذا الأمْـرَ شَـرٌ  لي في دينـي وَمَعـاشي وَعاقِـبَةِ أَمْـري،  عَاجِلِهِ و آجِلِه  فَاصْرِفْـهُ عَنّيِ  وَاصْرِفْني عَنْـهُ وَاقْـدُرْ ليَ الخَـيْرَ  حَيْـثُ كانَ ثُـمَّ أَرْضِـني بِـه.

Ee Allaah hakika mimi nakutaka (muongozo) unichagulie kwa ujuzi Wako, na nakuomba Uniwezeshe kwa uwezo Wako, na nakuomba fadhila Zako kubwa, hakika Wewe Unaweza, nami siwezi, Nawe unajua nami sijui, Nawe ni Mjuzi wa ya ghayb. Ee Allaah, iwapo jambo hili kutokana na ujuzi Wako (utalitaja jambo lako) lina kheri na mimi katika Dini yangu na maisha yangu na mwisho wa jambo langu, karibu na mbali, basi nakuomba Uniwezeshe nilipate, na Unifanyie wepesi, kisha Unibariki. Na iwapo Unajua kwamba jambo hili ni shari kwangu katika Dini yangu na maisha yangu na mwisho wa jambo langu (katika Dunia yangu na Aakhirah yangu) basi liepushe na mimi nami niepushe nalo, na nipangie jambo jengine lenye kheri nami popote lilipo, kisha niridhishe kwalo. [Al-Bukhaariy]

 

 

Swalaah ya Istikhaarah ni raka'ah mbili na  haina Suwrah maalumu na  huswaliwa siku yoyote, wakati wowote na mara zozote unapopenda kufanya jambo hadi hilo jambo ujaaliwe kulifanya au usijaaliwe itakuwa yote ni kheri kwani madamu tu umeshaswali Istikhaarah basi umeshamuelekea Rabb wako kutaka Yeye Akuongoze. Kwa hiyo hata ukiswali mara moja tu inatosha kabisa kuwa umeshatimiza Istikhaarah. 

 

Ni makosa kudhania kuwa mtu anaposwali Swalaah ya Istikhaarah kuwa lazima baada ya kuswali asizungumze na mtu bali aende kulala moja kwa moja na kutegemea kuota, au hata kutegemea tu kuoteshwa ndoto kuhusu hilo jambo. Hivyo sio sawa kwani hakuna uthibitisho wa hayo katika Shariy’ah.

Jambo muhimu jingine linalopasa tulijue kuhusu Swalaah hii ya Istikhaarah ni kwamba haifai kuitumia kwa mambo yasiyomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), mfano asiswali mtu Istikhaarah kwa kutaka kuchukua haki ya mtu au kugombana na mtu au kwenda kwenye maasi na kadhalika, bali ni kuitumia katika mambo ya yafaayo ki-Shariy’ah  mfano anapotaka kuposa au kupokea posa, kufanya kazi au  kibarua katika shirika fulani, au kusafiri na kadhalika.    

 

Vile vile ni jambo zuri kuchukua ushauri wa watu wema unapokuwa na jambo la shaka kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Ametuamrisha kufanya hivo kama Alivyomshauri Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  

 

وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوكِّلِينَ ﴿١٥٩﴾

na washauri katika mambo. Na unapoazimia basi tawakali kwa Allaah. Hakika Allaah Anapenda wanaotawakali [Aal-‘Imraan: 159]

  

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share