Zingatio: Jihisabu Kabla Hujahisabiwa

 

Zingatio: Jihesabu Kabla Hujahesabiwa

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ihisabu nafsi yako katika kila jambo hapa Duniani kabla ya kufariki na kabla ya kuhisabiwa Siku ya Malipo mbele ya Rabb. Kutengenea kwa tabia na amali zetu kutategemea namna Muislamu anavyozichunga amali zake kwa namna sawa na ilivyo kwa tajiri na biashara yake. Rasilimali ya tajiri huwa inachungwa, basi vivyo hivyo iwe kwa Muislamu kuchunga fardhi zake. Sunnah zote zitazame kama vile ni faida au nyongeza aipatayo tajiri kwenye biashara yake. Madhambi yahisabu vyema kwa mtazamo wa khasara na majuto makubwa katika biashara hii baina yako na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Muislamu anatakiwa akae kila kukicha na kwa muda mrefu ili atengeneze matatizo kwa kuihisabu nafsi yake kwa kila kitendo katika siku yake. Akae kwa kupiga hisabu aliyoyatenda kuanzia asubuhi hadi usiku, na akiona upungufu afanye upesi kulipa faradhi na afanye pupa ya nyongeza katika mambo ya Sunnah na mambo mengine yenye fadhila.

 

Khasara ya kupitwa na fadhila pamoja na faradhi ajutie mno fursa hiyo. Atubu haraka kutokana na kufanya maasi na madhambi kwa kuisawazisha nafsi yake na Rabb wake. Ajutie hali hiyo iliyompita na aendelee kila kukicha kufanya mema ili alipe yale aliyoyapoteza.

 

Hivyo ndivyo namna ya kuilea nafsi na kuielekeza katika njia iliyo sahihi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema katika Kitabu Chake: 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Hashr: 18]

 

Kwani nafsi ni kama mtoto mdogo mwenye madai na maombi ya kila namna yasio na kichwa wala miguu. Namna utakavyomlea ndivyo atakavyokua. Na nafsi haiamrishi jambo ila ni lenye uovu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

 إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ 

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu.. [Yuwsuf: 53]

 

Njia muafaka ya kuizuia nafsi kutenda maovu ni kujiweka karibu na Rabb kwa kuhisabu amali ulizozitenda kila siku. Hivyo, ni vyema tuzifanyie hisabu amali zetu kabla hatujahisabiwa na tuzifanyie wizani kabla hatujapimiwa.

 

Share