Talaka Kaituma Kupitia Mtu Na Mtu Huyo Hakuifikisha

SWALI:

SUALA LANGU LAHUSU; TALAKA

MIMI NINA NDUGU AMBAE ANAISHI DAR ES SALAAM NA MUME WAKE, HUYU BWANA KAKUMBWA NA MITIHANI KAACHISHWA KAZI. SASA HUYU BWANA KAKUSUDIA KUMUACHA HUYU NDUGU YANGU,LAKINI HII TALAKA KAIPITISHIA KWANGU KABLA SIJAIFIKISHA KWA MUHUSIKA KABADILIKA NA KASEMA NIICHANE NA NISIMWAMBIE LOLOTE KUHUSU HILI. JE, HII TALAKA ITAKUWA IMESIHI AU HAIKUSIHI KWA SABABU MWENYEWE HAJUI CHOCHOTE KUHUSU HILI

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani ndugu yetu katika Imani kwa suala lako kuhusu mas-ala muhimu katika Dini yetu tukufu ya Uislamu.

 

Jambo hili la talaka na mas-ala mengine ya kijamii ni mambo ambayo tumekuwa tukiyasisitizia kila wakati na kila mara. Hakika ni kuwa hili ni tatizo la kijamii sugu ambalo limesumbua jamii yetu pamoja na ujahili ambao umelizidisha na kulikuza.

 

Ni nasaha kutoka kwetu kuwa tusiwe ni wenye kuchezea talaka. Talaka kuwekwa mikononi mwa mwanaume ni kuwa awe mwangalifu na mwenye busara katika kuitumia wala asiwe ni mwenye kuitoa ovyo. Kukosa kazi si sababu ya mtu kutoa talaka. Inatakiwa mume na mke waishi kwa kuvumiliana kwa kiasi kikubwa sana. Ikiwa walikuwa na wasaa mzuri wamshukuru Allaah Aliyetukuka na wasaa kama huo ukiingia dosari basi pia wamshukuru Allaah Na hayo yote ni kheri kwao.

 

Talaka ni halali moja ambayo haina mzaha kabisa kwa maana ya kuwa unapoitamka inakuwa ni yenye kupita. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):  

Kila talaka inajuzu isipokuwa talaka ya mwenye kulazimishwa kwa akili yake” (at-Tirmidhiy).

 

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

Mambo matatu ukweli ni ukweli na mzaha wake ni ukweli: Nikaah, talaka na kumrudia mkeo (baada ya kumtaliki)” (Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

Kati ya mambo ambayo yanafanya talaka kupita ni kutoa kauli ya wazi isiyo na utata ya kumtaliki, kumwandikia, kutumia ishara kwa asiyesikia au kutuma mjumbe kutoa salamu. Kwa kuwa mume katuma mjumbe kuwa amemtaliki fulani basi talaka hiyo imepita na jukumu lako ni kufikisha ujumbe huo bila kungojea muda zaidi upite. Kutopeleka ujumbe ni makosa juu yako na hili ni funzo kwake na kwa wengineo wasiwe ni wenye kufanya masikhara na jambo hili zito.

 

Kwa kuwa ametambua kuwa alilofanya ni makosa anaweza kumrudia mkewe ikiwa hiyo ni talaka ya kwanza au ya pili. Ikiwa ametoa hiyo ni talaka ya kwanza anaweza kumrudia kabla ya eda kumalizika bila ya mahari wala ndoa mpya. Iwapo eda itamalizika basi itabidi atume posa mpya, na mahari watakayokubaliana baina yao na kuridhika kwa mke mwenyewe kuolewa tena na mume huyo wa awali. Kwa hiyo, ndugu yetu usichelewe kwa wajibu uliopatiwa na tunamuombea ndugu yetu asiwe ni mwepesi mara nyengine kutoa talaka bila kuangalia kila upande wa suala hilo nyeti.

 

Tunamuombea ndugu yetu Allaah Aliyetukuka Ampatie kazi ya halali iliyo bora kuliko ya awali na Ampatie usahali katika maisha yake ya ndoa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share