Mume Anayo Haki Kukataa Kuishi Na Shemeji

 

SWALI:

Naishi na ndugu yangu nanimaharimu yangu. Nimeolewa na naishi na mume wangu na watoto.Swali langu ni hili: Mume wangu hamtaki kakangu tuishi nae na  kakangu ana shida kama mujuavyo nchi za ulaya mpaka upate sharia ya kuishi yaani makaratasi na bado hajafanikiwa sioni kama ana makosa yuaswali, yuani sikiza kwa kila jambo ana adabu na heshima kwa jumla. Mume wangu ametoka nyumba kwa ajili yake myezi sita sasa bila kuuliza watoto wala mimi.Naomba unieleze jee nimefanya makosa au yeye ana makosa?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu kwa swali lako hilo. Mas-ala ya wanandoa ni nyeti sana na kwa mahusiano baina ya jamaa za mke au mume huenda ikaimarisha uhusiano huo au kuuvunja.

Katika swali lako umesema kuwa kaka yako huyo ni maharimu yako, lakini hukueleza ni kaka yako hasa au kaka kijamaa? Maana upo undugu aina nyingi. Huyo unayemuita ndugu anaweza kuwa kweli ni maharimu yako au si maharimu wako. Ikiwa atakuwa ni ndugu yako shakiki (baba na mama mmoja), au kwa baba mmoja au kwa mama mmoja basi hao wanakuwa ni maharimu zako. Lau undugu wenyewe utakuwa ni kwa sababu yeye ni mtoto wa shangazi yako, au halati yako, au mjombako au ami yako wote hao si maharimu zako. Sasa undugu wenu ni wa aina gani?

Katika maisha ya ndoa mume ana haki na wajibu wake kama vile mke ana haki na wajibu wake. Kila mmoja anafaa atekeleza haki za mwenziwe pamoja na wajibu wake ili ndoa iwe njema na yenye masikilizano. Mke ambaye ni mwema ni yule ambaye anatii amri ya mume wake na hamruhusu yeyote yule ambaye mume hamtaki pale. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Basi wanawake wema ni wale wenye kutii, wanaojihifadhi hata wasipokuwepo waume zao; kwa kuwa Allaah Amewaamrisha wajihifadhi” ().

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza:

Je, siwaambi hazina bora aliyonayo mwanamme? Ni mke mwema (mcha Mngu); ambapo anapomuangalia, anamfurahisha, na anapomuambia chochote, anamtii na anapokuwa hayupo nyumbani, anatizama (mke) maslahi ya mumewe” (Abu Daawuud).

Ni makosa kwa mke kuchukulia tu maadamu huyu ni ndugu yangu basi naweza kumuweka kwenye nyumba ya mume wangu hata akikataa. Mume amekuoa wewe na kumtendea wema ndugu yako ni hisani kutoka kwake japokuwa Uislamu unahimiza jambo kama hilo.

Tunashangazwa kuwa umesema huko Ulaya kuna shida, sasa vipi penye shida watu wapakimbilie? Huoni kuwa nyinyi wenyewe ndio mnaosababisha matatizo hayo a hata kuchangia kuvuruga ndoa zenu kwa mambo ambayo hayana umuhimu wala udharura?

Wewe kama mke inabidi sasa umtafute mumeo, japokuwa yeye kakuacha na watoto bila kutaka kujua maendeleo yenu wala hali zenu za kimaisha, ana makosa kwa sababu kama msimamizi wa nyumba alikuwa akuweke chini akufahamishe makosa yako na akuonye kabla hajachukua uamuzi kama huo. Kwa sasa kwa kuwa hayupo hapo mtafute kwa njia zote ili muweze kukaa chini kama mume na mke ili mtatue tatizo hilo. Katika kikao chenu hicho kikiamuliwa kuwa inafaa huyo ndugu yako atoke itabidi mufanye hivyo kwa maslahi mengi. Sisi kama Waislamu hatufai kufanya mambo kiholela holela kisha tuje tulaumu wengine.

Wewe una makosa zaidi kwa kutomtii mume wako na umechunga zaidi la kumridhisha ndugu yako jambo ambalo si sahihi kwa kuwa mume wako ndio bora zaidi kwako na wa kutiiwa zaidi kuliko ndugu yako. Hii haina maana usimsikilize ndugu yako au usimpende, bali umtii na umpende bila kudhulumu au kupandia kwenye mgongo wa mumeo.

Kila mmoja kati yenu ana makosa lakini kosa halitatuliwi na kosa jengine bali ni masikilizano mema na mazungumzo ya ukweli na uwazi.

Tunawaombea ufumbuzi wa tatizo hilo na masikilizano mema.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share