Anapewa Pesa Na Serikali, Je, Mume Hapasi Kumhudumia Ikiwa Ni Hivyo?

SWALI:

 

Asalam alekum. Naomba kuuliza suali ni sawa kama tuko ulaya waume zetu kuwa wasema tuna pesa zetu twapawa na sirkali kwa hivo mume hana haki yakukutizama kukupa masrufu hatakama unashida pesa haikotoshi ni sawa kweli naomba munijibu kwa sababa sio mimi peke yangu kuna wenzangu wengi wana shida hio hapa ulaya shukran.

 JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupewa masrufu na mumeo. Mara nyingi katika jamii yetu ya Waislamu wanawake hunyanyasika na kunyanyaswa kwa sababu moja au nyengine. Mbali na kuwa Dini ya Kiislamu imemlinda sana mwanamke ili asiwe ni mwenye kunyanyaswa.

Wanaume huwa wanachukua fursa kwa kuwa wanawake wetu hawana maalumati ya Kidini huwa ni rahisi sana kupoteza haki zao. Inatakiwa ieleweke kuwa wanawake wana haki sawa na wanaume kwa nyanja kadhaa. Ni jukumu la mume kumpatia mkewe malazi, chakula, nguo, matibabu na mengineo, ikiwa mke ni tajiri au masikini. Jukumu hilo haliondoki kwa mume hata kama mke anapata kipato kikubwa zaidi. Anachopata mke ni chake na cha mume ni cha wote, lakini mke kwa ridhaa yake bila kulazimishwa akitaka kumsaidia mumewe hakatazwi na Dini kufanya hivyo na atapata thawabu kwa hilo.

 

Hata hivyo tuelewe kuwa, kwanza, ni vipi mwanamke ana pesa zake? Vipi serikali impatie mwanamke pesa na hali ana mume na mume anafanya kazi? Bila shaka hapo ima kuna njia zisizo halali zimetumika za kupata chumo hilo, au kuna udanganyifu wa kudanganya serikali hiyo na kutoa madai kama ambayo tunayasikia ya kuwa mwanamke anakwenda kudai serikalini kuwa hana mume na hali anaye, au kujiita 'single mother' na serikali kumpatia masurufu yake kila wiki, na ikamlipia na nyumba, na bado ikampa na pesa za kumhudumia mtoto/ watoto wake.

Hakika njia hizo ni mbaya, za dhuluma na chafu. Mbaya kwa sababu kunatumika uongo kupata maslahi hayo, Dhuluma kwa sababu unapokea usichostahiki na hivyo kuchukua kwa dhuluma. Chafu kwa sababu ya kuikataa ndoa yako na kudai uko peke yako na hali una mume, na isitoshe Uchafu zaidi waja kwa sababu kila mara mwanamke huyo huyo wa Kiislam, tena labda na Hijaab yake, anaonekana na akiwa na mimba na kisha kuzaa na hali kasema yeye ni 'single mother' au hana mume! Hakika huko ni kuutukanisha Uislam, na kuchafua jina la Dini yetu safi. Inaleta picha kwa makafiri kuwa wanawake wengi wa Kiislam ni Malaya pamoja na mahijaab yao wanayovaa.

Kosa hilo kwanza kabla ya yote linamwendea mume, mume kwa kuruhusu mkewe kuchukua pesa hizo serikalini kwa udanganyifu na madai ya kuwa si mkewe, na utakuta hata mume anaogopa kukaa au kulala kwenye nyumba hiyo ya mke wake kwa sababu serikali inatambua kuwa hiyo ni nyumba ya mwanamke 'single mother' na wakimkuta mwanaume humo, huenda wakapata mashaka na hata kumkatia huyo mwanamke pesa wanazompa na malipo ya kodi ya nyumba wanayomlipia kila wiki. Mwanaume wa namna hiyo, ni mwanaume mchafu, asiye na ghera, asiye na Iymaan, na hata asiye na maadili wala khofu kwa Mola wake.

Hali kadhalika, wanawake wengine waliokwenda kwenye nchi hizo za Ulaya na kuweza kupata nyumba na kipato cha bure serikalini, na wakawa wanaendelea kupata chumo hilo la haraam hata baada ya kupata waume wa kuwaoa, bado wanaendelea kuchukua pato hilo ilihali waume zao wanaweza kuwahudumia kwa kila kitu. Hao ni wenye makosa makubwa kwa tamaa zao hizo ambazo huenda zikawapeleka kwenye adhabu kali ya Mola wao. Na waume hao dhaifu wenye kupenda maslahi na kubana matumizi na kukwepa kulipa kodi za nyumba, ndio wamekuwa wakiyafurahia maisha hayo wakiona kuwa wanaweza kubana matumizi na kutogharamika sana. Matokeo yake tumesikia wanaume wengi wamefukuzwa na wake zao kwenye hizo nyumba kwa sababu mwanamke ndiye mwenye kumiliki nyumba na kulipiwa na serikali. Ndio kumekuwa na mtindo wa kutimuliwa waume kwenye nyumba na wake zao kwa sababu wake ndio wenye kujulikana na serikali kuwa ndio wenye hizo nyumba. Hii ni fedheha kubwa na aibu na udhalilishwaji kwa waume hao wasiomuogopa Allaah.

Tunawasisitiza nyote, mke, na mume, mubadilishe maisha yenu haraka, na muachane na hizo tamaa za kidunia zitakazowapeleka pabaya hapa duniani na kesho Akhera.

Mwanaume arejee kwenye Uislam wake na atekeleze maamrisho ya Dini yake ambayo yanamtaka awe ni msimamizi kamili wa nyumba yake, kuanzia kulipa kodi ya nyumba, kuilisha na kuivisha na kuitibu familia yake, pamoja na majukumu mengineyo yanayompasa yeye. Na awe na uchungu kuona mkewe analishwa na makafiri, na kuhifadhiwa na makafiri. Pia aone vibaya na achukizwe zaidi kuona mkewe anajulikana kama Malaya kwa kuzaa watoto bila mume. Hilo tu hakika latosha kumfanya mume mwenye chembe cha Iymaan na Uislam, kupinga kwa nguvu jambo hilo la mkewe kulishwa na kuhifadhiwa na serikali.

Na mke aone vibaya kuendeleza uongo na kujidhalilisha na kujitukanisha kwa makafiri na kuutukanisha Uislam wake.

Rejeeni kwa Mola wenu na mumche Yeye. Kwani Yeye ni Mwenye Kuona na ni Mwenye Kusikia Yote na Mjuzi wa yote muyafanyayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share