Pesa Anazopata Kwa Kuongopa Serikalini Zinafaa Kutumika Kwa Matumizi yake na kufanyia Mambo Ya Kheri?

 

SWALI:

As'alaikum.

Mimi ni kijana wa Kiafrica ninaeishi Ulaya na kama inavyofahamika kutokana na ugumu wa maisha ya nyumbani basi tunalazimika kukimbia ili angalau kutafuta njia itakayotukwamua na hali ya ngumu ya maisha.Sasa tunapofika huku Ulaya huwa tunajaribu kuongopa ili tupate hifadhi ya kuishi huku,hujaribu kudanganya kwa kusema tumekimbia vita au machafuko na mambo mengi yatakayoipa uzito hoja yangu ili nipate hifadhi,sasa mara unapopatiwa hifadhi huwa unalipwa pesa ili zikusaidie ktk masuala mbali mbali ikiwemo la kula,kuvaa na mengineyo. Ukweli ni kuwa tunatumia pesa hizo hizo kuwatumia wazee nyumbani ili angalau wapate pesa za chakula na kujitimizia mahitaji yao,Je hii pesa iliyotokana na mimi kusema uongo itaswihi pia kuitumia kununulia chakula ambacho mimi nitafturu??je itaswihi pesa hii kuitumia kusaidia watu na mimi nikapata thawabu?? Je pesa hii itaswihi kujengea Msikiti au Madrassa??

Ni mategemeo yangu makubwa umeelewa maudhui ya swali langu.  Ma'a salaam.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako, kwa hakika swali kama hili tayari tumelijibu kabla, lakini hapana ubaya kulielezea tena. Uislamu ni Dini iliyohimiza na kusisitiza sana kuhusu mas-ala ya ukweli. Zipo fadhila kubwa sana kwa mwenye kuwa na maadili kama hayo. Na yeyote asiyekuwa na tabia hiyo basi anaingia katika unafiki moja kwa moja.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119).

Amesema tena Aliyetukuka, “Na wasemao kweli wanaume na wanawake” (33: 35). Pia, “Utiifu na kauli njema. Na jambo likishaazimiwa, basi wakiwa ni wakweli kwa Allaah, bila ya shaka itakuwa ni kheri kwao” (47: 21).

Na Amesema tena Aliyetukuka: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na semeni maneno ya sawasawa (ya kweli). Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na Akusameheni madhambi yenu. Na anayemtii Allaah na Mtume Wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa” (33: 70 -71).

Na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kuwa wakweli kwa kutuambia:

Hakika ukweli unamuongoza mtu katika wema na wema unampeleka mtu Peponi. Na hakika mtu huendelea kusema ukweli mpaka akaitwa mkweli mbele ya Allaah. Na hakika uongo unampeleka mtu katika uchafu na uchafu unampeleka mtu Motoni. Na mtu huendelea kusema uongo mpaka akaandikwa kuwa ni muongo mbele ya Allaah” (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

Amesema tena Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka. Hakika ukweli ni utulivu na uongo unakera” (At-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ahmad na Isnadi yake ni Sahihi).

Na kauli ya Abu Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Hiraql kumuelezea sifa za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Muabuduni Allaah peke Yake wala musimshirikishe Yeye na chochote na muache wanayosema wazazi wenu na anatuamuru kusimamisha Swalah na kusema ukweli, kuwa watwahirafu na kuunganisha kizazi (kwa kuwasaidia jamaa)” (Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim).

Uongo una madhara mengi kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Makosa yote yanaweza kupatikana kwa Muumini ila ukosefu wa uaminifu na uongo” (Imaam Ahmad).

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Je, Muumini anaweza kuwa muoga?’ Akasema: ‘Ndio’. Akaulizwa tena: ‘Je, Muumini anaweza kuwa bakhili?’ Akajibu: ‘Ndio’. Akaulizwa tena: ‘Je, Muumini anaweza kuwa muongo?’ Akasema: ‘Hapana (haiwezekani)” (Imaam Maalik).

Anatuelezea tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

Watu aina tatu hawawezi kabisa kuingia Peponi. Mzee mkongwe mzinzi, mtu anayesema uongo na masikini mwenye kiburi” (Al-Bazzaar).

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Yeyote anayemuita mtoto akimwambia kuwa atampatia kitu na asimpatie, basi amesema uongo” (Imaam Ahmad).

Anasema tena: “Muumini hawezi kuwa na Imani kamili mpaka aache uwongo katika dhihaka na mijadala japokuwa katika mambo mengine yote” (Imaam Ahmad).

Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaripoti kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtu anaendelea kusema uongo mpaka doa jeusi linawekwa katika moyo wake na polepole linaendelea kukua mpaka moyo wote unakuwa mweusi. Wakati huo jina lake linaingizwa katika orodha ya waongo mbele ya Allaah” (Imaam Maalik).

Uislamu umehimiza ukweli na uongo unampeleka mtu pabaya hapa duniani na kesho Akhera.

Hivyo hakuna kipengele cha wewe kusema uongo katika mas-ala hayo. Sema ukweli na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakutolea njia nyengine za riziki. Kwani Yeye Amesema:

Na anayemcha Allaah humtengezea njia ya kutokea. Na Humruzuku kwa njia asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah kajaalia kila kitu na kipimo chake” (65: 2-3).

Kwa kuwa jambo hili lishatokea ikiwa ni kwa kujua au kutojua. Ikiwa ni kwa kutojua inakuwa sahali kwani Allaah Aliyetukuka Anasema:

Toba inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi. Hao ndio Allaah huipokea toba yao. Na Allaah ni Mjuzi na Mwenye hekima” (4: 17).

Toba isiyokubaliwa ni ile ya mtu anayefanya maovu mpaka mauti yakakaribia, hapo ndipo akasema: Mimi nimetubia sasa. Hali hii ya pili inamfikisha mtu huyo pabaya sana.

Lakini katika hili swali inaonyesha raghba na azma kubwa ya ndugu yetu kutaka kujua uhakika wa anayopata katika masurufu kwa kuongopa na hivyo kutaka kurudi kwa Mola wake. Hiyo ndio njia ya kuwa na azma ya kutorudia tena kosa, kujuta na kurudi kwa Mola kwa kufanya mambo mema. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Hakika mema hufuta maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka” (11: 114).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema: “Mche Allaah popote ulipo, na ufuatilize jambo baya kwa jema litafuta hilo baya na utangamane na watu kwa tabia nzuri” (Ahmad, at-Tirmidhiy na ad-Daarimiy, nayo ni Hadiyth Sahihi).

Jambo ambalo unafaa ufanye sasa, wakati huu ukiwa mzima, mwenye siha na nguvu ni kufanya mambo ya kheri mengi zaidi. Jitoe katika jambo hilo la kuchukua hizo pesa kuanzia wakati huu kwa njia ambayo hawatashuku lolote wala chochote. Lau itakuwa haiwezekani hivyo basi utaendelea kuchukua lakini usiwe unatumia kunufaika wewe wala wale wanaokutegemea moja kwa moja. Unapoichukua unatakiwa uitoe kwa wengine na usitarajie malipo yoyote kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Ikiwa hiyo akiba uko nayo basi unaweza kuitoa sadaka kwa njia moja au nyengine hasa kwa wale walioko sehemu ya nyumbani Afrika Mashariki ambao wapo katika hali mbaya. Unaweza kuwasaidia wasiojiweza kwa kulipa karo zao za shule, kusaidia masikini au waliosilimu na wako katika shida.

Pesa hizo huwezi kuzitumia kwa kujengea Msikiti au Madrasah lakini unaweza kusaidia katika kuchimba kisima au choo au jambo jingine lolote la kusaidia jamii. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri” (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]). Lililobaki ni wewe kujaribu kutafuta kazi ya halali ili uwe unapata chumo la halali la kukuwezesha kujikimu kimaisha. Bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakupatia tawfiki kwa hilo.

Allaah Aliyetukuka kwa kuwa Anatuonea huruma sana sisi hutufutia yaliyopita, hivyo ni juu yetu kuganga yajao. Anasema: “Allaah Amekwisha yafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Allaah Atamuadhibu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu” (5: 95).

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka kwa majina Yake Matukufu Akusamehe na Akupe moyo na tawfiki ya kutorudia hayo tena katika maisha yako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share